I&M Bank yapanda miti 400 ya matunda katika shule 10 za Temeke
Muktasari:
- Lengo la mradi huo ni kuweza wanafunzi kuwa na uelewa wa uhifadhi na utunzaji wa mazingira.
Dar es Salaam. I&M Bank Tanzania imepanda miti 400 ya matunda katika shule 10 za msingi za Manispaa ya Temeke ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uhifadhi wa mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Mpango huo umehusisha wafanyakazi wa benki, wateja, wadau mbalimbali pamoja na Shirika la Africa Transformational Initiative (ATI), ambapo walishiriki kupanda miti ya matunda kupitia programu ya One Tree Initiative inayotekelezwa na benki hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Sheria na Kiongozi wa Uendelevu wa I&M Bank Tanzania, Maria Gonsalves amesema benki hiyo inaona uendelevu kuwa sehemu ya msingi wa kujenga thamani ya muda mrefu kwa jamii.
"Kupanda miti ya matunda ni uwekezaji wa muda mrefu unaolenga kuboresha mazingira ya shule, kuongeza lishe kwa wanafunzi na kuwajengea utamaduni wa kutunza mazingira kwa vizazi vijavyo," amesema Gonsalves.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Africa Transformational Initiative (ATI), Wisdom Robert Mande amesema ushirikiano wao na I&M Bank Tanzania umeendelea kuzaa matunda katika utekelezaji wa miradi ya mazingira.
Amesema baada ya mafanikio ya kupanda zaidi ya miti 20,000 ya mikoko Kigamboni mapema mwaka huu, mradi wa Temeke unalenga kuwahamasisha wanafunzi kuwa walinzi wa mazingira na mabalozi wa maendeleo endelevu.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu na Mkurugenzi Mtendaji wa I&M Bank Tanzania, Zahid Mustafa amesema benki hiyo inaamini maendeleo endelevu yanapatikana kupitia uwekezaji unaowanufaisha wananchi na kulinda mazingira.
Amesema miti hiyo 400 itachangia kuboresha mazingira ya kujifunzia, kuhifadhi mazingira na kuacha urithi wenye manufaa kwa jamii zinazozunguka shule hizo.
Kwa mujibu wa I&M Bank Tanzania, miti ya matunda husaidia kufyonza hewa ya ukaa, kuboresha ubora wa hewa, kupunguza mmomonyoko wa udongo, kuongeza bioanuwai na baadaye kutoa matunda yanayoweza kuboresha lishe ya wanafunzi.
Mpango huo unaendana na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, hususan SDG 13 kuhusu hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, SDG 15 kuhusu uhifadhi wa mazingira ya nchi kavu na SDG 3 kuhusu afya bora na ustawi.