Katibu tawala Kilimanjaro awaonya madiwani 'wekeni maslahi ya wananchi mbele'
Muktasari:
- Ufupi:Baraza hilo lenye madiwani 43, wakiwamo wa kuchaguliwa kutoka Kata 32 pamoja na viti maalum, madiwani walimchagua Diwani wa Njiapanda John Meela kuwa Mwenyekiti na Diwani wa Mwika Kaskazini, Samuel Shao, kuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri.
Moshi. Wakati Madiwani wa Halmashauri ya Moshi wakila kiapo na kumchagua Mwenyekiti na makamu wa Halmashauri hiyo , Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa, amewataka madiwani kuweka maslahi ya wananchi mbele katika maamuzi na majukumu yao ya kila siku, akisisitiza kuwa dhamana waliyopewa ni ya kuwatumikia wananchi, si vinginevyo.
Baraza hilo lenye madiwani 43, wakiwamo wa kuchaguliwa kutoka Kata 32 pamoja na viti maalum, madiwani walimchagua Diwani wa Njiapanda John Meela kuwa Mwenyekiti na Diwani wa Mwika Kaskazini, Samuel Shao, kuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri.
Nzowa ametoa Rai hiyo leo Desemba 3, 2025, kwenye kikao maalumu cha Baraza la madiwani,Halmashauri ya Moshi, ambapo amesema jukumu kuu la madiwani ni kusimamia na kuishauri ipasavyo menejimenti ya halmashauri, hivyo hawapaswi kusita kutoa ushauri, kufuatilia na kudai uwajibikaji pale inapohitajika.
“Ndugu zangu Madiwani, mpo hapa kwa ajili ya wananchi. Kila mtakachokifanya, kiwe kwa maslahi ya wananchi waliowapa dhamana. Msisite pale ambapo mnatakiwa kusimamia na kuishauri menejimenti ya halmashauri.” amesema Nzowa.
Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Moshi wakila kiapo
Audha amesisitiza kuwa usimamizi madhubuti wa mapato ya halmashauri uwe agenda ya kudumu katika vikao vyao, kwa kuwa mapato ni moyo wa Halmashauri na nguzo kuu ya utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
“Mapato ni moyo wa halmashauri. Ili tuwahudumie wananchi ipasavyo lazima tuwe na mapato ya kutosha. Nendeni mkabuni mikakati ya kuongeza mapato na kuhakikisha yanakusanywa kikamilifu,” ameongeza.
Kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Nzowa amesema madiwani wana wajibu wa kufuatilia na kusimamia miradi inayotekelezwa katika maeneo yao ili ikamilike kwa wakati, kwa viwango na bila ubabaishaji.
Aidha, amewataka madiwani kushirikiana na menejimenti kusimamia nidhamu na uwajibikaji wa watumishi, akisema watumishi wasiowajibika wanapaswa kuchukuliwa hatua ili huduma kwa wananchi zisikwame.
Katika maeneo ya utawala, Nzowa amewakumbusha madiwani kuhakikisha vikao vya kisheria kuanzia ngazi ya kata, vijiji na vitongoji vinafanyika kwa wakati na kutoa nafasi kwa wananchi kusikilizwa na kupata ufumbuzi wa kero zao.
Amesisitiza pia umuhimu wa ajenda ya ulinzi na usalama kuwa ya kudumu, akiwataka madiwani kutoa elimu kwa wananchi kuhusu thamani ya amani na kuchukua hatua mapema pale panapoonekana viashiria vya uvunjifu wa amani.
“Mnakumbuka Oktoba 29 kulikuwa na baadhi ya maeneo ambayo kulitokea vurugu. Kilimanjaro hakukuwa na changamoto lakini naomba agenda ya ulinzi na usalama iwe ya kudumu katika maeneo yenu na mtoe elimu kwa wananchi kuwa amani ni tunu ya taifa letu na mnapoona viashiria vya uvunjifu wa amani mtoe taarifa ili hatua zichukuliwe mapema kudhibiti hali hiyo".
Nzowa ametumia pia nafasi hiyo,kuwahimiza madiwani kujisomea majarida, kanuni na sheria mbalimbali ili kuongeza uelewa na uwezo wa kuchangia hoja zenye tija zitakazosaidia kusogeza mbele maendeleo ya halmashauri zao na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla.
Akizungumza mwenyekiti wa halmashauri hiyo, John Meela, ameahidi kuimarisha umoja, ushirikiano na kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa usawa katika kata zote bila ubaguzi.
Meela amesema pia atashirikiana na Mkurugenzi pamoja na timu ya watendaji kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza uwezo wa Halmashauri kutekeleza miradi ya maendeleo.
“Ninawaomba umoja na ushirikiano ili tuwatumikie wananchi waliotupa dhamana. Niwahakikishieni kuwa kila kata itapata mradi wa maendeleo bila ubaguzi. Pia tutabuni miradi mipya ya kuongeza mapato ya Halmashauri,” alisema Meela.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti, Samuel Shao amewashukuru madiwani kwa kuwapa imani na kuahidi kushirikiana na mwenyekiti katika kufanikisha malengo ya maendeleo kwa wananchi wa Moshi.
Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Moshi wakila kiapo
"Niwashukuru madiwani kwa kutuamini na kutupa nafasi ya kuwaongoza. Nitamshauri vizuri mwenyekiti. niombe madiwani mtupe ushirikiano ili kuwezesha yale ambayo tumekusudia kuyafanya katika Halmashauri yetu yafanyike na wananchi wapate maendeleo"amesema Shao.
Diwani wa viti maalumu Asia Kimaryo amesema atashirikiana na madiwani kuhakikisha mikopo ya halmashauri inawafikia wanawake wengi zaidi na kwa wepesi,ili kuwawezesha kuondokana na mikopo umiza ikiwemo kausha damu.
Aidha, Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini, Ramadhan Mahanyu, amewataka madiwani kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia kiapo chao na kufanya kazi kama timu, akisisitiza kuwa “sisi ni familia moja.”