Kesi ya mauaji ya Rhoda yaahirishwa, upelelezi waendelea
Washatakiwa wa kesi ya mauaji ya Rhoda Mobe, wakiingia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma kwaajili ya kesi yao kutajwa. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
- Rhoda ambaye alikuwa ni mkulima na mkazi wa Kijiji cha Burunga wilayani Serengeti mkoani Mara anadaiwa kuuwawa Oktoba 23, 2025 majira ya usiku baada ya kuvamiwa nyumbani kwake kijijini hapo.
Musoma. Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma imeahirisha kesi ya mauaji inayowakabili washtakiwa watatu wanaotuhumiwa kumuua Rhoda Mobe (42), mkazi wa Kijiji cha Burunga wilayani Serengeti, mkoani Mara.
Kesi hiyo namba 23/12/2025 imeahirishwa hadi Aprili 13, 2026, baada ya upande wa mashtaka kueleza kuwa upelelezi bado haujakamilika na unahitaji kufanyika kwa kina zaidi ili kukusanya ushahidi wa kutosha.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Simon Ruhinda (55), muhudumu wa ofisi katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Marco Maginga (45), mwalimu wa shule ya msingi jijini Mbeya na Mwita Maginga (47), mkulima mkazi wa Tarime.
Akitoa uamuzi huo leo Jumanne Machi 31, 2026, Hakimu Mkazi Mkuu, Eugenia Rujwahuka alisema upelelezi wa shauri hilo una mlolongo mrefu na unahusisha pia makosa ya kimtandao, hivyo unahitaji muda zaidi ili kukamilika.
“Upelelezi bado unaendelea na unahitaji kufanyika kwa kina, hasa kutokana na kuhusisha masuala ya ‘cyber crime’, hivyo kesi imeahirishwa hadi Aprili 13 kwa ajili ya kutajwa,” alisema.
Awali, Wakili wa Serikali, Joyce Matimbwi aliieleza mahakama kuwa upelelezi haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo.
“Washtakiwa wote wapo mahakamani na upelelezi bado unaendelea, hivyo tunaomba tarehe nyingine,” alisema.
Akizungumza baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, wakili anayefuatilia mwenendo wa shauri hilo, Linus Amri alisema kutokana na uzito wa tukio hilo, ni muhimu upelelezi ufanyike kwa kina ili haki iweze kutendeka kwa pande zote.
Alisema tukio hilo lilivuta hisia za watu wengi kutokana na ukatili wake, hivyo ni lazima ushahidi wa kutosha upatikane ili kubaini ukweli wa jambo hilo.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa hao wanadaiwa kumuua Rhoda Mobe kwa kumkata kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake baada ya kuvamia nyumbani kwake usiku wa Oktoba 23, 2025.
Inadaiwa walitenda kosa hilo kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu. Kesi hiyo haina dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi haina mamlaka ya kuisikiliza hadi itakapopelekwa Mahakama Kuu.
Washtakiwa wote wamerudishwa rumande wakisubiri hatua zaidi za kisheria.