Kikwete: Sitamzuia mke wangu kufanya kazi ya siasa
Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete akizungumza na wananchi wa Mchinga wakati akimuombea kura mgombea ubunge wa Jimbo la Mchinga Salma Kikwete.
Muktasari:
- Salma Kikiwete anaomba ridhaa kwa mara nyingine kutoka kwa wananchi ya kulitumikia jimbo Mchinga kwa miaka mitano ijayo.
Lindi. Rais mstaafu, Jakaya Mrisho Kikwete, amesema hana pingamizi lolote kwa mkewe, Salma Kikwete kuendelea kufanya kazi za uwakilishi bungeni.
Amewataka wananchi wa Jimbo la Mchinga, lililopo mkoani Lindi, kumpigia kura ili aendeleze alipoishia katika kipindi kilichopita. Salma amelitumikia jimbo hilo kwa miaka mitano kuanzia 2020 hadi 2025.
Kikwete amesema hayo leo Jumapili, Septemba 7, 2025, wakati wa uzinduzi wa kampeni za Chama cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Mchinga uliofanyika katika Uwanja wa Rutamba, mkoani Lindi.
“Mimi sina tatizo na mke wangu Salma Kikwete. Nimevumilia miaka mitano na safari hii tena nitavumilia. Namuacha aendelee na kazi zake za ubunge ili awatumikie wananchi wa Mchinga,” amesema Rais huyo mstaafu.
Amewaomba wananchi wa jimbo hilo, ikifika Oktoba 29, 2025, wampigie kura Mama Salma ili amalizie changamoto zilizobaki na kuwatumikia wananchi kwa ufanisi zaidi katika kipindi cha miaka mingine mitano ijayo.
Kikwete pia amewaomba wananchi waendelee kumuunga mkono mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, pamoja na wagombea wote wa chama hicho kuanzia ngazi ya ubunge hadi udiwani, ili waendeleze miradi na mipango ya maendeleo iliyoanzishwa na inayotarajiwa kuanzishwa kwa maendeleo ya Tanzania.
Kwa upande wake, Mama Salma amewaomba ridhaa wananchi kusudi aendelee kulitumikia jimbo hilo, akiahidi kushughulikia changamoto za maji katika vijiji na vitongoji, kuboresha barabara na kuongeza kituo cha afya katika eneo la Rutamba.
“Niwaombe wananchi wenzangu muendelee kuniamini kwa kunipa kura, ili tumalizie kazi tulizoanza na kuondoa changamoto tulizonazo ndani ya miaka mitano ijayo,” amesema.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akifungua kampeni hizo, amewahimiza wananchi wa Mchinga kuichagua CCM katika nafasi zote, akisisitiza kuwa uongozi wa chama hicho ndio utakaowaletea maendeleo.
“Kuna mradi mkubwa wa reli ya kisasa ya ukanda wa kusini kutoka Mtwara, kupitia Songea hadi Liganga na Mchuchuma, ambao Rais Samia atautekeleza. Hivyo tunapaswa kumpa kura nyingi ili aendelee kuleta maendeleo katika Taifa letu,” amesema Majaliwa.