Lindi yaibua mjadala wa Upandaji Miti kuelekea siku ya misitu duniani
Muktasari:
- Lindi yaendelea na maadhimisho ya siku ya misitu duniani kupitia jukwaa la biashara kwa biashara (B2B).
Lindi. Kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani sambamba na Kampeni ya Kitaifa ya Upandaji Miti, Mkoa wa Lindi umeanzisha mjadala mpana wa wadau kupitia Jukwaa la Biashara kwa Biashara (B2B).
Akifungua mjadala huo leo Machi 18, 2026 Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, amesema kuwa lengo kuu la mdahalo huo ni kubaini njia bora zitakazomwezesha binadamu kuishi kwa ustawi bila kusababisha uharibifu wa mazingira.
Amesisitiza kuwa huu ni wakati muafaka wa kujadili kwa kina mchango wa sekta ya misitu katika kukuza pato la taifa pamoja na kuimarisha juhudi za uhifadhi.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, akizungumza wakati akifungua mjadala huo
"Sekta ya misitu ni mhimili muhimu kwa maendeleo ya nchi, ikichangia takribani asilimia 3 ya pato la taifa. Pia ni chanzo kikuu cha nishati, dawa, na nyenzo muhimu katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.amesema Telack
Amebainisha kuwa juhudi hizo zinahitaji kuungwa mkono na wananchi ili kuhakikisha rasilimali hizo zinaendelea kunufaisha kizazi cha sasa na kijacho.
Aidha, Telack ametoa wito wa kuimarishwa kwa utoaji wa elimu endelevu kwa wananchi kuhusu sera, kanuni na taratibu zinazosimamia sekta ya misitu na wanyamapori, Lengo ni kuhakikisha shughuli zote zinafanyika kwa kuzingatia sheria, bila kuathiri uhifadhi, na hivyo kuwawezesha wananchi kunufaika kiuchumi huku wakichangia katika kulinda na kuhifadhi mazingira yao.
Baadhi ya wananchi waliokuwa katika mjadala huo wa upandaji miti kuelekea siku ya misitu duniani
Hata hivyo watoa mada wamehimizwa kuangazia fursa mpya za kiuchumi, zikiwemo biashara ya kaboni pamoja na matumizi ya teknolojia katika sekta ya misitu,hii inalenga kuwawezesha wananchi kupata taarifa sahihi,zitakazowaongoza kujipanga na kushiriki kikamilifu katika masoko hayo.
Kwa upande Mkufunzi kutoka Chuo Cha Misitu na Viwanda Mafinga (FWITC) Said Omary amewataka wananchi kujifunza aina za miti ya mbao ambapo watu wengi wamekuwa wakiitumia katika kufanya biashara za mbao napia itasaidia kulinda miti ya asili.
Omary amesema kuwa baadhi ya miti ambayo wananchi hawaijui na inaweza kisaidia kutengeneza vifaa ya samani kama mti wa mtundu ,mti wa kipepe,mti wa mchenyele,mti wa mlapwezi pamoja na mti wa mesala.
"Wananchi wanatakiwa kujifunza aina mbalinbali za miti ambapo kunabaadhi ya miti ambayo imefanyiwa uchunguzi inafaa katika biashara ya mbao na kuacha miti ya asili."amesema Omary.