Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Machinga: Amani ndiyo msingi wa biashara zetu

Muktasari:

  • Wito umetolewa kwa vijana nchini kuepuka kurubuniwa kushiriki katika vurugu, wakisisitiza umuhimu wa kujikita katika shughuli za kiuchumi zinazojenga maisha yao na familia zao.

Dar es Salaam. Amani imetajwa kuwa nguzo kuu ya ustawi wa jamii na maendeleo ya kiuchumi, huku wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga wa Wilaya ya Kinondoni na eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam wakisisitiza kuwa bila utulivu hakuna biashara wala maisha endelevu ya familia.

Katika msimamo huo, machinga hao wametangaza kutoshiriki maandamano yanayopangwa kufanyika Julai 7, 2026, wakisema kipaumbele chao ni kulinda amani ya nchi na kuendeleza shughuli zao za kila siku bila usumbufu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Machinga Wilaya ya Kinondoni, Palejia Mushi, wamesema wameamua kujitenga na maandamano hayo kutokana na hofu ya athari za kiuchumi na kijamii zinazoweza kujitokeza endapo kutatokea vurugu.

Mushi amesema machinga wengi wamejifunza kutokana na matukio ya nyuma yaliyosababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara wadogo, ikiwemo kupoteza mali, kuharibika kwa mitaji na kusimama kwa shughuli za biashara.

“Tunawahimiza machinga na vijana wote kutokubali kushawishiwa kushiriki maandamano. Amani yetu ni msingi wa biashara zetu. Bila amani hatuwezi kufanya kazi wala kuendesha familia zetu,” amesema.

Kwa upande wake, mfanyabiashara wa soko la Mwenge, Tumaini Ulotu, amesema wafanyabiashara hao wamekubaliana kwa kauli moja kutoshiriki maandamano hayo, wakisisitiza kuwa hawataki kurudia madhara yaliyowahi kujitokeza katika matukio ya vurugu za nyuma.

Amesema matukio hayo yaliwaathiri kwa kiasi kikubwa, ambapo wengi walipoteza mitaji yao na wengine kukosa kipato kutokana na kusimama kwa shughuli za usafiri na biashara.

Wafanyabiashara hao wamesisitiza kuwa njia sahihi ya kutatua changamoto ni kupitia majadiliano ya amani na si maandamano yanayoweza kuhatarisha utulivu wa nchi.

Aidha, wametoa wito kwa vijana nchini kuepuka kurubuniwa kushiriki katika vurugu, wakisisitiza umuhimu wa kujikita katika shughuli za kiuchumi zinazojenga maisha yao na familia zao.