Prime
UCHAMBUZI WA MJEMA: Tukubali au tukatae, maandamano yamewekewa utaratibu
Julai 7, 2026, ambayo ni siku ya mapumziko ya umma, imepangwa kuambatana na Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), tukio ambalo mwaka huu linaadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake kama Jubilei ya Dhahabu.
Ni maonesho yanayotarajiwa kuvutia zaidi ya wafanyabiashara 3,500 na wageni zaidi ya 550,000, yakibeba ajenda kubwa za biashara za kimataifa, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi kati ya sekta ya umma na binafsi.
Kwa kawaida, Sabasaba ni jukwaa la kiuchumi lenye uzito mkubwa katika kalenda ya biashara ya taifa na ukanda kwa ujumla.
Hujikita katika kuimarisha mitandao ya biashara ya kimataifa, kuonyesha fursa za uwekezaji na kutoa nafasi kwa taasisi za serikali na sekta binafsi kuwasilisha huduma na bidhaa zao kwa umma na wageni kutoka mataifa mbalimbali.
Hata hivyo, katika mazingira ya mwaka huu, kumetokea mjadala mpana kufuatia wito unaosambazwa kupitia mitandao ya kijamii ukihamasisha kufanyika kwa maandamano ya nchi nzima siku hiyo hiyo ya Julai 7.
Wito huo ambao haujatolewa na taasisi rasmi au chama cha siasa kilichosajiliwa kuongoza maandamano hayo, umeibua tahadhari na wasiwasi kuhusu uwezekano wa kuvuruga shughuli muhimu za kiuchumi na kijamii.
Ni muhimu kueleza kuwa, hadi sasa hakuna chama cha siasa au taasisi rasmi nchini iliyotangaza kuandaa maandamano hayo, bali yanatajwa kuenezwa zaidi kupitia majukwaa ya kidijitali kama X, Instagram na TikTok.
Hali hii imefanya mjadala huo kuingia katika eneo nyeti la uhalali wa maandamano na uzingatiaji wa sheria za nchi.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 20(1), kila mtu ana haki ya kukutana, kujumuika na kutoa maoni yake kwa amani, bila kuathiri sheria za nchi.
Haki hii pia imewekewa misingi katika Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu (African Charter on Human and Peoples’ Rights wa 1981), unaoruhusu haki ya kukusanyika huku ukitoa nafasi ya vizuizi vya kisheria kwa maslahi ya usalama wa taifa.
Hata hivyo, haki hiyo ya kukusanyika na kuandamana inategemea pia kufuata taratibu za kisheria zilizowekwa. Kwa Tanzania, waandaaji wa maandamano wanatakiwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi angalau saa 48 kabla ya tukio, likiwa na maelezo ya mahali, muda, njia na ajenda ya maandamano hayo.
Kwa mujibu wa kifungu cha 11(4) na (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2019, Polisi wana wajibu wa kupokea taarifa hizo na kutoa uamuzi wa kuruhusu au kuzuia kwa misingi ya kiusalama.
Katika muktadha huo, hoja inayojitokeza ni nani hasa aliyeandaa maandamano ya Julai 7, ni wapi taarifa rasmi imewasilishwa, ni njia gani zitakazotumika, na ni wapi maandamano hayo yatakomea.
Ukosefu wa majibu ya maswali haya muhimu unazua mjadala kuhusu uhalali na uhalisia wa wito huo unaosambazwa mitandaoni.
Mazingira haya pia yameibua hisia za kisiasa, ambapo baadhi ya viongozi wa chama tawala CCM wamewataka wananchi kutoshiriki maandamano hayo, wakihusisha wito huo na hujuma za kisiasa.
Hata hivyo, upande mwingine wa mjadala unasisitiza umuhimu wa kusikiliza na kuchambua hoja zinazotolewa badala ya kuzibeza moja kwa moja.
Kwa mtazamo wa kisheria na kiusalama, maandamano yasiyofuata utaratibu wa kisheria yanaweza kupoteza uhalali wake na kusababisha changamoto kwa vyombo vya dola katika kudhibiti usalama wa raia na mali zao.
Lengo la taarifa ya awali kwa polisi si kukandamiza haki, bali ni kuwezesha ulinzi na kuzuia uwezekano wa watu au makundi kutumia mikusanyiko hiyo kufanya uhalifu.
Ni ukweli usiopingika kwamba maandamano ya amani hujengwa juu ya msingi wa haki na wajibu. Wakati wananchi wana haki ya kikatiba ya kuandamana, pia wana wajibu wa kuheshimu sheria zinazotawala utaratibu huo, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa mamlaka husika kabla ya kufanya mikusanyiko ya aina hiyo.
Julai 7 pia si siku ya kawaida katika kalenda ya taifa. Ni Siku ya Sabasaba, ambayo kila mwaka hujulikana na kutambulika kitaifa na kimataifa kama siku ya maonesho makubwa ya biashara. Ni siku ambayo serikali, wafanyabiashara na wageni wa kimataifa hujiandaa kwa muda mrefu kushiriki tukio hilo muhimu la kiuchumi.
Kwa mantiki hiyo, kuchagua siku hiyo hiyo kwa maandamano yasiyokuwa na utaratibu rasmi wa kisheria kunazua maswali ya msingi kuhusu uzingatiaji wa maslahi mapana ya taifa, hususan sekta ya biashara na uwekezaji.
Ni ukweli kwamba hakuna mtu anayependa kuona ukiukwaji wa haki za binadamu, kukosekana kwa demokrasia au uwepo wa ukandamizaji.
Hata hivyo, njia ya kutafuta mabadiliko haiwezi kuwa nje ya mfumo wa sheria uliowekwa na nchi. Kinyume chake, kufanya hivyo huweza kusababisha migogoro na hatari ya kuvunjika kwa amani.
Katiba ya nchi pia inaweka bayana misingi ya utawala wa sheria, ikisisitiza kwamba hakuna aliye juu ya sheria iwe ni serikali, viongozi au wananchi.
Hii ina maana kwamba kila hatua ya kijamii na kisiasa inapaswa kufanyika ndani ya mipaka ya sheria, si nje yake.
Hivyo, kama kuna hoja za msingi zinazoibuliwa na wanaotaka kuandamana, njia sahihi ni kupitia mifumo iliyopo ya kisheria: kuwasilisha taarifa, kupata kibali au zuio, kukata rufaa na hata kwenda mahakamani endapo kuna malalamiko ya kukiukwa kwa haki za kikatiba.
Kwa hatua hiyo, hoja zingetafutiwa majibu ndani ya mfumo wa sheria badala ya kuzalisha mgongano wa moja kwa moja na vyombo vya dola.
Kwa taifa ambalo limefikia hatua nyeti ya kisiasa na kijamii, ni muhimu zaidi sasa kusisitiza maridhiano, mazungumzo na uwajibikaji wa pande zote.
Serikali, wananchi na viongozi wa kisiasa wanapaswa kukaa pamoja kwa lengo la kutafuta suluhisho la pamoja badala ya kuingia kwenye mivutano inayoweza kuhatarisha mshikamano wa taifa.
Utawala wa sheria unamaanisha kuwa kila upande unapaswa kuheshimu sheria hizo hizo wanazozitumia kudai haki. Ni kwa njia hiyo pekee ndipo taifa linaweza kudumisha amani, mshikamano na maendeleo endelevu.
Daniel Mjema ni mwandishi wa habari na mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.