Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mallya aahidi kushughulikia changamoto ya umbali kwa wanafunzi

Mgombea udiwani wa Kata ya Karanga, Manispaa ya Moshi, Deogratius Mallya (kulia).

Moshi. Mgombea udiwani wa Kata ya Karanga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Deogratius Mallya, amewahakikishia wananchi kwamba atashughulikia changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda shuleni, endapo atachaguliwa kuwa diwani.

Akizungumza jana Septemba 28, 2025 wakati wa uzinduzi wa kampeni zake uliofanyika kata hiyo, Mallya amesema shule nyingi zipo mbali na makazi ya wananchi, jambo linalowalazimu wanafunzi kutembea hadi kilomita tano kila siku kwenda na kurudi shuleni.

“Hali hii inawaathiri kitaaluma, kwani hufika shuleni wakiwa wamechoka na mara nyingine huchelewa. Nitahakikisha tunapata suluhisho la kudumu ili watoto wetu wapate elimu katika mazingira rafiki,” amesema Mallya.

Amesema shule mpya itajengwa pembezoni mwa Chuo cha Ufundi Karanga, akibainisha kuwa ni mradi muhimu unaolenga kuinua kiwango cha elimu katika kata hiyo.

Aidha, Mallya ameahidi kuboresha miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami ili kuhakikisha zinapitika nyakati zote, jambo litakalorahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Karanga.

“Nawaahidi, endapo mtanirudisha madarakani, nitahakikisha barabara zote ndani ya kata zinaunganishwa kwa kiwango cha lami kwa kushirikiana na mamlaka husika,” amesema Mallya.

Mgombea huyo pia amesisitiza kuwa, “Naomba mnitume tena. Karanga mpya inawezekana sana. Tuliwapa wapinzani nafasi kwa miaka 15, lakini leo ukiuliza walichofanikisha, hakuna majibu ya kuridhisha.”

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, amewahakikishia wananchi kuwa, endapo atachaguliwa, atasimamia uwepo wa mwanasheria katika ofisi ya Mbunge atakayewasaidia vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupata elimu ya kisheria, mikopo ya halmashauri, na ushauri wa mikataba.

“Nataka niwaahidi, Oktoba 29 mkishanichagua, tutaweka mwanasheria katika ofisi ya Mbunge. Atakuwa msaada kwa vikundi vyote kuwaandikia mikataba, kuwashauri kisheria na kuwasaidia kupata mikopo,” amesema Shayo.

Kuhusu watu wenye ulemavu, Shayo amesema hatowalazimisha kujiunga na vikundi ili kupata mikopo, bali atahakikisha wanapatiwa fedha moja kwa moja.

Aidha, ameeleza nia yake ya kununua magari mawili aina ya Costa kwa ajili ya matumizi ya kijamii kama misiba na harusi, ambayo yatafanywa bila malipo kwa wananchi.

“Nitazinunua kwa fedha zangu mwenyewe. Baada ya Oktoba 29, mkishanipa kura za kutosha, mtakuwa huru kupiga simu ofisi ya Mbunge mnapokuwa na dharura yoyote, iwe ni harusi, msiba au mgonjwa. Magari haya yatakuja kuwasaidia bila gharama yoyote,” amesema Shayo.

Mgombea huyo amesisitiza kuwa lengo lake ni kuhakikisha ofisi ya Mbunge inakuwa sehemu ya msaada wa moja kwa moja kwa wananchi, hasa nyakati za uhitaji mkubwa.