Mara kugawa vyandarua milioni 1.5 kupambana na malaria
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni ya ugawaji wa vyandarua mkoani Mara ikiwa ni mkakati wa kutokomeza ugonjwa wa malaria mkoani humo. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
- Kaya zaidi ya 464,000 zinatarajiwa kunufaika; Mkuu wa Mkoa aonya watakaobadili matumizi ya vyandarua kuchukuliwa hatua.
Musoma. Serikali inatarajia kugawa vyandarua milioni 1.5 vyenye dawa ya kuua mbu waenezao malaria, vyenye thamani ya zaidi ya Sh22 bilioni, kwa wakazi wa Mkoa wa Mara katika jitihada za kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo.
Vyandarua hivyo vitagawiwa katika halmashauri saba za mkoa huo, huku kaya zaidi ya 464,000 zenye wakazi zaidi ya milioni 2.3 zikitarajiwa kunufaika na kampeni hiyo itakayokamilika Agosti 20, 2026.
Akizungumza leo Jumatatu Julai 13, 2026 mjini Musoma wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Mratibu wa kampeni ya kuzuia Malaria nchini kutoka Wizara ya Afya, Wilfred Mwafongo amesema mkoa wa Mara ni wa pili nchini kwa maambukizi ya malaria baada ya Kagera.
Amesema Mara ina kiwango cha maambukizi cha asilimia 22, ikifuatiwa na Kagera yenye asilimia 24, huku Iringa ikiwa na kiwango cha chini zaidi cha asilimia moja.
Baadhi ya wadau wakiwa kwenye uzinduzi wa kampeni ya ugawaji wa vyandarua mkoani Mara ikiwa ni mkakati wa kutokomeza ugonjwa wa malaria mkoani humo. Picha na Beldina Nyakeke
Kutokana na hali hiyo, amesema Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Tanzania Malaria Initiative (TMI), imeanzisha kampeni hiyo inayohusisha ugawaji wa vyandarua sambamba na utoaji wa elimu kuhusu matumizi sahihi ya vyandarua na matibabu stahiki ya malaria.
Halmashauri zitakazonufaika ni Musoma Vijijini, Bunda Vijijini, Butiama, Rorya, Serengeti, Bunda Mji na Tarime Vijijini.
Mwafongo amesema wananchi watapaswa kujisajili kupitia utaratibu maalumu utakaosimamiwa na halmashauri husika kabla ya kupewa vyandarua hivyo.
"Vyandarua vitatolewa bila malipo na vitawafikia wananchi wote, hata wanaoishi visiwani, mradi ni wakazi wa halmashauri husika," amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amewataka wananchi kuvitumia vyandarua kwa lengo lililokusudiwa na kuachana na tabia ya kuvitumia katika shughuli nyingine.
Amezitaka Kamati za Ulinzi na Usalama pamoja na Kamati za Huduma za Jamii na Maendeleo kuanzia ngazi ya vitongoji kusimamia utekelezaji wa kampeni hiyo na kuhakikisha vyandarua vinatumika ipasavyo.
"Kuna watu wanafuga kuku kwa kutumia vyandarua, wengine wanavitumia kwenye bustani za mboga au kuvulia dagaa. Hii ni hasara kwa Serikali na inakwamisha mapambano dhidi ya malaria. Wanaokiuka wachukuliwe hatua," amesema.
Pia amepinga dhana kwamba vyandarua vyenye dawa hupunguza nguvu za kiume, akieleza kuwa taarifa hizo hazina msingi wa kisayansi na kuwahimiza wananchi kupima malaria kabla ya kutumia dawa.
Kanali Mtambi amesema endapo kampeni hiyo itatekelezwa kwa ufanisi, Mkoa wa Mara unaweza kufikia lengo la kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2030.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Stanley Kajuna, amesema shughuli za uchimbaji madini na uwepo wa madimbwi mengi ya maji ni miongoni mwa sababu zinazochangia kiwango kikubwa cha maambukizi ya malaria mkoani humo.
Amesema mkoa pia umeanza kutumia dawa za kuua mazalia ya mbu, baada ya kupokea lita 23,000 za dawa kwa ajili ya kudhibiti mazalia hayo.