Mwaitebele: Madiwani epukeni kuwa chanzo cha migogoro, tangulize maslahi ya umma
Baadhi ya madiwani Manispaa ya Moshi,wakiwa kwenye kikao cha kwanza cha mkutano wa baraza la Madiwani
Muktasari:
- Mwaitebele ametahadharisha dhidi ya tabia zisizofaa, ambapo amesema haitarajiwi kuona diwani anakuwa chanzo cha migogoro katika Halmashauri au kwenye jamii yake.
Moshi. Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro,wametakiwa kuepuka kuwa chanzo cha migogoro katika maeneo yao ya kazi na badala yake wawe chachu ya utulivu, uwajibikaji na maendeleo kwa wananchi wanaowaongoza.
Rai hiyo imetolewa leo,Desemba 4,2025 na Katibu Msaidizi kutoka Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kaskazini, Gerald Mwaitebele, wakati akizungumza kwenye mkutano wa wa kwanza wa baraza la madiwani, Manispaa ya Moshi, akisisitiza umuhimu wa viongozi hao kutambua kuwa nafasi walizopewa ni dhamana na si fursa ya kujinufaisha.
Katika kikao hicho, Madiwani wamemchagua Diwani wa Kata ya Njoro,Zuberi Kidumo kuwa Meya wa Manispaa ya Moshi na diwani wa Longuo B, Benedictor Mwashambwa kuwa Naibu Meya, ambapo wamechaguliwa kwa kura zote 28 za ndiyo.
Mwaitebele ametahadharisha dhidi ya tabia zisizofaa, ambapo amesema haitarajiwi kuona diwani anakuwa chanzo cha migogoro katika Halmashauri au kwenye jamii yake.
Baadhi ya madiwani Manispaa ya Moshi,wakiwa kwenye kikao cha kwanza cha mkutano wa baraza la Madiwani
“Hatutegemei kiongozi kuwa mzizi wa mivutano, fitina au makundi yasiyo na maadili. Vilevile, epukeni migongano ya kimaslahi. Madiwani msifanye kazi za wataalamu au kugombana na wakuu wa idara. Kila mtu atimize wajibu wake,” alisisitiza.
Mwaitebele amesema viongozi wengi huchukulia cheo kama nafasi ya kutumika vibaya, jambo ambalo linawanyima heshima wanapoondoka madarakani.
“Umepewa cheo siyo kwa sababu una akili sana au unafaa kuliko wengine. Umepewa ili siku ukiondoka watu wakukumbuke kwa alama nzuri uliyoiweka. Tambueni kuwa Moshi ina watu wengi, na uongozi ni dhamana,” amesema.
"Kusoma na kufuata kanuni ni muhimu ili kuepuka migongano isiyo ya lazima. Mkikwama kuna mwanasheria wa Halmashauri atakayewasaidia. Msilete mgogoro kwenye Halmashauri; fanyeni kazi yenu ili mkiondoka mkumbukwe kwa utumishi bora,na muache alama,” ameongeza.
Aidha, amewataka madiwani kuwa kimbilio la wananchi katika kata zao kwa kusikiliza na kutatua kero badala ya kusubiri Viongozi juu kama Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa.
“Katika kuwahudumia wananchi, msichunguze uwezo wa mtu, dini wala itikadi za kisiasa. Wananchi wote ni wenu; wahudumieni bila ubaguzi,” amesema.
Mwaitebele aliwataka pia kuwa mfano wa kuigwa katika jamii kupitia matendo, mazungumzo, mavazi na ushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii.
“Maadili ni kufanya jambo sahihi mahali popote na wakati wowote. Katika miaka mitano ya uongozi wenu, wekeni alama chanya ya kukumbukwa. Msigombane na watendaji wala Mkurugenzi, maana ninyi mnajenga nyumba moja, hivyo hamna sababu ya kugombea fito,” amesisitiza.
Pia amewakumbusha madiwani kutanguliza maslahi ya umma katika maamuzi yao yote kwa manufaa ya maendeleo ya wananchi na Halmashauri kwa ujumla.
Naye, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Kiseo Nzowa amewataka madiwani hao kwenda kusimamia miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao na kuhakikisha inatekelezwa kwa ubora na kwa kiwango kinachotakiwa kulingana na thamani ya fedha inayotolewa na serikali.
"Mhakikishe mnakwenda kusimamia ipasavyo miradi ya maendeleo kwa wananachi na inakamilika kwa wakati ili wananachi wetu weweze kupata huduma nzuri kwenye maeneo yao,"amesema Nzowa
Aidha, amewataka kuwa wabunifu na kuwa na Maarifa mbalimbali kuhakikisha mapato ya Halmashauri yanaongezeka mara dufu.
"Mapato ndio moyo wa Halmashauri yetu, bila mapato hakuna kitakachofanyika, hivyo muwe wabunifu na kuja na maarifa mbalimbali kuhakikisha mapato yetu ya yanaongezeka mara dufu,"amesema
Meya wa Manispaa ya Moshi, Zuberi Kidumo
Akizungumza Meya Kidumo amesema atashirikiana na madiwani wote pamoja na menejimenti kuhakikisha yale yote waliyowaahidi wananchi wakati wa kampeni yanatekelezwa kikamilifu na wananchi wanapata maendeleo waliyoyakusudia.
"Madiwani mmeweka imani kubwa juu yangu nami nawaahidi sitawaangusha.Katika kipindi cha kampeni yapo mengi ambayo tuliwaahidi wananchi, niwaahidi tutashirikiana madiwani wote pamoja na serikali kuhakikisha ilani ya CCM inatekelezwa na wananchi wanapata maendeleo waliyoyalududia" amesema Kidumo.
Aidha amesema katika kuchochea maendeleo kwa kasi,watahakikisha wanaboresha barabara zote za pembezoni, zinazounganisha kata tisa ili kurahisisha upatilanaji wa huduma kwa wananchi.
"Ili kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi, tupo tayari kukosolewa na kukumbushwa yale ambayo yanahitaji utekekezaji kwani nia yetu sote ni kuhakikisha tunasogeza mbele gurudumu la maendekeo. Tutamalizia miradi yote viporo na kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza ukusanyaji wa mapato"amesema Zuberi.
Akizungimza Mwashambwa, amewaomba madiwani kuwapa ushitikiano ili kiwatumikia wananchi kwa uaminifu na kuyafikia malengo yaliyokusudiwa ya kuleya maendeleo.
"Niombe madiwani mtupe ushirikiano. Tumemaliza uchaguzi,sasa twendeni tukachape kazi kwa mustakabali wa wananchi wa Manispaa ya Moshi. Tutakapokosea tupo tayari kukodolewa katika kuhakikisha manispaa yetu inadonga mbele"amesema Mwashambwa.