NEMC yakabidhiwa maabara tembezi ya kisasa kukagua mazingira
Dar es Salaam. Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekabidhiwa rasmi maabara tembezi ya kisasa kutoka Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA), itakayowezesha ukaguzi wa haraka wa sampuli mbalimbali za mazingira nchini.
Maabara hiyo, iliyotolewa kupitia Mradi wa Kujenga Uwezo kwa Taasisi za Serikali na Binafsi (EMA Project) unaotekelezwa na NEMC kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais, inalenga kuboresha uwezo wa kupima ubora wa maji, kelele, udongo, kemikali, hewa na sampuli nyinginezo za kimazingira kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza wakati wa mapokezi ya maabara hiyo katika ofisi za NEMC jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Immaculate Semesi, amesema upatikanaji wa maabara hiyo utapunguza gharama na muda uliokuwa ukitumika kusafirisha sampuli kwenda maabara zilizoidhinishwa, ambapo kipimo kimoja kiligharimu kati ya Sh5 milioni hadi Sh10 milioni kulingana na aina ya sampuli.
“Kwa sasa NEMC itaweza kufanya uchunguzi ndani ya muda mfupi na kuchukua hatua stahiki mara moja, hali itakayoongeza ufanisi katika kulinda mazingira,” amesema Semesi.
Kwa niaba ya SIDA, Meneja Miradi ya Nishati na Mazingira kutoka Ubalozi wa Sweden nchini, Stephen Mwalufamba, amesema mradi huo unachangia juhudi za Serikali katika maendeleo endelevu na uhifadhi wa mazingira kwa ustawi wa wananchi.
Ameipongeza NEMC kwa jitihada zake katika kusimamia na kulinda mazingira, akisema ushirikiano huo unaimarisha taasisi za ndani kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Naye Mratibu wa Mradi wa EMA (NEMC), Paul Kalokola, amesema maabara hiyo imewekewa vifaa vya kisasa vinavyotoa matokeo sahihi ya kisayansi, ikiwemo kamera ya juu (drone) inayoweza kusafiri umbali mrefu na kusaidia uchukuaji sampuli kwa ajili ya uchunguzi.
Mradi wa EMA ulianza Juni 2020 na unatarajiwa kukamilika Juni 2026, ukiwa na lengo la kujenga uwezo wa taasisi za serikali na binafsi katika utekelezaji wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004, Sura ya 191.