Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIDA yazindua namba ya bure kufuatilia taarifa za Vitambulisho vya Taifa kwa SMS

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (wa pili kulia) akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi wa namba ya bure (15274) itakayowawezesha wananchi kufuatilia taarifa za Vitambulisho vya Taifa kupitia ujumbe mfupi wa maandishi (SMS).  Wa pili kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imezindua rasmi namba ya bure (15274) itakayowawezesha wananchi kote nchini kufuatilia taarifa za Vitambulisho vya Taifa kupitia ujumbe mfupi wa maandishi (SMS), hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuongeza uwazi katika utoaji wa taarifa muhimu za utambulisho wa raia.

Uzinduzi huo umefanyika Desemba 29, 2025 katika ofisi za Makao Makuu ya NIDA, jijini Dar es Salaam, ukiwahusisha viongozi wa Serikali, wawakilishi wa kampuni za simu   pamoja na wafanyakazi wa mamlaka hiyo.

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, ameipongeza NIDA kwa kuja na mfumo huo wa kisasa unaotumia teknolojia ya simu za mkononi.

Simbachawene amesema mfumo wa namba ya bure kwa SMS ni hatua muhimu katika mageuzi ya utoaji wa huduma za umma, hasa kwa wananchi walioko maeneo ya mbali wasio na urahisi wa kufika katika ofisi za NIDA au kutumia huduma za mtandao.

“Mfumo huu unawapa wananchi fursa ya kufuatilia taarifa zao za Vitambulisho vya Taifa kwa haraka, bila gharama na bila usumbufu. Ni suluhisho rafiki kwa wananchi, linalochochea uwajibikaji na kuimarisha imani ya umma kwa NIDA,” amesema Simbachawene.

Waziri huyo amebainisha kuwa matumizi ya namba ya bure yatachangia kupunguza msongamano katika ofisi za NIDA, kuokoa muda kwa wananchi na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.

Aidha, amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono taasisi zinazowekeza katika mifumo ya kidijitali ili kufikia malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuimarisha uchumi wa kidijitali na utoaji wa huduma kwa njia za kisasa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji amesema uzinduzi wa namba ya bure ni matokeo ya uwekezaji mkubwa wa mamlaka hiyo katika mifumo ya kidijitali, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya TEHAMA, usalama wa taarifa na mifumo ya mawasiliano inayokidhi mahitaji ya wananchi.

“NIDA imewekeza kwa kiasi kikubwa katika teknolojia ili kuhakikisha taarifa za wananchi zinalindwa, zinapatikana kwa urahisi na zinatumiwa kwa ufanisi. Mfumo huu ni sehemu ya mkakati mpana wa kidijitali unaolenga kumweka mwananchi katikati ya huduma zetu,” amesema.

Aliongeza kuwa kupitia namba hiyo ya bure, wananchi wataweza kupata taarifa muhimu kuhusu hali ya Vitambulisho vyao, ikiwemo hatua ilipofikia maombi yao, bila kulazimika kusafiri au kutumia gharama za ziada. Hata hivyo, amesisitiza kuwa NIDA itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya mfumo huo ili kuhakikisha unaleta tija iliyokusudiwa.