Nondo nne za TLP, wasiokuwa na kipato halali kutibiwa bure
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji Jacobs Mwambegele akimkabidhi fomu ya uteuzi kwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Yustas Rwamugira leo Jumatatu Agosti 11, 2025 kwenye ofisi za tume zilizopo Njedengwa Jijini Dodoma.
Dodoma. Mgombea wa urais wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Yustas Rwamugira amenadi mambo manne yatakayompeleka Ikulu katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Rwamugira ametaja mambo hayo ni afya na elimu bure, ulinzi, utawala bora na uchumi imara akisisitiza kila Mtanzania lazima afanye kazi itakayomuingizia kipato.
Mgombea urais huyo ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Agosti 11, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhiwa fomu ya kuomba kuwania nafasi hiyo katika Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mtaa wa Njedengwa Jijini Dodoma.
Kwenye ulinzi wa nchi, watasisitiza zaidi kuzilinda sheria za nchi ili kutoa nafasi ya kila mmoja kufanya kazi kwa uhuru na kujipatia kipato.
"Tanzania tuna ardhi, madini, mashamba, lakini tunayo bahari, sasa tukisema mambo yatabadilika lazima wananchi watuelewe tunalenga nini," amesema Rwamugira.
Akizungumzia suala la afya, amesema ni aibu maiti kuzikwa na jiji kwa sababu ya ndugu kuzikimbia wakikwepa madeni ambayo maiti hudaiwa na hospitali.
"Kwenye elimu, TLP tutaanza kufundisha ufundi kutoka shule za chekechea hadi vyuo vikuu, tunataka kila Mtanzania apate elimu bora nchini," amesema.
Hata hivyo, amezungumzia suala la bima akisema wataanza na waendesha pikipiki na watumishi wengine huku akitangaza wenye kazi halali watalipia matibabu kupitia bima, lakini wengine matibabu itakuwa bure.