Oryx Gas yaendeleza mapambano ya uharibifu wa mazingira, kuchochea nishati safi
Dar es Salaam. Kampuni ya Oryx Gas Tanzania imeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kama sehemu ya mchango wake katika uhifadhi wa mazingira, huku ikisisitiza umuhimu wa wananchi kuachana na matumizi ya kuni na mkaa yanayochangia uharibifu wa mazingira nchini.
Wito huo umetolewa leo Juni 5, 2026 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika Soko la Kimataifa la Samaki Feri jijini Dar es Salaam, ambapo wafanyakazi wa kampuni hiyo walishiriki kufanya usafi wa mazingira na kukabidhi vifaa mbalimbali vya usafi kwa soko hilo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja Masoko na Mauzo wa Oryx Gas Tanzania, Shaban Fundi amesema kampuni hiyo imekuwa ikitekeleza shughuli mbalimbali zinazolenga kuhamasisha utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati safi kwa jamii.
Amesema maadhimisho ya mwaka huu yameipa kampuni hiyo fursa ya kuungana na wafanyabiashara na wananchi wanaotumia Soko la Feri katika kutekeleza vitendo vya kulinda mazingira badala ya kuishia kwenye ujumbe wa maneno pekee.
“Leo tumeamua kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani kwa njia tofauti. Tumeungana na wateja wetu kufanya usafi wa mazingira, tumetoa vifaa vya usafi pamoja na vifaa vya kunawia mikono na kutupia taka ili kuboresha mazingira ya soko hili na maeneo yanayolizunguka,” amesema Fundi.
Ameongeza kuwa Oryx Gas inaamini kuwa uhifadhi wa mazingira hauwezi kutenganishwa na matumizi ya nishati safi, ndiyo maana imeendelea kuwekeza katika upatikanaji wa gesi ya kupikia katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa Fundi, Soko la Kimataifa la Samaki Feri ni mfano wa mafanikio ya matumizi ya nishati safi baada ya wafanyabiashara wengi kuhamia matumizi ya gesi badala ya kuni na mkaa, hatua iliyosaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuongeza usalama katika shughuli za biashara.
“Hapo awali matumizi ya kuni na mkaa yalikuwa makubwa sana katika maeneo mengi ya biashara. Leo tunaona mabadiliko makubwa ambapo usafi umeongezeka, mazingira yameboreshwa na hata usalama wa wafanyabiashara umeimarika kutokana na matumizi ya gesi,” amesema.
Amesema matumizi ya gesi si tu yanasaidia kuhifadhi misitu na mazingira, bali pia yanapunguza athari za kiafya zinazoweza kusababishwa na moshi unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa.
Kutokana na hali hiyo, ametoa mwito kwa wananchi kuendelea kuhamia kwenye matumizi ya gesi ya kupikia ambayo amesema ni salama, nafuu na rafiki kwa mazingira.
“Tunawahimiza wananchi kuachana na matumizi ya kuni na mkaa. Gesi ni nishati safi inayosaidia kulinda mazingira yetu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kizazi kijacho,” amesema.
Aidha, amesema kampuni hiyo inaendelea kupanua mtandao wa huduma zake katika maeneo mbalimbali ya nchi ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata fursa ya kutumia nishati safi bila kujali kama wanaishi mijini au vijijini.
Kwa upande wake, Meneja wa Soko la Kimataifa la Samaki Feri ameipongeza Oryx Gas kwa kuchagua soko hilo kuwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, akisema hatua hiyo inaonyesha dhamira ya kampuni hiyo katika kuunga mkono juhudi za kulinda mazingira.
Amesema soko hilo ni miongoni mwa masoko makubwa ya samaki nchini na hupokea wafanyabiashara pamoja na wageni kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania na nje ya nchi, hivyo uwekezaji wa nishati safi umechangia kuboresha mazingira ya biashara na huduma kwa wateja.
“Tunawashukuru Oryx Gas kwa uwekezaji mkubwa walioufanya hapa sokoni. Walituwekea tanki kubwa la gesi na kuwaunganishia wafanyabiashara huduma hiyo, jambo ambalo limeleta manufaa makubwa kwa biashara zetu na mazingira kwa ujumla,” amesema.
Ameeleza kuwa mradi huo umechangia kutekeleza kwa vitendo sera ya taifa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia na kupunguza changamoto zilizokuwa zikitokana na matumizi ya kuni na mkaa.
Naye mfanyabiashara wa samaki katika soko hilo, Mwanahawa Noel amesema kampeni za mazingira zinazoendeshwa na Oryx Gas zimeongeza uelewa kwa wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira na kudumisha usafi katika maeneo yao ya kazi.
“Tunawapongeza kwa kutukumbuka. Uwepo wao hapa unatukumbusha wajibu wetu wa kuweka mazingira safi muda wote. Hata wageni wanaotembelea soko hili kutoka maeneo mbalimbali wanafurahia mazingira mazuri wanayoyakuta,” amesema.
Mfanyabiashara mwingine, Shaibu Ulaya amesema mradi wa matumizi ya gesi uliotekelezwa katika soko hilo umeleta mabadiliko makubwa katika shughuli za biashara kwa kupunguza gharama na changamoto zilizokuwa zikitokana na matumizi ya nishati za jadi.
Amesema pamoja na kuimarisha mazingira ya kazi, matumizi ya gesi yameongeza usalama kwa wafanyabiashara na kusaidia kufanya shughuli za upishi kuwa rahisi na zenye ufanisi zaidi.
Maadhimisho hayo ya Siku ya Mazingira Duniani yalitumika pia kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi katika kupunguza uharibifu wa mazingira, kulinda afya za jamii na kuchangia maendeleo endelevu ya taifa, huku wadau mbalimbali wakisisitiza haja ya kuongeza kasi ya matumizi ya nishati safi nchini ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa misitu.