Osha yatajwa miongoni mwa taasisi za kimkakati Tanzania
Mwenyekiti wa Bodi ya Osha, Makwaia Makani, akimkabidhi vitendea kazi Mjumbe wa Bodi hiyo, Rehema Ludanga, baada ya kuhitimisha mafunzo elekezi ya Bodi ya Ushauri ya Osha yaliyofanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere, Kibaha Mkoani Pwani.
Muktasari:
- Osha imetajwa kuwa taasisi ya kimkakati inayochochea maendeleo ya Taifa kupitia usimamizi wa usalama na afya mahali pa kazi, huku Bodi mpya ikiahidi kuimarisha mazingira salama, ustawi wa wafanyakazi na utekelezaji wa malengo.
Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Hazina imesema Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (Osha) ni miongoni mwa Taasisi muhimu kwa maendeleo ya Tanzania kutokana na jukumu lake la msingi la kusimamia masuala ya usalama na afya katika maeneo ya kazi nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Usimamizi Rasilimali Watu Taasisi za Umma-Ofisi ya Msajili wa Hazina, Hussein Kakurwa wakati wa mafunzo elekezi kuhusu majukumu ya Bodi ya Ushauri ya Osha yaliyofanyika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere, Kibaha Mkoani Pwani.
"Kama tunavyojua suala la usalama na afya ni la msingi sana na ili Taifa lolote liweze kuendelea ni lazima lihakikishe watu wake wanafanya kazi katika mazingira salama na wanakuwa na afya njema," amesema na kuongeza.
"Kwahiyo jukumu ambalo Osha wamepewa ni la msingi sana na Ofisi ya Msajili wa Hazina tunaichukulia Osha kuwa miongoni mwa Taasisi nyeti na za kimkakati katika jukumu la serikali ya kusukuma maendeleo ya wananchi, ameeleza Kakurwa," ameeleza.
Aidha, amesema Ofisi ya Msajili wa Hazina inajukumu la kuendesha mafunzo kwa viongozi wa Taasisi za umma ili kuwafahamisha na kuwakumbusha kuhusu majukumu yao ya msingi kwa mujibu wa sheria zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Mwenyekiti wa Bodi ya Osha, Makwaia Makani amewahakikishia wafanyakazi nchini kuwa Bodi yake itakuwa karibu na waajiri wote ili kuhakikisha kwamba wanaboresha mazingira ya kazi ili kulinda afya, usalama na ustawi wa wafanyakzi.
Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Usimamizi Rasilimali Watu katika Taasisi za Umma-Ofisi ya Msajili wa Hazina, Hussein Kakurwa (wakwanza kushoto), akijibu maswali na kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali katika mafunzo elekezi ya Bodi ya Ushauri ya Osha yaliyofanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere, Kibaha Mkoani Pwani.
Amedokeza kuwa mafunzo elekezi waliyoyapata yamewapa fursa ya kuielewa kikamilifu Taasisi ya Osha na hivyo kuwa kwenye nafasi nzuri ya kusimamia na kufuatilia utendaji wa Taasisi hiyo.
Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi hiyo, Rehema Ludanga, amesema baada ya mafunzo hayo ni wajibu wao kama Bodi kutumia maarifa na uzoefu wao katika kumshauri Waziri na Menejimenti ya Osha ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya msingi ya Taasisi.
Mtendaji Mkuu wa Osha, Khadija Mwenda, amewashukuru viongozi wa juu kwa kuhakikisha Taasisi ya OSHA inapata Bodi mpya baada ya iliyokuwepo kuhitimisha kipindi chake.
“Tumeiahidi Bodi kwamba malengo yote tuliyoyaweka katika mpango mkakati wetu wa miaka mitano (2026-2031) ambayo yamezingatia vipaumbele vya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 tutayatekeleza ipasavyo.
”Bodi ya Ushauri ya Osha iliundwa hivi karibuni na kuzinduliwa rasmi Mei 25, 2026 Jijini Dar es Salaam ambapo miongoni mwa majukumu ya msingi ya Bodi hiyo ni kumshauri Waziri mwenye dhamana ya Kazi, kuhusu utendaji wa Osha hususan kuandaa vipaumbele, mipango na bajeti pamoja na kufuatilia utekelezaji wa mipango hiyo ili kufikia malengo ya Taasisi," amesema