Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Profesa Kahyarara: Serikali yaendelea kuboresha usafiri wa anga nchini

Serikali itaendelea kuwekeza katika kuimarisha sekta ya usafiri wa anga nchini kwa kuboresha miundombinu, kuimarisha usalama wa safari za anga na kuhimiza matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma. Hayo yamebainishwa jana Juni 22,2026  na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara,  alipotembelea banda la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) katika maonyesho ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, yanayofanyika katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.

Akiwa katika banda hilo, Profesa Kahyarara alipokewa na Meneja wa TCAA Kituo cha Dodoma, Aswile Kamendu, ambaye alimueleza juhudi mbalimbali zinazotekelezwa na Mamlaka katika kuimarisha sekta ya usafiri wa anga nchini, ikiwemo maboresho ya miundombinu ya anga, kuimarisha usalama wa safari za anga pamoja na kuhimiza matumizi ya teknolojia za kisasa katika utoaji wa huduma.

Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Profesa Kahyarara alisema, “Serikali inaendelea kuwekeza katika kuimarisha sekta ya usafiri wa anga kwa kuhakikisha miundombinu inaboreshwa, usalama unaimarishwa na teknolojia za kisasa zinatumika ili kuongeza ufanisi wa huduma. Hatua hizi ni muhimu katika kuchochea maendeleo ya uchumi na kuimarisha ushindani wa nchi yetu kikanda na kimataifa.”

Mbali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, wageni wengine waliotembelea banda la TCAA ni pamoja na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,  Juma Mkomi, Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Profesa Philipo Sanga, na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), Dk Habibu  Suluo.

Wageni hao walipata maelezo kuhusu majukumu ya TCAA, mafanikio yaliyopatikana pamoja na mikakati inayotekelezwa katika kuimarisha usalama, ufanisi na maendeleo ya sekta ya usafiri wa anga nchini.

Kupitia ushiriki wake katika maonyesho hayo, TCAA pia imetumia fursa hiyo kuwahamasisha vijana na wadau wa sekta ya usafiri wa anga kuchangamkia fursa za mafunzo zinazotolewa na Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania (CATC), kinachomilikiwa na mamlaka hiyo. Mafunzo yanayotolewa chuoni hapo yanalenga kukabiliana na changamoto ya upungufu wa wataalamu wa ndani katika sekta ya usafiri wa anga kwa kuzalisha wataalamu wa kutosha na wenye viwango vinavyokubalika kimataifa.

Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu”, ikisisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia katika kuboresha huduma kwa wananchi na kuimarisha uwajibikaji katika utumishi wa umma. Wiki ya Utumishi wa Umma huadhimishwa kila mwaka kwa lengo la kutambua mchango wa watumishi wa umma katika maendeleo ya Taifa, ambapo maadhimisho ya mwaka huu yanatarajiwa kufikia kilele chake leo  Juni 23, 2026.