RC Mara aagiza ujenzi wa uzio kudhibiti wanyama wakali Serengeti
Mkuu wa Mkoa wa Mara,Kanali Evans Mtambi akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Makundusi wilayani Serengeti kwaajili ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
- Uzio huo unatarajiwa kujengwa katika vijiji saba kwa urefu wa kilomita 35. Hadi sasa vijiji vitano vimekubaliana na mapendekezo ya wataalamu kuhusu njia ya uzio, huku vijiji viwili vikiendelea kutofautiana juu ya eneo utakakopita.
Serengeti. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi ameagiza kuanza mara moja kwa ujenzi wa uzio wa kuzuia wanyama waharibifu na wakali katika vijiji vinavyozunguka mapori ya akiba ya Ikorongo na Grumeti wilayani Serengeti.
Pia ameagiza kuitishwa kwa mikutano mikuu ya vijiji vya Makundusi na Parknyigoti ili kutatua mgawanyiko uliopo miongoni mwa wananchi kuhusu eneo ambalo uzio huo unapaswa kupita, hatua itakayowezesha utekelezaji wa mradi huo kuanza.
Maagizo hayo ameyatoa leo Juni 3, 2026 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Makundusi kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Katika mkutano huo, wananchi walitaka kupatiwa ufumbuzi wa kudumu wa changamoto ya uvamizi wa wanyama waharibifu na wakali ambao wamekuwa wakihatarisha maisha yao, mifugo na mazao ya mashambani.
Wamesema kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na mashambulizi ya tembo na wanyama wengine, hali iliyosababisha vifo, majeruhi na hasara kubwa ya mazao.
Baadhi ya wananchi wakiwa kwenye mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Makundusi wilayani Serengeti ambapo Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amesikiliza na kutatua kero zao. Picha na Beldina Nyakeke
Mkazi wa eneo hilo, Meng'anyi Mahe, amesema uvamizi wa tembo mashambani umekuwa jambo la kawaida na kusababisha wakulima wengi kukosa matumaini ya kuvuna mazao yao.
“Hapa suala la tembo kuvamia mashamba ni la kila siku. Tunachoka kuanza upya kila msimu kwa sababu mazao yanaliwa kabla ya kufikia mavuno. Tunaomba suluhisho la kudumu,” amesema.
Kwa upande wake, Sophia Prosper alisema baadhi ya mazao ya chakula yameanza kutoweka katika vijiji hivyo kutokana na hofu ya kuvamiwa na wanyama.
“Tumefikia hatua ya kusahau kulima mazao kama mihogo. Hata yale tunayolima hatuna uhakika wa kuyavuna kwa sababu uvamizi hutokea mara kwa mara,” amesema.
Naye Sabato Sabato amesema wanyama hao wameendelea kuhatarisha maisha ya wananchi na mifugo yao, akieleza kuwa ndugu yake aliwahi kufariki dunia baada ya kukanyagwa na tembo.
“Zaidi ya miaka 10 tumekuwa tukiahidiwa kujengwa kwa uzio huu. Tunaomba utekelezwe kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu kwa sababu waathirika wakubwa wa uvamizi huu ni wakulima,” amesema.
Amedai mgawanyiko uliopo katika Kijiji cha Makundusi unatokana na tofauti za maslahi kati ya wakulima na wafugaji kuhusu maeneo ya malisho.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Makundusi, Joseph Mseti, amesema wananchi wengi wanaunga mkono ujenzi wa uzio huo, lakini baadhi ya wafugaji wana hofu ya kupoteza maeneo yao ya malisho.
Baadhi ya wananchi wakiwa kwenye mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Makundusi wilayani Serengeti ambapo Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amesikiliza na kutatua kero zao. Picha na Beldina Nyakeke
“Wanafikiri malisho yao yataingia ndani ya uzio na watashindwa kuyatumia. Pia wana hofu kwamba ikitokea wanakimbizwa na wanyama wakali wakati wa kuchunga mifugo, uzio unaweza kuwa kikwazo kwao,” amesema.
Akizungumza baada ya kusikiliza hoja za wananchi, Kanali Mtambi amesema Serikali inalenga kupata suluhisho la kudumu la changamoto hiyo ambayo imekuwa ikiwatesa wakazi wa eneo hilo kwa miaka mingi.
“Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali, lakini tatizo limeendelea kuwepo. Kwa mujibu wa ushauri wa wataalamu, uzio huu utasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza migogoro kati ya binadamu na wanyamapori. Hatutaki kuendelea kutoa kifuta machozi kwa waathirika, tunataka kuzuia machozi yasitoke kabisa,” amesema.
Amesema endapo uzio utajengwa kwa kufuata mapendekezo ya baadhi ya wananchi wanaotaka maeneo ya malisho yaachwe nje ya uzio, kuna hatari ya kuathiri mfumo wa ikolojia na kukiuka masharti ya uhifadhi wa wanyamapori.
“Wataalamu wameeleza kuwa uzio unatakiwa kwenda katika mstari ulioainishwa. Ukianza kukata kona kwa ajili ya kuacha maeneo ya malisho au vyanzo vya maji nje ya uzio, utaharibu malengo ya mradi na kuathiri upatikanaji wa maji kwa wanyamapori,” amesema.
Kanali Mtambi amesema Serikali ya Mkoa wa Mara ina mpango wa kuendelea kujenga uzio huo hadi kufika eneo la Ziwa Victoria upande wa Bunda ili kupunguza madhara yanayosababishwa na wanyama wakali na waharibifu kwa wananchi.
Amesema atashiriki binafsi katika mikutano mikuu ya vijiji vya Makundusi na Parknyigoti pamoja na wataalamu wa sekta husika ili kutoa elimu zaidi kwa wananchi kabla ya kufanyika kwa maamuzi ya mwisho.
Kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa katika mkutano huo, uzio huo unatarajiwa kujengwa katika vijiji saba kwa umbali wa kilomita 35. Vijiji vya Nyanungu, Nyichoka, Nattambiso, Motukeri na Bukore tayari vimekubaliana na mapendekezo ya wataalamu, huku Makundusi na Parknyigoti vikisubiri maamuzi yatakayopatikana kupitia mikutano mikuu ya vijiji.