Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

RC Mara awataka vijana kueneza ujumbe wa matumaini

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi

Muktasari:

  • RC Mtambi amewataka viongozi wa dini kuendelea kuliombea taifa na mkoa huo ili kudumisha amani na utulivu, akieleza kuwa dunia inapitia kipindi kigumu kinachohitaji mshikamano na uzalendo.

Musoma. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi, amewaomba wakazi wa mkoa huo, hususan vijana, kubeba na kusambaza ujumbe wa matumaini, upendo na mshikamano ili kuimarisha ustawi wa jamii.

RC Mtambi ametoa wito huo wakati akitoa salamu za Serikali katika ibada ya Pasaka iliyofanyika katika Kanisa Anglikan la Mtakatifu Yohana, Dayosisi ya Mara, mjini Musoma.

Katika hotuba yake, amewataka pia viongozi wa dini kuendelea kuliombea taifa na mkoa huo ili kudumisha amani na utulivu, akieleza kuwa dunia inapitia kipindi kigumu kinachohitaji mshikamano na uzalendo.

“Endeleeni kuombea mkoa wetu na taifa letu kwa ujumla kwani hali ya dunia si nzuri, tunapaswa kutanguliza maslahi ya taifa ili tuendelee kuwa salama,” amesema.

Baadhi ya waumini wa kanisa la Anglikan Dayosisi ya Mara wakiwa kwenye ibada ya Pasaka mjini Musoma.  Picha na Beldina Nyakeke

Amegusia pia suala la malezi ya vijana, akiwataka viongozi wa dini kuwa mstari wa mbele kuwaongoza vijana wa kike na wa kiume ili kuepuka mmomonyoko wa maadili unaochangiwa na matumizi yasiyo sahihi ya mitandao ya kijamii.

Amesisitiza kuwa, licha ya Serikali na wazazi kuwa na wajibu katika malezi, viongozi wa dini wanapaswa kuchukua nafasi kubwa zaidi katika kujenga jamii yenye maadili mema.

Aidha, amewatahadharisha wananchi kuchukua tahadhari katika kipindi cha mvua, hasa wachimbaji wadogo, akieleza kuwa udongo na miamba imelegea hivyo kuongeza hatari ya ajali. Ameagiza pia mamlaka husika kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo ya uchimbaji kwa ajili ya usalama.

Akihubiri katika ibada hiyo, Askofu wa Kanisa Anglikan Dayosisi ya Mara, George Okoth, amewataka Watanzania kuacha tabia ya kulaumu viongozi kwa changamoto zao na badala yake kujitathmini na kupanga mipango ya maendeleo.

Amesema baadhi ya wananchi wamezoea kulaumu viongozi wa Serikali, dini na hata wazazi wao kwa kutofanikiwa, hali ambayo si sahihi.

“Badala ya kulalamika, tumieni akili tulizopewa na Mungu kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo,” amesema.

Ameongeza kuwa jamii inapaswa kutumia historia kama rejea ya maendeleo badala ya kuishi kwa malalamiko, akisisitiza kuwa mafanikio huanza na mtu binafsi mwenye malengo.

Askofu Okoth amewahimiza waumini kuitumia Pasaka ya mwaka 2026 kujipanga upya na kutekeleza mipango ya maisha kwa vitendo.

Kwa upande wao, baadhi ya waumini wamehimiza kuendelezwa kwa mema yaliyofanywa kipindi cha Kwaresma. Mmoja wao, Elija Alfred, amesema hakuna sababu ya kurejea katika matendo yasiyoendana na mafundisho ya dini baada ya kipindi hicho.

“Kwaresma ni ukumbusho wa namna bora ya kuishi, hivyo tuendeleze mema yote tuliyojifunza,” amesema.