Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

RC Mtambi: Chukueni hatua dhidi ya watumishi bila kujali majina, vyeo

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mara, Mohamed Shariff akizungumza kwenye warsha ya wadau wa usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Mara.  Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameagiza Takukuru kuwachukulia hatua watumishi wa umma watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo bila kujali vyeo, majina au umaarufu wao.

Musoma. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani humo kuwachukulia hatua watumishi wa umma watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa wakati wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo bila kujali vyeo, majina au umaarufu wao.

Kanali Mtambi alitoa agizo hilo Julai 13, 2026, mjini Musoma wakati akifungua warsha ya wadau wa usimamizi na utekelezaji wa programu na miradi ya maendeleo iliyoandaliwa na Takukuru.

Alisema mapambano dhidi ya rushwa ni nguzo muhimu ya utawala bora, huku akisisitiza kuwa uwajibikaji na uadilifu ni msingi wa kufanikisha vita dhidi ya vitendo hivyo.

Alisema endapo watumishi wanaobainika kujihusisha na rushwa wataendelea kuachwa kwa kuzingatia majina au vyeo vyao, juhudi za kupambana na rushwa hazitazaa matokeo yaliyokusudiwa.

"Najua jukumu kubwa mlilo nalo ni pamoja na kuzuia, lakini nawaagiza muongeze kasi ya kupambana. Badala ya kumuonya mtumishi aliyebainika kujihusisha na vitendo hivi, mchukulieni hatua. Mnapowaacha kwa kigezo cha kuwaonya, wataendelea kufanya hivyo wakijua hakuna hatua zitakazochukuliwa dhidi yao," amesema.

Kanali Mtambi amesema ni vigumu kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 ikiwa vitendo vya rushwa vitaendelea kuvumiliwa, akieleza kuwa Takukuru ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha malengo ya dira hiyo yanafikiwa.

Alisema kutowajibika, kufanya uzembe na kusababisha miradi kutokamilika kwa wakati au kutotoa thamani halisi ya fedha ni makosa yanayotambuliwa na sheria ya rushwa.

"Kutokuwajibika katika majukumu yako yaliyobainishwa kisheria pamoja na kufanya uzembe na kusababisha miradi kutokukamilika kwa wakati na kwa thamani ni kosa kwa mujibu wa sheria ya rushwa. Matukio kama haya yapo, Takukuru mtusaidie kupambana nayo," amesema.

Amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, kijamii na kimkakati kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi, hivyo watumishi wanaokwaza utekelezaji wa miradi hiyo wanapaswa kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Pia ameitaka Takukuru kuhakikisha inachukua hatua stahiki ili kunusuru fedha za Serikali, akisema vitendo vya rushwa vinaendelea kukwamisha juhudi za maendeleo.

Akizungumza katika warsha hiyo, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mara, Sharrif Mohamed, amesema mafunzo hayo yameandaliwa kwa lengo la kuwakumbusha wasimamizi wa miradi wajibu wao wa kutekeleza miradi kwa kuzingatia sheria, maelekezo na mikataba husika.

Amesema Takukuru ina jukumu la kuzuia vitendo vya rushwa kwa kutoa elimu, hivyo warsha hiyo inalenga kuongeza uelewa wa wadau ili kuepusha ukiukwaji wa taratibu katika utekelezaji wa miradi.

Kwa mujibu wake, baadhi ya changamoto zinazojitokeza ni pamoja na miradi kutokamilika kwa wakati, kutekelezwa chini ya kiwango, kutofuata maelekezo na kutotoa thamani ya fedha kutokana na ubadhirifu.

Kutokana na hali hiyo, amesema taasisi hiyo imeona umuhimu wa kuwakutanisha wadau ili kujenga uelewa wa pamoja kuhusu usimamizi bora wa miradi ya maendeleo.

Mohamed amesema katika kipindi cha miaka mitatu, Takukuru Mkoa wa Mara imekagua miradi 244, huku miradi 85 ikipewa maelekezo na kufanyiwa marekebisho baada ya kubainika kuwa na kasoro mbalimbali, ikiwamo viashiria vya rushwa.

Baadhi ya washiriki wa warsha hiyo wamesema mafunzo ya aina hiyo yanapaswa kutolewa mara kwa mara ili kuwajengea uwezo wasimamizi wa miradi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Wamesema mazingira ya kazi wakati mwingine huchangia wasimamizi wa miradi kuonekana kutotimiza wajibu wao, hususan pale makandarasi wanaposhindwa kutekeleza miradi kwa wakati, hivyo mafunzo hayo yatawasaidia kufahamu hatua sahihi za kuchukua.

Mmoja wa washiriki, Joseph Mrimi, amesema kabla ya warsha hiyo hakuwa akifahamu kuwa uzembe katika usimamizi wa miradi unaweza kuwa kosa chini ya sheria ya rushwa.

"Kuna watu tulikuwa hatujui kama uzembe ni kosa kisheria, tena chini ya sheria ya rushwa. Hivyo unaweza kuona namna wasimamizi wa miradi wanavyoweza kufanya makosa bila kujua. Niiombe Takukuru na taasisi nyingine kuendelea kutoa warsha za namna hii mara kwa mara," amesema.