Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sabasaba yatajwa kusogeza huduma za Serikali karibu na wananchi

Muktasari:

  • Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Sospeter Mtwale,amesema  ushiriki wa taasisi za Serikali katika maonyesho ya  Sabasaba unatoa fursa kwa wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu huduma zinazotolewa, huku ukiwawezesha wajasiriamali kutangaza bidhaa na huduma zao na kupanua masoko.

Dar es Salaam. Serikali imesema Maonyesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yamekuwa jukwaa muhimu la kusogeza huduma kwa wananchi na kuongeza uelewa kuhusu programu na miradi inayotekelezwa na taasisi za umma.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Sospeter Mtwale, baada ya kutembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo, Mtwale amejionea huduma mbalimbali zinazotolewa kwa wananchi pamoja na mafanikio yaliyofikiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake katika utekelezaji wa majukumu yao.

"Maonyesho haya kwetu Serikali ni muhimu kwa kuwa taasisi zetu zinakuwa karibu na wananchi na wananchi wanapata nafasi ya kuuliza maswali na wengine kuhudumiwa na taasisi zetu, kwahiyo maonyesho haya yamesogeza huduma kwa wananchi,"amesema.

Amesema ushiriki wa taasisi za Serikali katika Sabasaba unatoa fursa kwa wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu huduma zinazotolewa, huku ukiwawezesha wajasiriamali kutangaza bidhaa na huduma zao na kupanua masoko.

Katika ziara hiyo, Mtwale amejionea  programu, miradi na huduma zinazotekelezwa kupitia ofisi ya Waziri Mkuu, akielezwa hatua hizo zinalenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo.

Mtwale pia alitembelea mabanda ya baadhi ya mikoa na halmashauri zinazoshiriki maonesho hayo, ambapo aliwapongeza viongozi na wadau kwa kutumia maonesho hayo kutangaza huduma na kuwafikia wananchi moja kwa moja.

Kwa upande wake mkazi wa Mbagala, Dar es Salaam, Zainab Jackson amesema maonesho ya Sabasaba yamekuwa yakirahisisha wananchi kupata taarifa za huduma za Serikali bila kulazimika kutembelea ofisi mbalimbali.

"Ni jambo zuri Serikali kutumia maonesho haya kuwasogezea wananchi huduma. Unapata nafasi ya kuuliza maswali na kupata majibu papo hapo, jambo linaloongeza uelewa kuhusu huduma zinazotolewa," amesema.

Naye John Francis, mfanyabiashara wa bidhaa za kilimo kutoka Morogoro, amesema ushiriki wa taasisi za Serikali katika Sabasaba unasaidia kujenga mahusiano mazuri kati ya wananchi na Serikali, lakini ameshauri huduma hizo zisibaki kwenye maonesho pekee.

"Maonesho ni fursa nzuri, lakini ni muhimu taasisi ziendelee kuwafikia wananchi hata baada ya Sabasaba kupitia kampeni na huduma zinazowafikia maeneo yao ili watu wengi zaidi wanufaike," amesema.