Serikali yaonyesha njia salama za kufanya biashara na China
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Denis Londo akizungumza na wafanyabiashara wakati akiwaelekeza njia salama za kufanya biashara na nchi ya China ikiwa ni moja ya njia ya kusisimia biashara zao katika maonyesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DiTF).
Muktasari:
- Kuanzia Mei mosi, 2026, China ilianza kutekeleza mpango wa kuondoa ushuru kwa takriban asilimia 98 ya bidhaa zinazotoka katika nchi nyingi za Afrika, ikiwemo Tanzania.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imewataka wafanyabiashara kutumia njia salama na rasmi za biashara wanapojihusisha na masoko ya kimataifa, hususan China, ili kujikinga na hatari za udanganyifu, taarifa potofu na miamala isiyoaminika.
Hayo yamebainishwa katika Kliniki ya Biashara na Uwekezaji iliyoandaliwa na Mamlaka ya Uwekezaji na Kanda Maalum za Kiuchumi Tanzania (Tiseza), kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini China, iliyofanyika katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba.
Kliniki hiyo ililenga kuwajengea uwezo wafanyabiashara wa Tanzania kuhusu mbinu salama za kufanya biashara, taratibu sahihi za kuagiza bidhaa kutoka China pamoja na fursa za biashara na uwekezaji katika soko hilo kubwa la Asia.
Akizungumza katika kliniki hiyo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, amewataka wafanyabiashara kutumia taasisi rasmi za Serikali katika kufanya biashara za kimataifa, huku akisisitiza umuhimu wa Ubalozi wa Tanzania nchini China kama njia salama na ya kuaminika ya kupata taarifa na kufanya miamala ya biashara.
“Wafanyabiashara wanapaswa kutumia njia salama na rasmi za Serikali, hususan kupitia Ubalozi wetu nchini China, ili kupata taarifa sahihi, kuepuka udanganyifu na kuhakikisha wanajenga mahusiano ya biashara ya kuaminika,” amesema Londo.
Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazofaidika na sera mpya ya China ya kupunguza na kuondoa ushuru kwa bidhaa zinazoingia katika soko lake.
Kuanzia Mei mosi, 2026, China ilianza kutekeleza mpango wa kuondoa ushuru kwa takriban asilimia 98 ya bidhaa zinazotoka katika nchi nyingi za Afrika, ikiwemo Tanzania.
Mpango huo unatarajiwa kuongeza ushindani wa bidhaa za Afrika katika soko la China kwa kuzifanya ziingie bila gharama za forodha.
Balozi wa Tanzania nchini China, Dk Suleiman Suleiman, amesema soko la China linaendelea kutoa fursa kubwa kwa bidhaa za Afrika, huku akisisitiza umuhimu wa kufuata viwango vya ubora ili kufanikisha upatikanaji wa masoko hayo.
“China ni soko kubwa na lenye fursa nyingi, lakini ni lazima bidhaa zetu zikidhi viwango vinavyotakiwa ili tunufaike na fursa ya biashara ya bidhaa zisizo na ushuru kwa baadhi ya bidhaa za Afrika,” amesema.
Mkurugenzi wa Kukuza Uwekezaji wa Tiseza, George Mukono, amesema taasisi hiyo inaendelea kuimarisha uhusiano kati ya wawekezaji wa ndani na nje kwa kuwasaidia kupata taarifa sahihi, fursa za uwekezaji na washirika wa biashara wa kuaminika.
Amesema lengo ni kuhakikisha Watanzania wanashiriki kikamilifu katika sekta za uzalishaji na kutumia fursa zilizopo ndani na nje ya nchi kupitia mifumo salama ya uwekezaji na biashara.
Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na kuimarisha mifumo salama ya ushirikiano wa kimataifa ili kulinda wafanyabiashara na kukuza uchumi wa Taifa.