Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wachina wanavyotumia sauti kuondoa mawe kwenye figo

Dk Kanansia Mbowe kulia akizungumza na mmoja wa wananchi waliofika kwenye maonyesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) alipotembelea katika banda lao kupata ushauri wa kitabubu.

Muktasari:

  • Hadi mwaka 2025 idadi ya watu wenye matatizo ya figo wanaopata huduma ya usafishaji damu ‘dialysis’ katika vituo vya afya nchini imeongezeka kutoka 1,017 mwaka 2019 hadi 3,327 mwaka 2025.

Dar es Salaam. Wakati wagonjwa wengi wa mawe kwenye figo wakikabiliwa na gharama za upasuaji na muda mrefu wa kupona, Hospitali ya Sino Kangning Polyclinic imeanza kutumia teknolojia ya mawimbi ya sauti kuvunja mawe hayo bila kufungua mwili wa mgonjwa.

Teknolojia hiyo inalenga kupunguza gharama za matibabu, muda wa kulazwa hospitalini na kuwawezesha wagonjwa kurejea katika shughuli zao za kawaida kwa haraka.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi, Julai 4, 2026 Katika Viwanya vya Maonyesho ya Biashara maarufu sabasaba jijini Dar es Salaam, Dk Kanansia Mbowe wa hospitali hiyo amesema huduma hiyo hutumia mawimbi ya sauti kuvunja mawe yaliyopo kwenye figo na kuyageuza vipande vidogo vinavyoweza kutoka mwilini kupitia mkojo bila upasuaji.

"Mgonjwa hahitaji kufanyiwa upasuaji wala kulazwa hospitalini. Tunatumia kifaa kinachotuma mawimbi ya sauti kuelekea kwenye jiwe lililopo kwenye figo. Jiwe husagika na kuwa kama mchanga, kisha hutoka lenyewe kupitia mkojo," amesema.

Amesema teknolojia hiyo bado ni mpya nchini na inapatikana katika hospitali chache, lakini imeanza kuwasaidia wagonjwa wengi kuepuka upasuaji pamoja na muda mrefu wa kupona.

Kwa mujibu wa Mbowe, wagonjwa wengi hufika hospitalini wakiamini upasuaji ndiyo njia pekee ya kuondoa mawe kwenye figo, ilhali maendeleo ya teknolojia yameleta njia mbadala isiyohusisha majeraha makubwa.

Mbali na huduma hiyo, amesema hospitali hiyo ina madaktari bingwa wa mfumo wa mkojo wanaotoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali yanayohusu figo, kibofu na njia ya mkojo.

Takwimu zinaonyesha kuwa mahitaji ya huduma za matibabu ya magonjwa ya figo yanaendelea kuongezeka nchini. Hadi mwaka 2025, idadi ya wagonjwa waliokuwa wakipata huduma ya usafishaji damu (dialysis) iliongezeka hadi 3,327 kutoka 1,017 mwaka 2019.

Mbowe amesema hospitali hiyo pia imeleta madaktari bingwa wa upasuaji wa mifupa kutoka China wenye uwezo wa kuunganisha viungo vilivyokatika kabisa, ikiwamo vidole, mikono na sehemu nyingine za mwili.

Amesema mafanikio ya huduma hiyo hutegemea mgonjwa kufikishwa hospitalini ndani ya saa nane tangu ajali itokee.

"Ndani ya muda huo mishipa ya damu na mishipa ya fahamu huwa bado inaweza kuunganishwa. Kadri muda unavyoongezeka, kiungo hupoteza uhai kutokana na kukosa damu, hivyo uwezekano wa kukiokoa hupungua," amesema.

Mbali na hilo, amesema wataalamu hao pia hutoa huduma za kufunika vidonda sugu vinavyotokana na kisukari kwa kutumia ngozi kutoka sehemu nyingine ya mwili (skin grafting), matibabu ya makovu pamoja na huduma za afya ya uzazi.

Mmoja wa watembeleaji wa maonyesho hayo, Manjit Kumar amesema teknolojia ya kuvunja mawe kwenye figo bila upasuaji inaweza kupunguza gharama za matibabu na muda ambao wagonjwa hutumia hospitalini na nyumbani wakipona.

"Hii itapunguza muda wa kukaa hospitalini na nyumbani kujiuguza, hivyo wagonjwa watarejea mapema kwenye shughuli zao za uzalishaji," amesema.