Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Malori ya migodini yanayotumia mafuta kidogo yavutia wawekezaji

Rais wa Msumbiji, Daniem Chapo (kushoto) akimkabidhi tuzo mwakilishi wa GF Trucks kama mshindi wa jumla katika maonyesho ya 50 ya biashara ya kimataifa Dar es Salaam (Sabasaba) kama banda lililoongoza kwa ubora mwaka 2026.

Muktasari:

  • Malori haya ambayo baadhi yameunganishwa nchini, chini ya mpango wa “Made in Tanzania” yanatajwa kuchangia kuongeza ufanisi, kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza tija katika shughuli za madini

Dar es Salaam. Wakati gharama za mafuta zikiendelea kuwa miongoni mwa changamoto zinazoathiri sekta za madini na ujenzi, Kampuni ya GF Trucks and Equipment imeanza kuleta malori na mitambo yenye teknolojia inayopunguza matumizi ya mafuta, hatua inayolenga kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza tija kwa wawekezaji.

Hatua hiyo, pamoja na mambo mengine, imeiwezesha kampuni hiyo kutwaa tuzo ya mshindi wa jumla wa washiriki wa Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), yanayoendelea katika Viwanja vya Sabasaba.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo jana Ijumaa, Julai 3, 2026, Mkurugenzi wa Biashara wa GF Trucks and Equipment, Salman Karmali amesema mwenendo wa soko umebadilika kwani wateja wengi sasa hawazingatii tena gharama ya kununua mashine pekee, bali pia gharama za kuiendesha katika kipindi chote cha matumizi yake.

"Matumizi ya mafuta yamekuwa jambo muhimu kwa wateja wetu, hasa katika sekta za madini na ujenzi ambako mitambo hufanya kazi kwa saa nyingi kila siku. Wanahitaji mashine zenye uwezo mkubwa wa kufanya kazi na zinazotumia mafuta kidogo," amesema.

Amesema baadhi ya malori ya migodini yaliyoonyeshwa katika maonyesho hayo yameunganishwa nchini Tanzania kupitia mpango wa Made in Tanzania, huku kampuni hiyo ikiendelea kuleta mitambo yenye teknolojia za kisasa za injini, zinazopunguza matumizi ya mafuta bila kuathiri uwezo wa kufanya kazi.

Kwa mujibu wa Karmali, mitambo hiyo imekusudiwa kutumika katika shughuli za uchimbaji madini, machimbo ya mawe, ujenzi wa miundombinu na uchimbaji wa visima vya maji, sekta ambazo zinaendelea kukua kwa kasi nchini.

Amesema matumizi madogo ya mafuta yanasaidia kampuni kupunguza gharama za uendeshaji, kuongeza ufanisi wa kazi na hatimaye kuboresha faida za miradi.

"Soko sasa linaangalia zaidi ufanisi. Wateja wanahitaji mitambo inayodumu, inayotegemewa na yenye gharama nafuu za uendeshaji kwa sababu ndiyo huamua faida ya mradi," amesema.

Karmali amesema tuzo hiyo itaiwezesha kuongeza wigo wa soko na kuendelea kuleta teknolojia zinazokidhi mahitaji ya sekta mbalimbali za uzalishaji.

Akizungumzia mwenendo wa sekta hiyo, wadau wa madini wanasema gharama za mafuta zinaendelea kuwa sehemu kubwa ya matumizi katika shughuli za uchimbaji na ujenzi, hali inayoongeza mahitaji ya mitambo inayotumia mafuta kwa ufanisi zaidi.

Mtaalamu wa sekta ya madini, Carlos Masha amesema matumizi madogo ya mafuta ni miongoni mwa vigezo muhimu vinavyozingatiwa na kampuni nyingi wakati wa kufanya maamuzi ya kununua mitambo.

"Kwa kampuni kubwa za uchimbaji madini, mitambo inayotumia mafuta kidogo inaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za uendeshaji. Kampuni imeleta malori haya kwa wakati sahihi, na nitashauri kampuni ninayofanyia kazi ichunguze uwezekano wa kuyatumia," amesema.