Samia: Fomu ni mwanzo safari kuisaka dola
Muktasari:
- Rais Samia amechukua fomu ya uteuzi wa kugombea urais INEC leo, Jumamosi Agosti 29, 2025 akiambatana na mgombea mwenza wake, Dk Emmanuel Nchimbi.
Dodoma. Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amesema hatua ya kuchukua fomu Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ni ishara kwamba mbio za kuisaka dola zimeanza rasmi.
Samia anayetetea kiti cha urais amechukua fomu ya uteuzi INEC leo Jumamosi Agosti 9, 2025 akiambatana na mgombea mwenza wake, Dk Emmanuel Nchimbi.
Akizungumza na wanachama makao makuu ya CCM Dodoma baada ya kuchukua fomu, amesema mbio za kuelekea Oktoba zimeanza rasmi, akifananisha kama ni mpira, filimbi imepulizwa na mpira umeanza.
Samia amesema ukitaka kujua utamu wa ngoma ni vema uingie ndani uanze kudemka, ndiyo maana ameingia kwenye uchaguzi kudemka.
Amesema Serikali imefanya mambo makubwa katika sekta zote na mengi yameshaelezwa katika majukwaa mbalimbali.
Amesema matarajio yake ya kufanya mambo makubwa zaidi yanaanza rasmi, baada ya kuchukua fomu kuwaomba Watanzania ridhaa ya kuwa Rais.
Hata hivyo, amesema hiyo si safari yake na mgombea mwenza pekee, bali ya kila Mtanzania na chama cha siasa, ndiyo maana kila baada ya miaka mitano wanarudi kwa wananchi kuomba ridhaa.
Amesema wananchi wanakwenda kuchagua chama kitakachowaletea maendeleo, utu, ustawi na kujitegemea.
"Hii ni safari ya kwenda kuwaeleza wananchi sera ya kila chama katika kuhakikisha tunajenga hatima njema ya Watanzania," amesema.
Samia amesema tayari wameshaweka wazi yatakayokwenda kufanywa na chama hicho kupitia Ilani ya Uchaguzi ya 2025-2030, ikiwamo kuimarisha uchumi wa viwanda na ubunifu, kuongeza ajira na bima ya afya kwa wote.
Amesema angalau CCM ina uzoefu mkubwa katika utekelezaji wa hayo, kwani vyama vingine vyote vinapaswa kujifunza kwanza.
"Nimechukua fomu kuwania nafasi ya urais na ili ikamilike lazima wajitokezeka wanachama watakaokuwa wadhamini wa wagombea," amesema.
Amesema fomu hiyo itapelekwa mikoa yote kuomba kupata wadhamini watakaomdhamini kuwa mgombea wa CCM.
Samia, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM ametumia jukwaa hilo, kuwaomba wanachama, kwa kuwa michakato ya nafasi mbalimbali inaendelea na kisha uteuzi wa wagombea wa udiwani na ubunge, makada waepushe makundi na ushindani wa ndani ya chama uishe, ili wabaki kuwa madhubuti.
Katikati ya hotuba yake, amempa dakika mbili Dk Nchimbi awasalimie Watanzania, akimuahidi kuwa msaidizi wake badala ya mshindani ili ilani itekelezwe.
Dk Nchimbi amesema yuko tayari kuungana na Samia kuitafutia ushindi CCM nchi nzima na kwamba, amejiandaa kikamilifu akijua CCM inataka ushindi.
"Nimejiandaa kikamilifu kuwa msaidizi wako na siyo mshindani wako, nitakusaidia kwa nguvu zangu zote ili uweze kutekeleza ilani ya CCM," amesema.
Makamu Mwenyekiti wa CCM- Bara, Stephen Wasira amesema hatua ya Samia kuchukua fomu ya urais ni utekelezaji wa azimio la mkutano mkuu wa Januari uliofanyika Dodoma.
"Ujumbe kwa wanachama wa CCM ni kwamba, tumeanza safari na mitambo iko sawa kabisa. Tumeijaribu na inafanya kazi. Mwezi huu baada ya kutimiza matakwa ya kisheria, sasa tutaanza kazi ya kampeni rasmi kwa muda wa siku 60," amesema.
Amewaambia wanachama kwamba, kuna silaha mbili zitakazotumika ambazo ni mafanikio ya utekelezaji wa ilani iliyopita na ahadi za ilani ya miaka mitano ijayo, akisema imesheheni maono na ikitekelezwa mwaka 2030 kutakuwa na Tanzania tofauti na iliyopo sasa.
"Wanachama hamna cha kuhofu, hata wakija wagombea wangapi. Kwa sababu kwenye msafara wa mamba hata kenge wapo," amesema.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), John Mongella amesema chama hicho hakijaruka wala kukiuka ibara ya katiba au kanuni zake katika mchakato wa kumteua Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea urais.
Kauli ya Mongella inajibu malalamiko ya baadhi ya makada wa chama hicho, wanaodai utaratibu ulikiukwa katika uteuzi wa mgombea huyo, uliofanyika Januari 19, 2025.
"Kazi zote za kukuteua wewe kuwa mgombea wetu na Dk Nchimbi kuwa mgombea mwenza na Dk Hussein Mwinyi kuwa mgombea urais wa Zanzibar, zilifanyika kwa kuzingatia misingi ya katiba ya chama chetu, bila kukiuka ibara wala kanuni yoyote," amesema.
Amesisitiza tayari chama hicho kimeshakamilisha maandalizi ya ushindi, kwanza kwa uteuzi wa mgombea Januari 19, pili kuchukua fomu INEC.
Awali, kauli kama ya Mongella ilitolewa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa aliyesema wanachama waliojitokeza kusherehekea tukio hilo ni uthibitisho kuwa hakuna mwenye uwezo wa kuurudisha nyuma uamuzi wao wa Januari 19.
"Hakuna wa kutuzuia, wanachama waliamua. Tupo milioni 13 tuliamua, hakuna wa kuturudisha nyuma," amesema Kimbisa na kuibua shangwe kutoka kwa wafuasi na wanachama wa chama hicho, waliokusanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya chama hicho, Dodoma.
Kwa kuwa lengo la kwanza la CCM ni kushinda uchaguzi na kuunda Serikali, Mongella amesema chama hicho kimejizatiti na kujiandaa vizuri, kimuundo na kimkakati kuhakikisha kinashinda nafasi zote.
"Maandalizi ya ushindi wa chama chetu katika uchaguzi mwaka huu, yameshakamilika na kupitia mkutano mkuu wa Januari tulitekeleza mambo yote," amesema.
Amesema Agosti 22, CCM itatangaza wagombea wake kwa ngazi ya jimbo hadi wadi.
Amesema sehemu ya pili ya maandalizi ya ushindi imejikita katika misingi ya sheria na shughuli hiyo ni mwanzo wa safari ya ushindi wa CCM.
"Kuanzia leo hakuna kulala mpaka kieleweke na tunamaanisha hilo," amesema.
Shamrashamra
Msafara wa uchukuaji fomu ulipambwa na magari zaidi ya 20, baadhi yakinakshiwa na picha ya mgombea wa CCM, huku vijana wa bodaboda wakiwa sehemu ya msafara huo, wakipeperusha bendera ya chama hicho.
Msafara pia ulihusisha vikundi vya waendesha viatu vya magurudumu, huku wananchi wakibeba mabango yenye ujumbe na picha mbalimbali za kiongozi huyo.
Isingekuwa rahisi kujua nani ni kada wa CCM na yupi ni mfuasi tu, kwani kila mmoja alionekana akidemka kwa namna yake kuanzia kwenye msafara hadi ofisi za makao makuu ya CCM ambako Samia alizungumza nao.
Samia aliyeiongoza Tanzania kwa miaka minne, akiapishwa Machi 19, 2021 baada ya kifo cha mtangulizi wake, hayati Dk John Magufuli, amewasili makao makuu ya CCM saa 6:15 mchana.
Samia alifika ofisi za INEC saa 5:15 asubuhi kwa ajili ya kuchukua fomu akiwa amepanda gari lenye rangi ya kijani.
Msafara wake ulitanguliwa na wa Dk Nchimbi, ambaye ni Katibu Mkuu wa CCM uliofika saa 5:11 asubuhi.
Alipowasili Samia alipokewa na Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda na Dk Nchimbi, huku viongozi wa chama na Serikali wa mikoa ya Dodoma na Singida wakiwa kwenye foleni.
Samia ni nani?
Samia ndiye mwanamke wa kwanza kuwa Makamu wa Rais na kuwa Rais wa Tanzania. Ni Rais wa pili wa Tanzania kutokea Zanzibar baada ya Ali Hassan Mwinyi aliyeiongoza kuanzia mwaka 1985 mpaka 1995.
Samia aliyezaliwa Januari 27 mwaka 1960 visiwani Zanzibar, ni Rais wa kwanza Tanzania kuongoza Serikali baada ya mtangulizi wake kufariki dunia akiwa madarakani.
Mwaka 2000 CCM kilimteua kuwa mwakilishi kupitia Viti Maalumu na akiwa kwenye Baraza la Wawakilishi aliteuliwa na Rais Amani Karume kuwa waziri.
Mwaka 2005 aliteuliwa tena hadi mwaka 2010 alipogombea ubunge katika Jimbo la Makunduchi alikoshinda kwa asilimia 80. Baada ya uchaguzi huo aliteuliwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais kushughulikia Muungano.
Mwaka 2014, Samia alichaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba lililoandaa Rasimu ya Katiba Mpya.
Jumapili ya Julai 12 mwaka 2015, Dk John Magufuli alipopitishwa kuwa mgombea wa urais wa CCM, Samia aliteuliwa mgombea mwenza.