Serikali kudhamini wananchi 69,000 Mara kujiunga na bima ya afya
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi akimpa mwanafunzi dawa ya minyoo na kichocho ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa kampeni ya utoaji wa dawa kinga dhidi ya kichocho na minyoo tumbo mkoani humo. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
- Wanufaika hao ni wale walioko chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), ambao tayari wameanza kupatiwa kadi hizo zitakazoanza kutumika rasmi pindi mpango huo wa kitaifa utakapoanza kufanya kazi.
Bunda. Zaidi ya watu 69,000 kutoka kaya masikini mkoani Mara wanatarajiwa kujiunga na mpango wa bima ya afya kwa wote kupitia udhamini wa Serikali, huku zoezi la uhakiki, uandikishaji na utoaji wa kadi za bima likiendelea kwa kasi.
Wanufaika hao ni wale walioko chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), ambao tayari wameanza kupatiwa kadi hizo zitakazoanza kutumika rasmi pindi mpango huo wa kitaifa utakapoanza kufanya kazi.
Akizungumza leo Februari 16, 2026 mjini Bunda wakati wa uzinduzi wa kampeni ya utoaji wa dawa kinga dhidi ya kichocho na minyoo ya tumbo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amesema uandikishaji umefikia hatua nzuri na unatarajiwa kufikia zaidi ya asilimia 90 kabla ya mwisho wa mwezi huu.
Alitoa wito kwa wananchi ambao hawapo kwenye udhamini wa Serikali kuanza kujiandaa ili watakapofikiwa waweze kuandikishwa na kunufaika na mpango huo, akisisitiza kuwa bima ya afya ni msingi wa uhakika wa matibabu kwa wakati wote.
“Hakuna jambo muhimu katika jamii kama kuwa na uhakika wa matibabu. Magonjwa hayatoi taarifa, yanaweza kukukuta huna fedha, hivyo tuhakikishe sote tunakuwa na bima,” amesema Mtambi.
Kuhusu kampeni ya dawa kinga, amewataka wakazi wa Mara kushiriki kikamilifu kwa kuwaruhusu watoto wa miaka 5 hadi 14 kupata dawa ili kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ifikapo 2030. Alisema bado zipo imani potofu kuhusu dawa hizo, akisisitiza kuwa ni salama na zimethibitishwa na mamlaka husika.
Akitoa taarifa ya kampeni hiyo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk Zabron Masatu, amesema watoto 653,045 wanatarajiwa kupatiwa dawa katika shule 932 mkoani humo. Alisema idara ya afya kwa kushirikiana na wadau inaendelea kutoa elimu ili kuondoa dhana potofu kuhusu kampeni za afya ya jamii.
“Changamoto iliyopo ni imani potofu kuhusu chanjo na kampeni kama hizi, lakini mwitikio unaendelea kuimarika. Mkoa wa Mara unalenga kutokomeza minyoo ya tumbo na kichocho ifikapo 2030,” amesema Dk Masatu.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Wizara ya Afya, Geofrey George, amesema kampeni hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kupambana na magonjwa matano yaliyokuwa hayapewi kipaumbele, ambayo ni mabusha, matende, usubi, minyoo ya tumbo na kichocho.
Amesema kiwango cha maambukizi ya magonjwa hayo mkoani Mara kwa sasa kiko katika daraja la kati, hali inayotoa matumaini ya kutokomezwa kwake ifikapo mwaka 2030.