Serikali: Mafanikio ya mradi wa WASH yaendelezwe
Kiongozi wa Sekta ya Maji wa SNV Tanzania, Olivier Germain akizungumza wakati wa hafla ya kufunga rasmi Programu ya WASH (WS4H) iliyofanyika mkoani Morogoro.
Muktasari:
- Mpango huo umeimarisha uwezo wa taasisi, mifumo ya takwimu, upangaji wa huduma na ujumuishaji wa kijinsia pamoja na ustahimilivu wa tabianchi.
Morogoro. Serikali imewataka washirika wa maendeleo, mamlaka za serikali za mitaa (LGA) na sekta binafsi kuendeleza mageuzi yaliyoanzishwa chini ya Mpango wa Mifumo ya WASH kwa Afya (WS4H), ikieleza kuwa upatikanaji wa muda mrefu wa huduma za maji, usafi wa mazingira na vifaa vya usafi unategemea taasisi imara, uratibu thabiti na ufadhili wa kuaminika badala ya miundombinu pekee.
Wito huo ulitolewa mjini Morogoro leo, Julai 15, 2026 wakati wa kufungwa rasmi kwa mpango huo, ambapo zaidi ya wawakilishi 80 kutoka taasisi za Serikali, washirika wa maendeleo na mashirika ya kiraia walitathmini mafanikio na yaliyojitokeza wakati wa utekelezaji.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, mhandisi mwandamizi wa wizara hiyo katika Idara ya Sera na Mipango, Diana Kimario, amesema hitimisho la mpango huo linaashiria mpito kutoka kwa usaidizi wa wafadhili kwenda kwenye umiliki wa kitaifa.
“Kipimo halisi cha mafanikio kitakuwa jinsi tunavyoendeleza na kukuza miradi ya majaribio, mifumo, ushirikiano na ubunifu ulioanzishwa na mpango huu,” amesema, na kuongeza kuwa Serikali itaunganisha mafanikio hayo katika mipango na bajeti ya kitaifa.
Mpango huo ulitekelezwa katika mikoa ya Dodoma, Arusha na Simiyu kupitia ushirikiano na Wizara ya Maji, Wizara ya Afya na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa), kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uholanzi (SNV) kwa usaidizi wa Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo ya Uingereza (FCDO).
Badala ya kuangazia miundombinu pekee, mpango huo uliimarisha upangaji, usimamizi na utoaji wa huduma kwa kujenga uwezo wa taasisi za mitaa kusimamia mifumo ya maji baada ya ujenzi.
Kimario amesema mpango huo ulisaidia maeneo manane ya kipaumbele, ikiwa ni pamoja na kuifanya sekta ya usambazaji wa maji vijijini kuwa ya kitaalamu kupitia uainishaji wa rasilimali na uunganishaji wa huduma, kuimarisha uwezo wa Ruwasa na Wizara ya Afya, kuboresha mifumo ya kielektroniki ya takwimu kwa ajili ya kufanya maamuzi kwa kuzingatia ushahidi na kuandaa mipango ya udhibiti wa huduma za vijijini kwa awamu.
“Pia ulihamasisha usafi wa mazingira katika wilaya, ukaunganisha ustahimilivu wa tabianchi, usawa wa kijinsia na ujumuishi wa kijamii katika huduma, huku ukiimarisha ufuatiliaji wa sekta na mifumo ya utoaji taarifa,” amesema.
Amezitaka LGA kuasisi zana na mbinu zilizotengenezwa chini ya mpango huo na kuimarisha ufuatiliaji ili kuboresha uwajibikaji.
Pia ametoa wito kwa washirika wa maendeleo kupitisha mbinu za kuimarisha mifumo katika mipango ya baadaye, ikiwa ni pamoja na programu zinazoungwa mkono na Benki ya Dunia na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef).
Kiongozi wa Sekta ya Maji wa SNV, Olivier Germain, amesema kufungwa rasmi kwa mpango huo hakutapunguza mchango wake wa muda mrefu katika sekta hiyo.
“Maarifa, ushirikiano na maboresho ya kimfumo yaliyopatikana kupitia WS4H yataendelea kusaidia juhudi za nchi kutoa huduma za kuaminika na endelevu kwa wananchi wote,” amesema.
Mkazi wa Dodoma, Julieth Kafanabo, amesema, “Kupitia mradi huu, wanawake, vijana na makundi yaliyo katika mazingira magumu waliwakilishwa vyema katika kufanya uamuzi.”