Shehe wa Mkoa wa Pwani aitaka Serikali kuangalia upya Mfumo wa Elimu
Shehe wa Mkoa wa Pwani Khamis Mtupa akiwaongoza waumini wa msikiti wa Mwanalugali Kibaha Mkoa wa Pwani swala hiyo leo Picha na Sanjito Msafiri
Muktasari:
- Shehe wa Mkoa wa Pwani, Khamis Mtupa, amesema ipo haja kwa Serikali kupitia Wizara ya Elimu kuangalia upya mfumo wa elimu nchini akidai shule nyingi zimejikita katika kutengeneza ufaulu mkubwa wa madaraja huku wanafunzi wakikosa uwezo wa kujitegemea na kukabiliwa na changamoto za kiafya kutokana na mizigo mikubwa ya mabegi wanayobeba kila siku.
Kibaha. Swala ya Eid El Adha imefanyika leo Jumatano Mei 27, 2026 katika Msikiti wa Mwanalugali uliopo Manispaa ya Kibaha Mkoa wa Pwani huku viongozi wa dini wakitoa wito kwa Serikali na Watanzania kwa ujumla kuweka vipaumbele katika elimu, malezi na maendeleo ya taifa.
Akizungumza baada ya kuongoza swala hiyo, Shehe wa Mkoa wa Pwani, Khamis Mtupa amesema umefika wakati kwa Wizara ya Elimu kuangalia upya mfumo wa elimu wa sasa kwa madai kuwa shule nyingi zimeweka nguvu kubwa katika kuhakikisha wanafunzi wanapata ufaulu wa juu ili kuitangaza shule husika, lakini wanafunzi hao wanashindwa kujitegemea wanaporejea katika jamii.
“Leo utakuta mwanafunzi anapata Division One lakini akirudi nyumbani hawezi hata kuamka asubuhi bila kuamshwa na mzazi wake. Hapo tunajiuliza elimu hiyo inalisaidiaje taifa kama mtoto hana uwezo wa kujitegemea wala kufanya kazi za kawaida za maisha,” amesema Mtupa.
Shehe wa Mkoa wa Pwani Khamis Mtupa akiwaongoza waumini wa msikiti wa Mwanalugali Kibaha Mkoa wa Pwani swala hiyo leo Picha na Sanjito Msafiri
Amesema taifa linaelekea kuwa na wasomi wengi wasiokuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa jamii ikiwa mfumo wa elimu utaendelea kuzingatia zaidi ufaulu wa karatasi kuliko uwezo wa vitendo na kujitegemea.
“Tunazalisha watoto wanaojivunia ufaulu wa makaratasini lakini kiuhalisia hawana uwezo wa kufanya mambo ya msingi katika maisha yao. Serikali inapaswa kuingilia kati ili kuokoa kizazi hiki,” amesema.
Mtupa pia ameonyesha wasiwasi wake kuhusu afya za watoto kutokana na kubeba mabegi makubwa yenye madaftari mengi kila siku wanapoenda shule.
“Miaka 10 ijayo tunaweza kuwa na watoto wengi wenye matatizo ya migongo na nyonga. Hivi sasa wanafunzi wanabeba mizigo mikubwa mgongoni hadi unawaonea huruma. Mtoto ana ufaulu mkubwa lakini wakati huo huo anajenga ulemavu wa mwili kutokana na mfumo huu,” amesema.
Katika hatua nyingine kiongizi huyo wa kiimani amewataka watanzania kufanya kazi kwa kuweka vipaumbele ili kujenga maendeleo binafsi na ya taifa, akisema jamii isiyokuwa na mipango na vipaumbele sahihi hushindwa kufikia mafanikio.
Amesema kuweka vipaumbele kunasaidia kuongeza ufanisi katika kazi, matumizi sahihi ya muda pamoja na kufikia malengo kwa haraka huku kukosekana kwa vipaumbele kukisababisha kupotea kwa muda, rasilimali na kushuka kwa uwajibikaji.
Kwa upande wake, mkufunzi wa masomo ya dini ya Kiislamu, Shehe Nurdin Kilehiya amesema Watanzania wanapaswa kujijengea utamaduni wa kuweka vipaumbele katika utendaji wa kazi pamoja na kuhakikisha wanawarithisha watoto wao maadili na utamaduni unaokubalika katika jamii.
Shehe wa Mkoa wa Pwani Khamis Mtupa akiwaongoza waumini wa msikiti wa Mwanalugali Kibaha Mkoa wa Pwani swala hiyo leo Picha na Sanjito Msafiri
“Taifa imara huanzia kwenye malezi bora na jamii inayojua wajibu wake. Wazazi wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuwaandaa watoto wao kwa maisha yenye nidhamu, uwajibikaji na kujituma,” amesema Kilehiya.
Naye muumini wa dini hiyo, Sheila Mohammed ameema Serikali inapaswa kufanya tathmini ya kina kuhusu mfumo wa elimu ili kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa yatakayowasaidia kujitegemea baada ya masomo yao.
“Ni vizuri watoto kufaulu lakini elimu hiyo lazima iwajenge kuwa wabunifu, wafanyakazi na watu wanaoweza kujitegemea katika maisha yao ya baadaye,” amesema.
Muumini mwingine, Swaumu Juma ameunga mkono kauli hizo akisema ipo haja kwa jamii kushirikiana na Serikali kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira yanayowaandaa kwa maisha halisi badala ya kutegemea ufaulu wa mitihani pekee.
“Tusipobadilika sasa, tutakuwa na kizazi kinachojua kujibu maswali ya darasani lakini hakina uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha ya kila siku,” amesema.