Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shinikizo la uchunguzi wa fedha Chadema laongezeka

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Chadema Kanda ya Kati, Aquilin Claud (kushoto) na Katibu wa chama hicho, Mkoa wa Morogoro, Baranabas Okola wakizungumza na waandishi wa habari leo Julai, 12 2026.

Muktasari:

  • Sakata la wanaomtuhumu Heche, kuhusu matumizi ya fedha za michango wametoa wito kuundwa kwa tume huru ya uchunguzi huku wakisisitiza uwazi ili kurejesha imani ya wanachama.

Dar es Salaam. Licha ya uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuendelea kuwachukulia hatua viongozi wanaomtuhumu Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, John Heche, kuhusu matumizi ya fedha za michango, shinikizo la kutaka kufanyika uchunguzi huru kuhusu tuhuma hizo limeendelea kuongezeka ndani ya chama.

Wito huo unakuja wakati Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, akisisitiza kuwa viongozi wenye malalamiko wanapaswa kufuata taratibu za chama kwa kuwasilisha ushahidi kupitia vyombo vya ndani badala ya kuzungumza na vyombo vya habari.

Juzi, Mnyika alisema hatua zilizochukuliwa dhidi ya baadhi ya viongozi na wanachama zilizingatia Katiba, kanuni na maadili ya chama, akisisitiza kuwa yeyote asiyeafiki ana haki ya kukata rufaa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Aidha, alikanusha madai ya matumizi mabaya ya fedha za michango maarufu kama Tonetone, akisema fedha hizo hukusanywa na kuwekwa benki kabla ya kutumika kwa mujibu wa taratibu za chama.

Hata hivyo, leo Jumapili Julai 12, 2026, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Chadema Kanda ya Kati, Aquilin Claud, ameongeza sauti ya viongozi wanaotaka ukweli ubainike kwa kuitaka Sekretarieti ya chama kuunda tume huru itakayochunguza tuhuma hizo.

Claud amesema ili uchunguzi uwe huru na wenye kuaminika, kiongozi yeyote anayetuhumiwa anapaswa kujiweka pembeni kwa muda kupisha mchakato huo.

"Fedha za wadau ni mali ya chama na zinapaswa kusimamiwa kwa uwazi. Uchunguzi huru utasaidia kuondoa sintofahamu na kurejesha imani ya wanachama," amesema.

Amesema baada ya uchunguzi kukamilika, chama kinapaswa kuchukua hatua stahiki dhidi ya watakaobainika kukiuka taratibu ili kuzuia migogoro kama hiyo kujirudia.

Pia amewataka viongozi wa Chadema kuweka pembeni tofauti zao na kutafuta suluhu kupitia mazungumzo kwa lengo la kulinda umoja wa chama.

Katika hatua nyingine, aliyekuwa Katibu wa Chadema Mkoa wa Morogoro, Barnabas Okola, amekanusha madai ya Mnyika kwamba alipokea Sh2 milioni ili kutoa tuhuma dhidi ya Heche.

Okola amesema madai hayo hayana ushahidi na yanachafua heshima yake, akisisitiza kuwa msimamo wake ulikuwa ni kutaka uchunguzi ufanyike ili ukweli ujulikane.

Amesema viongozi wa chama hawapaswi kuwa juu ya uchunguzi na kwamba atatumia taratibu za chama kupinga hatua zilizochukuliwa dhidi yake baada ya kuondolewa katika nafasi ya Katibu wa Chadema Mkoa wa Morogoro.

Shinikizo hilo linaongezeka wakati Chadema ikiendelea kuwachukulia hatua viongozi waliojitokeza hadharani kumtuhumu Heche kutumia fedha za michango kwa masilahi binafsi.

Waliochukuliwa hatua hadi sasa kutokana na kutoa shinikizo hilo la kutaka Heche akae pembeni ni pamoja na Katibu wa Jimbo la Bumbuli, Abubakari Mashambo, aliyepokonywa wadhifa wake; aliyekuwa Katibu wa Chadema Mkoa wa Morogoro, Barnabas Okola; pamoja na wenyeviti wa Chadema Wilaya za Mkinga na Kilindi mkoani Tanga, Amuli Shindo, Joseph Mwakidasi na Mathias Cosmas.

Uongozi wa Chadema umeeleza kuwa hatua hizo zinalenga kulinda nidhamu ya chama, ukisisitiza kuwa malalamiko yote yanapaswa kushughulikiwa kupitia vyombo vya ndani kwa mujibu wa Katiba na kanuni za chama.