Tafico kuendesha miradi ya uvuvi kwa PPP, Serikali yataka matokeo ya uwekezaji
Dar es Salaam. Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Bashiru Ally ameielekeza Shirika la Uvuvi Tanzania (Tafico) kuharakisha utekelezaji wa miradi yake ya kimkakati kwa kutumia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), akisema Serikali inataka kuona uwekezaji uliofanywa ukianza kuleta matokeo ya kibiashara na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Dk Bashiru alisema hayo jana Julai 13, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akizindua Bodi ya Pili ya Wakurugenzi wa Tafico, ambapo aliipa bodi hiyo maelekezo tisa yenye lengo la kuimarisha shirika hilo na kulifanya kuwa injini ya uchumi wa buluu nchini.
Alisema Tafico imefikia hatua muhimu ambayo inahitaji kuondoka kwenye maandalizi na kuanza uzalishaji wa kibiashara kupitia miradi iliyopangwa, ikiwemo uvuvi wa bahari kuu, uchakataji na uongezaji thamani wa mazao ya uvuvi pamoja na ukuzaji wa viumbe maji.
“Tafico ipo katika hatua muhimu ya kujenga msingi wa uzalishaji wa kibiashara kupitia miradi ya kimkakati. Jukumu lenu si kuanza upya safari ya shirika, bali kuhakikisha uwekezaji uliofanywa na unaoendelea unazaa matokeo chanya ya kibiashara na maendeleo kwa Taifa,” alisema.
Alisema Serikali tayari imewekeza katika miundombinu ya sekta ya uvuvi, ikiwemo Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko, huku ikiendelea kuweka mazingira ya kuvutia wawekezaji katika uvuvi wa bahari kuu.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, baadhi ya miradi ya Tafico itatekelezwa kwa mfumo wa PPP ili kuongeza ufanisi, mitaji na utaalamu kutoka sekta binafsi.
Aliitaka bodi mpya kuhakikisha mradi wa meli ya uvuvi wa bahari kuu unakamilika kwa wakati na kuanza shughuli za uzalishaji wa kibiashara kwa kasi, akisema mradi huo ni miongoni mwa hatua muhimu katika kukuza uchumi wa buluu.
Mbali na hilo, aliitaka bodi kupitia upya Mpango Mkakati wa Tafico pamoja na mipango ya biashara ya miradi yake ili iendane na vipaumbele vya Serikali, huku ikiimarisha ushirikiano na taasisi za fedha, washirika wa maendeleo na wawekezaji binafsi.
Dk Bashiru pia aliitaka bodi kuboresha maandiko ya miradi ili kurahisisha upatikanaji wa fedha, kuimarisha rasilimali watu na masilahi ya watumishi, kupitia upya muundo wa shirika, kuhakikisha uwazi katika matumizi ya rasilimali na kufuatilia mali za Tafico.
Katika hafla hiyo, alimpongeza Mwenyekiti wa Bodi ya Tafico, Profesa Yunus Mgaya, kwa kuaminiwa kuendelea kuiongoza bodi hiyo kwa awamu ya pili, akisema uzoefu wake utasaidia kuongeza kasi ya utekelezaji wa mipango ya shirika.
Akizungumza kwa niaba ya bodi, Profesa Mgaya alisema watahakikisha maelekezo yote yanatekelezwa kwa kushirikiana na Menejimenti ya Tafico pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
“Tutahakikisha Tafico inaingia kwenye ukuaji, taasisi inasimamiwa kwa uwazi, miradi inafuatiliwa kwa karibu na uwekezaji unaendelea. Tunataka mchango wa shirika uonekane wazi kupitia utawala bora, uwajibikaji na tija,” alisema.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Tafico, Shaibu Matessa alisema shirika linaendelea kujenga msingi wa kuwa taasisi imara ya kibiashara kupitia uwekezaji katika uvuvi wa bahari kuu, hususan samaki aina ya jodari na jamii zake pamoja na miradi ya ukuzaji wa viumbe maji.
Alisema hadi Juni 30, 2026, Tafico ilikuwa na watumishi 63 na imekamilisha maandalizi ya miradi mbalimbali ya kuongeza mapato ya ndani, ikiwemo ukuzaji wa kamba, uzalishaji wa chakula cha samaki na utengenezaji wa zana za uvuvi.
Matessa alisema shirika pia limepanua ushirikiano na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuvutia mitaji, kuhamisha teknolojia na kuongeza uwezo wa uzalishaji wa mazao ya uvuvi.
Alisema ushirikiano huo unalenga kuiwezesha Tafico kuwa kitovu cha biashara ya uvuvi na kuchangia zaidi katika uchumi wa buluu wa Tanzania.