TASAC yatwaa tuzo ya umahiri uandaaji wa hesabu taasisi za Serikali 2024
Muktasari:
- Mkurugenzi wa Fedha TASAC, Pascal Karomba amesema kupata tuzo hiyo kunadhihirisha dhamira ya Shirika katika kuimarisha usimamizi wa fedha.
Dar es Salaam. Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeibuka mshindi wa pili tuzo ya umahiri katika uandaaji bora wa hesabu za fedha kwa kuzingatia viwango vya uandaaji hesabu vya kimataifa (IFRS) katika tuzo zilizotolewa na Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu nchini (NBAA).
Tuzo hiyo imepokewa na Mkurugenzi wa Fedha wa TASAC, Pascal Karomba kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, katika hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya APC, Bunju jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kukabidhi tuzo hizo, Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula aliyemwakilisha Waziri wa Fedha amesema kuwa taarifa za mahesabu zilizoandaliwa kwa viwango sahihi ni msingi muhimu wa maendeleo ya taasisi na uchumi wa taifa.
"Taarifa hizi za mahesabu ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa taasisi na taifa kwa ujumla," amesema Luswetula.
Luswetula, amezipongeza taasisi zote 86 zilizoshiriki hususani zile zilizoshinda kwa kufuata viwango vya kimataifa vya uandaaji wa taarifa za fedha,
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Fedha TASAC Karomba amesema kupata tuzo hiyo kunadhihirisha dhamira ya Shirika katika kuimarisha usimamizi wa fedha, uwazi, na uwajibikaji kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya uandaaji wa taarifa za kifedha.
Mamlaka imeendelea kuonesha mfano wa uwazi, uwajibikaji na weledi katika usimamizi wa fedha, kwa kupata hati safi ya ukaguzi kutoka Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) iliyopelekea kutwaa Tuzo hiyo ya umahiri kupitia NBAA.
Ushindi wa TPA unatokana na uwasilishaji wa taarifa bora za Fedha zilizoakisi uwazi kwa kufuata viwango vya kimataifa vya uandaaji wa hesabu (IFRS) ikiwasilisha taarifa bora za fedha zilizoakisi uwazi, utekelezaji makini wa bajeti na uwajibikaji wa kimenejimenti katika miradi ya kimkakati.