TPA yaboresha mfumo uendeshaji bandari ikifuata wa kimataifa
Muktasari:
- Miongoni mwa bandari zinazotumia mfumo wa kimataifa kama vile wa ada na tozo kujiboresha na kuendelea kuwa vinara wa biashara ya baharini duniani ni Bandari ya Rotterdam nchini Uholanzi, Bandari ya Singapore nchini Singapore
Dar es Salaam. Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeanza kupita njia zinazotumiwa na baadhi ya bandari kubwa duniani ili kuongeza tija, kuvutia uwekezaji na kuimarisha ushindani wa Tanzania katika biashara ya kimataifa.
Taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo leo Juni 5, 2026, imeeleza kuwa hatua hiyo inakuja wakati mamlaka hiyo ikiwa imetangaza kuanza kutekeleza tozo ya maendeleo ya miundombinu ya bandari (Ports Infrastructure Development Levy).
Mfumo unaolenga kuwezesha upatikanaji wa rasilimali za kuendeleza magati, kuongeza uwezo wa bandari, kuboresha huduma za usafirishaji wa mizigo na kuandaa miundombinu ya kukidhi mahitaji ya biashara ya miaka ijayo.
Tozo hiyo ya maendeleo ya miundombinu ya bandari, ambayo inatarajiwa kuanza kutumika Julai 1, 2026 kwa kiwango cha asilimia 4.5 ya thamani ya CIF ya shehena baada ya kupunguzwa kutoka asilimia 9.
Miongoni mwa bandari zinqzotumia mfumo huo wa ada na tozo kujiboresha na kuendelea kuwa vinara wa biashara ya baharini duniani ni Bandari ya Rotterdam nchini Uholanzi, Bandari ya Singapore nchini Singapore, Bandari ya Shanghai na Hong Kong nchini China, Bandari ya Los Angeles nchini Marekani, Bandari ya Hamburg nchini Ujerumani, Bandari ya Antwerp nchini Ubelgiji, Bandari ya Jebel Ali nchini Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na Bandari ya Tanger Med nchini Morocco.
Bandari hizi zimekuwa zikihudumia mamilioni ya makontena na mamia ya mamilioni ya tani za mizigo kila mwaka, zikiunganisha mabara mbalimbali kupitia biashara ya mafuta, gesi, magari, bidhaa za viwandani, malighafi za uzalishaji, bidhaa za kilimo na bidhaa za matumizi ya kila siku.
Inaelezwa kuwa bandari hizo kwa miaka mingi zimekuwa zikitumia tozo na ada mbalimbali za watumiaji wa bandari kama chanzo muhimu cha fedha za kuendeleza miundombinu yake, hatua iliyoziwezesha kuendelea kupanua uwezo wa kuhudumia mizigo, kuvutia biashara zaidi na kuimarisha nafasi yake katika uchumi wa dunia.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa sekta ya usafirishaji na biashara ya baharini, ushindani wa bandari za kisasa haujengwi na huduma za leo pekee, bali hujengwa na uwezo wa kuandaa mahitaji ya miaka 10, 20 na hata 30 ijayo.
Ndiyo maana bandari nyingi kubwa duniani zimeendelea kuongeza magati mapya, kupanua maeneo ya bandari, kuongeza kina cha njia za meli, kujenga reli za mizigo, maeneo ya logistics na kuwekeza katika mifumo ya kisasa ya teknolojia ili kuendelea kuvutia biashara zaidi.