Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TPRB yafungua milango Sabasaba, yapokea maombi ya usajili

Muktasari:

  • Bodi ya Usajili wa Wataalam wa Mipangomiji (TPRB) imeendelea kutoa huduma za usajili kwa wataalamu wa mipangomiji kupitia Maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba, hatua inayolenga kusogeza huduma karibu na wadau na kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo.

Dar es Salaam. Wataalamu wa mipangomiji wamepata fursa ya kupata huduma za usajili kwa urahisi kupitia Maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba, baada ya Bodi ya Usajili wa Wataalam wa Mipangomiji (TPRB) kufungua huduma zake kwa wadau wanaotembelea maonesho hayo.

Katika banda la TPRB lililopo ndani ya Banda la Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wataalamu hao wanapokea huduma mbalimbali ikiwamo kuwasilisha maombi ya usajili, kupatiwa maelekezo ya taratibu zinazohitajika pamoja na ushauri kuhusu masuala yanayohusu taaluma ya mipangomiji.

Maofisa wa Bodi wamekuwa wakitoa huduma ana kwa ana kwa waombaji, hatua inayolenga kupunguza changamoto za upatikanaji wa huduma hizo na kuhakikisha wataalamu wanapata usaidizi wa karibu wakati wa mchakato wa usajili.

Kaimu Msajili wa TPRB, Martha Mkupasi, amesema ushiriki wa Bodi katika maonesho hayo ni sehemu ya juhudi za kuwafikia wadau wengi zaidi na kusogeza huduma za usajili karibu na wananchi.

Amesema mbali na kupokea maombi ya usajili, Bodi pia inatumia jukwaa hilo kutoa elimu kuhusu majukumu yake, shughuli za mipangomiji pamoja na kupokea maoni na changamoto kutoka kwa wadau.

“Tunataka kuhakikisha wataalamu wanapata huduma kwa urahisi na kuelewa taratibu za usajili. Sabasaba imetupa nafasi nzuri ya kukutana nao moja kwa moja,” amesema.

Katika maonesho hayo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Leonard Akwilapo, alitembelea banda la TPRB na kupongeza jitihada za Bodi katika kuboresha utoaji wa huduma na kuwafikia wananchi.

Waziri alisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa umma na kuhakikisha huduma zinazotolewa na taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo zinakuwa bora na zenye manufaa kwa wananchi.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Lucy Kabyemela, alitembelea banda hilo na kujionea huduma zinazotolewa huku akiipongeza TPRB kwa hatua ya kusogeza huduma zake karibu na wadau.

Maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba yalianza Juni 28, 2026 na yanatarajiwa kufikia tamati Julai 13, 2026 jijini Dar es Salaam.