Vunjo yajipanga kufufua zao la kahawa, miche 500,000 ya kisasa ikipandwa
Katibu wa Mbunge Jimbo la Vunjo, Iddi Mfinanga akizungumza kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo hilo, Enock Koola wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Marangu Mashariki kujadili masuala mbalimbali ya zao la kahawa.Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Hatua hiyo inalenga kulifufua zao hilo la kahawa kwa kuongeza tija katika uzalishaji wake, kuinua kipato cha wakulima, na kurejesha hadhi ya kahawa kama zao muhimu la biashara katika eneo hilo.
Moshi. Wakati Jimbo la Vunjo, Mkoani Kilimanjaro likipanga kuotesha miche 500,000 ya kahawa ya kisasa katika msimu huu wa 2025/26, vijana wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuongeza nguvu ya uzalishaji wa zao hilo.
Wito huo umetolewa ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulifufua zao la kahawa ambalo kwa miaka ya nyuma lilikumbwa na misukosuko ya bei na kusababisha kupungua kwa ari ya wakulima kulizalisha.
Kwa sasa, kahawa ghafi ya Arabika(CPU-Parchment) imepanda kutoka Sh10,000 iliyokuwa msimu uliopita hadi Sh11,074 kwa kilo msimu huu, huku Robusta(maganda) ikiuzwa Sh Sh3,664 kwa kilo
Akizungumza leo Machi 19, 2026 kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo hilo, Enock Koola, Katibu wake, Iddi Mfinanga katika mkutano wa hadhara uliowakutanisha wakulima wa kahawa, kata ya Marangu Mashariki, amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza tija, kuinua kipato cha wakulima na kurejesha hadhi ya kahawa kama zao muhimu la biashara katika eneo hilo.
"Tunataka heshima ya kahawa kwenye eneo letu la Vunjo inarudi kama ilivyokuwa awali, kwani zao hili lilitusomesha, tulijenga, tulioa kwasababu ya kahawa sasa tunataka heshima ile irudi kwa wananchi wetu,"amesema Mfinanga
Aidha, amewataka wazee ambao ni wakongwe katika tasnia hiyo ya kahawa kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri ya kuwarithisha vijana zao hilo ili liweze kuwa ni endelevu kwa vizazi vijavyo.
"Nitoe rai kwa wazee wetu, hawa vijana ambao wanakuwa hebu tuwarithishe namna ya kulima na kuandaa mashamba ya kahawa, tushikamane na vijana hawa ili tuweze kuwarithisha utaalamu wa kuhudumia zao letu hili la kahawa ili tuzalishe kwa tija,"amesema Mfinanga
Wakulima wa kahawa kata ya Marangu Mashariki, Jimbo la Vunjo Mkoani Kilimanjaro, wakimsikiliza Katibu Mkuu a Mbunge wa Jimbo hilo, Iddi Mfinanga wakati wa mkutano uliowakutanisha wakulima hao katika kata hiyo.Picha na Janeth Joseph
Aidha, amewaondoa hofu wakulima hao, na kusema Mbunge wa Jimbo hilo, anafanya kila jitihada za kuhakikisha wakulima wa kahawa katika kata hiyo, wanzalisha kwa tija na wale wakulima ambao wanadai fedha katika vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) kwa muda mrefu fedha zao zinalipwa ili waendelee kufurahia kilimo hicho.
"Mbunge wetu Koola amedhamiria kuweka juhudi za ziada kuhakikisha kwamba tunafufua zao la kahawa katika ukanda wetu na kuwa zao tegemewa tena, ameweza kuonana na viongozi mbalimbali wa serikali kuona ni kwa namna gani tunaweza kuboresha hili zao letu ili kahawa iweze kurudi kama ilivyokuwa zamani,"amesema Mfinanga
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kata hiyo, Innocent Shirima amesema endapo ufufuaji wa zao hilo la kahawa utarejea kama ilivyokuwa hapo awali, italeta manufaa makubwa kwa wananchi na kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja.
"Tukiweza kuunga mkono hii ajenda vizuri, tukarudisha zao la kahawa tutapiga hatua kubwa, ukiangalia leo hii kilo ya kahawa ni zaidi ya Sh Sh10,000, hivyo tukirudisha kulima zao hili, tutanyanyua uchumi wa Wanamarangu Mashariki.Tuhamasishane kulima zao hili, ni zao lenye kuleta mafanikio chanya, naamini kila mmoja akioteshe kahawa tutarudi kama zamani,"amesema Diwani huyo
Naye, Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya wilaya ya Moshi, Magabu Mongela, amesema kutokana na maombi ya Mbunge wa Jimbo hilo, kuhusu miche 500,000 ya kahawa, itatolewa na itaanza kupandwa katika msimu huu unaomalizika wa 2025/26.
"Mbunge ameomba miche 500,000 kwa ajili ya Vunjo, kwa msimu huu wa mwaka 2025/26, tutagawa miche hii na tunaomba wananchi muioteshe na kama una miche ya zamani iondoe ioteshwe hii mipya,"amesema