Vyama vya siasa vyaonywa kuelekea uchaguzi mkuu
Muktasari:
- Katika kipindi hiki cha maandalizi ya uchaguzi, elimu juu ya athari ya rushwa inapaswa kutolewa ili kuisaidia jamii kushiriki uchaguzi mkuu na kuelimisha kuhusu madhara ya rushwa na utakatishaji fedha.
Dodoma. Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mwanaidi Ali Hamis, amevionya vyama vya siasa kuepuka vitendo vya rushwa na utakatishaji fedha katika kipindi hiki cha maandalizi ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Ametoa onyo hilo leo Jumatatu, Agosti 11, 2025, wakati akifungua kongamano la mwaka la wiki ya mashirika yasiyo ya kiserikali linalofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma. Kongamano hilo linatarajiwa kudumu kwa siku tatu.
Mwanaidi amesema mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) ni nyenzo muhimu katika maendeleo ya jamii, hivyo yanapaswa kuhakikisha yanatekeleza wajibu wao ipasavyo kulingana na changamoto zilizopo.
“Katika kipindi hiki cha maandalizi ya uchaguzi, mnatakiwa kutoa elimu itakayoisaidia jamii kushiriki uchaguzi mkuu na kuelimisha kuhusu madhara ya rushwa na utakatishaji fedha, ambavyo kwa kiasi kikubwa hufanyika katika nyakati kama hizi,” amedai Mwanaidi.
Amedai kuwa mara nyingi vyama vya siasa hutumia mashirika hayo kufanikisha malengo yao, lakini Serikali ipo makini kufuatilia mwenendo huo.
Aidha, amesema tathmini ya mashirika yasiyo ya kiserikali ni msingi wa mafanikio ya ushirikiano wao na Serikali, ili kuimarisha utendaji kazi unaozingatia weledi.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa mashirika hayo, ambaye pia ni Meneja wa Uhusiano kutoka Benki ya Stabic, Naomi Nduse amesema wataendelea kushirikiana na Serikali kusaidia jamii kupitia miradi ya elimu, afya na misaada ya kisheria kwa wananchi wanaokabiliwa na changamoto hizo.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Amoni Mpanju amesema kongamano hilo ni jukwaa muhimu la kuunganisha Serikali na mashirika hayo katika kutekeleza majukumu ya ujenzi wa Taifa.
“Lengo letu ni kutathmini mafanikio, changamoto na fursa zilizopo, pamoja na kuweka mikakati yenye malengo ya kuisaidia jamii kufikia maendeleo makubwa,” amesema Mpanju.
Ameongeza kuwa katika kongamano hilo, kutatolewa huduma mbalimbali bure kwa jamii ikiwemo za afya, elimu juu ya masuala mbalimbali, pamoja na msaada wa kisheria.