Wadau wa michezo wajitokeza kuinusuru African Sport kushuka daraja
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdallah akizungumza na wachezaji na viongozi wa timu ya African Sport wakati wa hafla ya chakula cha jioni nyumbani kwake, iliyolenga kuweka mikakati ya maendeleo ya timu hyo dhidi ya kushuka daraja. Picha na Mbonea Herman.
Muktasari:
- Timu hiyo inayoshiriki Championship ipo nafasi ya 15 kati ya timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo, hali ambayo ni hatari kubwa na endapo tahadhari haitachukuliwa, inaweza kushuka daraja.
Tanga. Wadau wa klabu ya African Sport ya Tanga wametenga Sh 45 milioni ili kuwezesha timu yao kubaki ligi daraja la kwanza.
Wadau wameweka malengo ya pamoja kuhakikisha timu hiyo inarejea kwenye ubora wake, akisisitiza kuwa bila mipango madhubuti kuna hatari ya kushuka daraja na kurudi daraja la chini.
Timu hiyo imecheza michezo tisa, ambapo sita ni ya nyumbani na mitatu ya ugenini,ili kubaki daraja la kwanza, inabidi ishinde mechi zote japokuwa ikishinda michezo sita pia inaweza kubaki.
Pia, ipo nafasi ya 15 kati ya timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo, hali ambayo ni hatari kubwa na endapo tahadhari haitachukuliwa, inaweza kusababisha kushuka daraja.
Makamu Mwenyekiti wa klabu ya African Sport, Hamza Bwanga akizungumza na wachezaji wa timu hiyo wakati wa hafla ya chakula cha jioni kwa ajili ya kujadili namna ya kujinafsua kwenye nafasi ya kushuka daraja kwenye michuano ya Championship. Picha na Mbonea Herman
Akizungumza Machi 11, 2026 kwa niaba ya wananchama wa klabu hiyo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdallah amesema Ili kushinda mechi hizi ipo mikakati madhubuti iliyopangwa ambapo viongozi wameona ikipatikana kiasi hicho cha fedha itasaidia timu kubaki daraja la kwanza, mimi nimewahakikishia nitatafuta wadau wa kutuunga mkono, Mbunge wa Tanga Kassim Makbel ameahidi kutoa sh5 milioni.
Katika kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa kwa upande wa Abdallah amechangia Sh20 milioni ambazo tayari zimeweka kwenye akaunti ya klabu, na mdau mwingine ameahidi kutoa milioni 20 Jumatatu.
“Kabla ya kuwa daraja la kwanza tulikuwa daraja la pili,mimi nilifanya jitihada kuhakikisha klabu hii inafanikiwa,lengo letu ni kurudisha heshima ya mpira wa Tanga kwenye ushindani wa soka,” amesema Abdallah.
Amesema viongozi wamekaa na kujitathmini na kuona changamoto mbalimbali zinazoikabili klabu hiyo, akibainisha kuwa sasa ni muda wa kujisahihisha na kufanya kazi kwa umoja.
“Tumekaa na viongozi tumeona changamoto nyingi ambazo klabu hii inapitia,inapaswa sisi wenyewe kama viongozi tujisahihishe,tunashukuru viongozi wa klabu yetu mnaonyesha dhamira njema na mmeanza kujirekebisha kwenye mapungufu yaliyokuwepo,” amesema
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdalah akizungumza na wachezaji na viongozi wa timu ya African Sport wakati wa hafla ya chakula cha jioni nyumbani kwake, iliyolenga kuweka mikakati ya maendeleo ya timu hyo dhidi ya kushuka daraja. Picha na Mbonea Herman.
Rajab amesema wachezaji hawapaswi kulaumiwa moja kwa moja, akieleza kuwa changamoto za klabu zimeweza kuathiri hali ya kisaikolojia ya wachezaji.
“Hatuwezi kuwalaumu wachezaji wetu hata siku moja,changamoto za klabu yetu ni kubwa, mchezaji akiona wazazi wake ambao ndio waliomsajili wanapitia changamoto kubwa, anaweza kuathirika kisaikolojia. Kwa hiyo tumekubaliana viongozi kwanza tukae sawa kuhakikisha klabu haishuki daraja,” amesema
Hata hivyo, amesema wachezaji wanapaswa kuelewa historia ya klabu yao ambayo ni kubwa na yenye heshima nchini, akibainisha kuwa African Sports ina ushindani wa muda mrefu na Coastal Union.
Wachezaji wa timu ya African Sport wakiwa kwenye hafla ya chakula cha jioni kilichoambatana na namna gani timu hiyo inatakiwa kufanya vizuri kwenye mechi zake. Picha na Mbonea Herman
“Wachezaji wetu wanatakiwa kujua historia ya timu yao kuwa ni timu kubwa, klabu yenye heshima kubwa nchini katika historia ya mpira wetu. Mshindani wa Coastal Union nchini ni African Sports, lakini Coastal Union haiwezi kufanya vizuri Ligi Kuu kama African Sports haitarudi,” amesema Rajab.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Hamza Bwanga, amesema moja ya mikakati yao ni kuhakikisha wanatangaza mechi ili kuongeza idadi ya mashabiki uwanjani badala ya kuangalia nyumbani kupitia runinga.
Amesema tayari wameanza kutumia gari la matangazo kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi uwanjani kabla ya mechi zao.
“Tumebakisha mechi tisa, sita tunacheza nyumbani,tutatumia gari la matangazo kuhamasisha wananchi siku tatu kabla ya mechi ili kujaza uwanja na kuwapa wachezaji morali,” amesmea Bwanga.
Aliongeza kuwa wameanza pia kusuluhisha tofauti za ndani ya klabu na sasa kuna hatua kubwa ya usawa na mshikamano.
Naye nahodha wa African Sports, Ayubu Masoud, ameahidi kuiokoa timu hiyo na kuirudisha kwenye hadhi yake ya awali, akisema kikosi kimepata mafunzo na sasa kina uwezo wa kupambana na kubadilisha hali.
“Tunaishukuru sana uongozi kwa msaada mkubwa, mimi nimekaa hapa kwa takribani miaka kumi nimeona mengi,tumepitia changamoto nyingi lakini sasa tuna matumaini mapya,” amesema Masoud.
Amesema msaada wa usafiri na mazingira bora ya timu umeongeza morali kubwa kwa wachezaji, na kuahidi kupambana kuhakikisha African Sports inabaki daraja la juu.