Wadau wahimiza matumizi ya usuluhishi kutatua migogoro
Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika kilele cha Wiki ya Usuluhishi wa Migogoro kwa Njia Mbadala wakipatiwa huduma na kusikilizwa changamoto zao na maofisa usuluhishi, katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Elimu kwa umma kuhusu faida za utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala yatakiwa kuimarishwa ili kupunguza msongamano wa kesi mahakamani na kukuza amani na maendeleo.
Dar es Salaam. Wadau wa sekta ya sheria wamewataka Watanzania kukumbatia njia mbadala za utatuzi wa migogoro (ADR), wakieleza kuwa husaidia kupunguza gharama, kuokoa muda na kujenga jamii yenye amani badala ya kukimbilia mahakamani.
Wito huo umetolewa wakati wa kilele cha Wiki ya Usuluhishi wa Migogoro kwa Njia Mbadala, iliyoanza Aprili 13 na kuhitimishwa Aprili 17, katika Mahakama Kuu ya Usuluhishi wa Migogoro kwa Njia Mbadala jijini Dar es Salaam.
Wadau hao wamesema tofauti na mahakama, ambako majaji hutoa maamuzi kwa kuzingatia misingi ya kisheria, usuluhishi huziwezesha pande zinazohusika kufikia mwafaka kwa hiari, hivyo kuondoa uhasama na kudumisha mahusiano.
Wakili kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Peter Mbogoro akieleza umuhimu wa jamii ya Watanzania wanavyotakiwa kuchangamkia fursa ya Utatuzi migogoro kwa njia mbadala.
Akizungumza katika hafla hiyo, Wakili kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Peter Mbogoro amesema changamoto kubwa inayokwamisha matumizi ya mfumo huo ni uelewa mdogo miongoni mwa wananchi.
“Mara nyingi mwananchi anapomfuata wakili anatarajia kushinda kesi. Unapomshauri kutumia usuluhishi, anaweza kudhani wakili hana uwezo,” amesema.
Amesema kuongezwa kwa elimu ya umma kutasaidia wananchi kuelewa kuwa usuluhishi si dalili ya kushindwa, bali ni njia bora ya kupata suluhu ya haraka na yenye manufaa kwa pande zote.
Kwa upande wake, Msuluhishi kutoka wizara hiyo, Erick Mukiza amesema wanashughulikia migogoro yote ya madai, iwe ipo nje au ndani ya mahakama, mradi ipate kibali husika.
Ameeleza kuwa hata kesi zilizo katika hatua za rufaa au utekelezaji zinaweza kushughulikiwa kupitia usuluhishi, jambo linalorahisisha upatikanaji wa haki kwa wakati.
“Usuluhishi unatoa majibu ya haraka. Tofauti na kesi za mahakamani zinazoweza kuchukua miaka, mchakato huu unaweza kukamilika ndani ya muda mfupi,” amesema.
Mukiza ameongeza kuwa gharama za kuendesha kesi mahakamani, zikiwemo ada za mawakili na muda wa kufuatilia mashauri, ni kubwa ukilinganisha na usuluhishi.
Msuluhishi aliyesajiliwa na Wizara ya Katiba na Sheria, Erick Mukiza, akizungumza kuhusu umuhimu wa kutoa elimu kwa jamii juu ya faida za kutumia njia mbadala za utatuzi wa migogoro, akisisitiza kuwa husaidia kupunguza gharama, kuokoa muda na kujenga mahusiano mema miongoni mwa wananchi.
Hata hivyo, ametaja changamoto zinazoikabili mfumo huo kuwa ni pamoja na uelewa mdogo wa wananchi na wakati mwingine ugumu wa kuwakutanisha pande zinazohusika.
“Mara nyingi mlalamikaji hudhani tutakuwa upande wake, wakati jukumu letu ni kusimama katikati na kupatanisha,” amesema.
Mkazi wa Ubungo Makoka, Zamiani Kisimbo amesema alinufaika na huduma hiyo baada ya kupata elimu kuhusu uwepo wake, akieleza kuwa alipata msaada kufuatilia mgogoro wa ardhi ya hekta 50 aliyodai kunyimwa katika eneo la Mvomero, Morogoro.
“Nimepokelewa vizuri na kuelekezwa namna ya kufuatilia haki yangu. Imekuwa faraja kubwa kwangu,” amesema.
Kwa upande wake, Wakili wa kujitegemea, Warehema Kibaha amesema usuluhishi una manufaa makubwa, ikiwemo kuimarisha mahusiano na kuondoa migogoro ya muda mrefu.
“Ulimwengu wa sasa unahitaji mazungumzo zaidi. Mahakama hutoa uamuzi, lakini usuluhishi hujenga uaminifu na kuondoa vinyongo,” amesema.
Ameongeza kuwa licha ya baadhi ya mawakili kuhofia kupungua kwa kazi, bado wana nafasi muhimu katika kutoa ushauri na elimu kwa wateja kuhusu njia sahihi za kutatua migogoro.
“Tutahamasisha zaidi matumizi ya mfumo huu, kwani unaweza kumalizika ndani ya siku 30,” amesema.