Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wafanyakazi wa nyumbani wana haki, walindwe kisheria

Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Usekelege Mpulla, amewataka wafanyakazi wa nyumbani  nchini kutambua thamani yao na kutokubali kunyimwa au kukandamizwa haki zao mahali pa kazi.

Pia amesema sheria za ajira na mahusiano mahali pa kazi inawalinda wao sawa na wafanyakazi wengine wote nchini.

Akizungumza jana Jumamosi Julai 18,2026 mkoani Morogoro wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya  wafanyakazi wa nyumbani kutoka mkoa huo yaliyoandaliwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa kushirikiana na Chama cha kutetea watumishi wa hifadhi, majumbani, watoa huduma na wa kwenye mahoteli nchini Tanzania (Chodawu), Mpulla alisema wafanyakazi wa nyumbani hawatakiwi kujiona wanyonge kutokana na sheria za nchi zinawatambua.

Alisema pamoja na sheria zilizopo pia CMA ipo kwa ajili ya kupokea na kushughulikia migogoro ya wafanyakazi wote bila ubaguzi, huku wafanyakazi wa nyumbani  wakipewa kipaumbele kutokana na mazingira yao ya kazi.

"Msijione wanyonge, sheria imewatambua na inawalinda kama wafanyakazi wengine wote. Tume ya Usuluhishi na Uamuzi inapokea migogoro ya wafanyakazi wote pasipo kubagua, na kwa upekee wenu sisi tunatoa kipaumbele ili kuhakikisha mnapata haki zenu kwa wakati.”

''Mara nyingi wafanyakazi wa nyumbani hukumbana na changamoto za kunyimwa stahiki zao za msingi ikiwemo mishahara, mapumziko na mazingira bora ya kazi, lakini CMA ipo kuhakikisha haki hizo zinalindwa kwa mujibu wa sheria,''alisema.

Mpulla alisema Tanzania imeendelea kuimarisha mifumo ya kulinda haki za wafanyakazi kwa kuzingatia miongozo na viwango vya kimataifa vya utatuzi wa migogoro ya kazi, jambo linalolenga kuhakikisha kila mfanyakazi anapata haki yake bila upendeleo.

Aidha, aliwahamasisha wafanyakazi wa nyumbani kutumia mfumo wa kidijitali wa e-Utatuzi, ambao unawawezesha kuwasilisha migogoro yao bila kufika katika ofisi za CMA na kwa wakati wowote.

Kwa Upande wake, muelimisha rika kutoka  mkoani Morogoro ambaye pia ni Mwenyekiti wa wafanyakazi wa nyumbani mkoani humo, Desdelia Haule, aliwashukuru ILO kwa kuwapatia mafunzo wafanyakazi hao wa nyumbani kutoka maeneo mbalimbali na kuahidi kilichofundishwa kwenda kufanyiwa kazi.

Alisema asilimia kubwa ya wafanyakazi hao hawakuwa wanajua haki zao za msingi mahali pa kazi na wala kujua wajibu wao na wawaajiri wao, hivyo mafunzo hayo yamewafungua fikra ya kuona nao ni wafanyakazi kama walivyo wengine kutoka sekta nyingine nchini.

''Nashukuru ILO kutupa heshima ya kutupatia mafunzo haya kwa mkoa wetu, tutatumia nafasi hii kwa kuwapa elimu wafanyakazi wengine wa nyumbani kujua sheria ya ajira na mahusiano kazini, kujua haki zao na wajibu wao na waajiri mahali pa kazi,''alisema  

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ambaye ni mfanyakazi wa nyumbani, Salama Rashid alisema kabla ya mafunzo hayo wafanyakazi wengi wa nyumbani wa mkoa huo hawakuwa wanatambua haki zao na mara nyingi walifanya kazi bila kuwa na mikataba rasmi ya ajira.

“Tumefundishwa kuhusu umuhimu wa mikataba ya kazi, muda wa mapumziko, likizo ya ugonjwa na haki nyingine za msingi. Haya ni mambo ambayo wengi wetu hatukuwa tunayafahamu. Sasa tunatoka hapa tukiwa na uelewa mkubwa zaidi wa haki na wajibu wetu,” alisema.

Alisema kuwa baada ya mafunzo hayo, washiriki wamejipanga kwenda kutoa elimu kwa wafanyakazi wengine wa nyumbani ambao hawakupata fursa ya kuhudhuria ili kuhakikisha taarifa hizo zinawafikia wengi zaidi.