WanaCCM 24 wajitokeza kinyang’anyiro cha ubunge Kongwa
Muktasari:
- Ndugai, aliyeongoza Jimbo la Kongwa tangu mwaka 2000 baada ya Gideon Senyagwa kutangaza kustaafu, alifariki dunia Agosti 6, 2025, siku mbili baada ya kufanyika kwa kura za maoni.
Dar/Dodoma. Wanachama 24 wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wamechukua fomu za kuomba ridhaa ya chama kuteuliwa kugombea ubunge katika Jimbo la Kongwa, mkoani Dodoma.
Hatua hiyo inafanyika kutokana na kufariki dunia kwa Job Ndugai, aliyekuwa miongoni mwa wanachama 20 waliochukua fomu kuwania uteuzi wa CCM katika uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025.
Baada ya mchujo wa awali uliofanywa na vikao vya juu vya chama, majina ya wagombea yalipunguzwa kutoka 20 hadi 10, likiwemo la Ndugai, na kupelekwa kwa wajumbe wa CCM kwa ajili ya kura za maoni.
Katika kura hizo, Ndugai aliongoza kwa kupata kura 5,692, akiwashinda wagombea wenzake Isaya Mngurumi (2,602), Deus Seif (1,260), Philip Chiwanga (558), Dk. Samora Mshang’a (544), Dk. Simon Ngatunga (517), Elias Mdao (435), Paschal Mahinyila (331), Balozi Emmanuel Mbennah (232), na Ngaya Mazanda (195).
Hata hivyo, Ndugai alifariki dunia Agosti 6, 2025, na alizikwa Agosti 10, 2025, kijijini kwao, wilayani Kongwa. Kutokana na msiba huo, CCM ilitangaza kuanzisha upya mchakato wa kumpata mgombea atakayeteperusha bendera ya chama katika jimbo hilo.
Jana Jumanne, Agosti 12, 2025, Katibu wa CCM Wilaya ya Kongwa, Joyce Mkaugala, alisema waliojitokeza kuchukua fomu hadi mchana walikuwa 24. Mkaugala pia alisema taratibu za chama zitafuatwa, ikiwemo kulipia Sh500,000 kwa kila fomu, na kwamba kura za maoni zitapigwa Jumapili, Agosti 17, 2025.
Mmoja wa viongozi wa chama hicho aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina, alisema idadi hiyo ni sahihi na hakuna mjumbe au mwanachama aliyejitokeza zaidi ya hao 24.
Taarifa zinaeleza kuwa baadhi ya wagombea waliokuwepo awali wamejitokeza tena, ikiwemo mmoja wa viongozi wa timu kubwa ya jijini Dar es Salaam, ingawa haijathibishwa.
Viongozi hawakutoa ufafanuzi kama kutakuwa na kampeni za kuzunguka kwa wajumbe kama awali, na walisema wanachama wasubiri maelekezo ya utaratibu.
Wilaya ya Kongwa ilizaliwa kutoka Wilaya ya Mpwapwa, Mkoa wa Dodoma, na kwa sasa inaundwa na kata 22.
Wachambuzi wanasema
Baadhi ya wachambuzi wamesema wameshangazwa na uamuzi wa CCM kuanzisha mchakato upya, huku wakidhani chama kingeendeleza na watiania waliobaki.
“Nilijua CCM ingendelea na watiania waliobaki, kama vile ilivyokuwa kwa wabunge wa viti maalumu kama ikitokea amekufa, basi wanaendelea majina yalipo kwenye orodha. Lakini kuurudia upya hali inaleta sintofahamu na kuna wingu zito nyuma yake.
“Ingetokea Ndugai amefariki dunia baada ya uteuzi wa INEC (Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi), hapo CCM ingerudia upya, lakini kwa hiki kilichotokea ni bora wangeendelea na watiania waliobaki,”ameeleza Ramadhan Manyeko.
Kwa mujibu wa Manyeko, kilichopo nyuma ya pazia CCM kuurudia upya mchakato ni kuwaridhisha wale makada waliomuunga mkono Ndugai kwa kuhakikisha jambo hilo linaanza tena hatua ya awali.
“Wakati wa kampeni za kata kwa kata za kuomba kura wajumbe, Ndugai alikuwa anazomewa au kuulizwa maswali ambayo kwa namna moja au mwenyewe (Ndugai) alisema watu hao wamepangwa au kutumwa na washinda wake,” amesema.
“Sasa ili kuwaridhisha watu wa Ndugai CCM wameamua kuanza upya ili kuweka mambo sawa, kuliko kuendeleza pale walipoishia kungezua maneno tena,”amesema Manyeko.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda amesema CCM ilitakiwa kuendeleza pale walipoishia mchakato huo badala kuurejea upya, kwa sababu kuna watu watalazimika kutoa tena Sh500,000 za fomu.
“Ninaona mambo mawili mchakato huu kurudiwa, mosi watiania wa awali wataingia hasara ya kuingia mfukoni kutoa Sh500,000 za fomu. Pili kutakuwa na kuongeza kwa demokrasia kwa watiania wapya watakaomua kuwania jimbo hilo.
“Kuna watu, enzi za uhai wa Ndugai hawakuchukua fomu kwa kumhofia au kumheshimu Spika huyo wa mstaafu, sasa kurejea upya kwa mchakato kutawaamsha kuchukua fomu za ubunge,”amesema Dk Mbunda.