Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wananchi 40,000 wanufaika na Sh57 milioni uhifadhi wa ushoroba wa Kitendeni

Mradi wa birika la kunyweshea maji mifugo lililojengwa katika Kijiji cha Lerang'wa lenye uwezo wa kunyweshea mifugo zaidi ya 1000 kwa siku.

Arusha. Zaidi ya wananchi 40,000 kutoka vijiji 11 wilayani Longido, mkoani Arusha, wamenufaika na Sh57 milioni kupitia mradi wa uhifadhi wa Ushoroba wa Kitendeni, fedha zilizotolewa kama motisha kwa ushiriki wao katika kulinda ukanda huo muhimu wa wanyamapori.

Mradi huo unaojulikana kama Wildlife Credit unatumia mfumo wa malipo kulingana na utendaji (performance-based payments), ambapo jamii hulipwa kutokana na matokeo ya uhifadhi. Ushoroba wa Kitendeni wenye ukubwa wa hekta 15,000 unaunganisha Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro na Hifadhi ya Taifa ya Amboseli, ukiwa njia kuu ya wanyamapori kama tembo, simba na twiga kuvuka mipaka ya Tanzania na Kenya.

Mradi huo unatekelezwa na World Wide Fund for Nature (WWF) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Enduimet (E-WMA), ukilenga kuokoa uhai wa ushoroba huo uliokuwa hatarini kutokana na uvamizi wa shughuli za kibinadamu.

Ofisa wa E-WMA, William Richard, amesema Ushoroba wa Kitendeni ni miongoni mwa njia mbili tu kati ya 61 za wanyamapori nchini zenye kiwango cha uhai zaidi ya asilimia 70, huku nyingi zikiwa hatarini kutoweka kutokana na uharibifu wa bioanuai.

Amesema vijiji vinavyoshiriki mradi huo ni Kitendeni, Lerang’wa, Irkaswa, Kamwanga, Ormolok, Elerai, Tingatinga, Ildonyo, Leremeta, Ildonyomali na Ngereyani.

“Mradi ulioanza mwaka jana umewezesha kuanzishwa mpango wa usimamizi wa malisho, udhibiti wa spishi vamizi na Kamati ya Usimamizi wa Ukanda wa Kitendeni. Pia kamera 36 na askari wa vijiji pamoja na watafiti raia waliopatiwa mafunzo ya SMART tools hufuatilia mienendo ya wanyamapori na vitendo haramu,” amesema Richard.

Amefafanua kuwa malipo ya motisha hutolewa kulingana na vigezo vya uwepo wa wanyamapori, kupungua kwa ukataji miti haramu, kudhibiti uvamizi wa binadamu, kuimarika kwa utawala bora na utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya jamii.

Mbali na uhifadhi, fedha hizo zimewezesha ujenzi wa birika la kunyweshea mifugo, shimo la kutupia kondo la uzazi katika zahanati ya Leremeta na ugawaji wa madawati katika shule mbalimbali.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Lerang’wa, Isaya Lembuya, amesema kijiji chao kilipokea Sh4 milioni zilizotumika kujenga birika la kunyweshea mifugo zaidi ya 1,000 kwa siku na kuhudumia wananchi zaidi ya 4,300 kwa maji.

“Kipindi cha kiangazi mifugo ilikosa maji, lakini sasa tuna miundombinu ya kuvuna maji ya mvua kwa msimu mzima,” amesema.

Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Leremeta, Dk Samson Philipo, amesema mradi huo pia umesaidia kutatua changamoto ya utupaji usio salama wa kondo la uzazi kwa wanawake wanaojifungua katika kituo hicho kinachohudumia zaidi ya wananchi 2,678.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), zaidi ya njia 41 kati ya 61 za wanyamapori nchini ziko hatarini kutoweka kutokana na uvamizi wa binadamu, ikiwemo ukataji miti, kilimo, ufugaji na maendeleo ya makazi.

Taarifa ya taasisi hiyo inaeleza kuwa hadi sasa ni ushoroba mbili tu zimepokelewa rasmi na bado zina uhai wa zaidi ya asilimia 70, ambazo ni Ushoroba wa Kitendeni unaounganisha Longido na West Kilimanjaro na ule wa Mpanga-Kipengere.