Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wananchi Kibosho wafungua barabara za mkato, wapunguza gharama za usafiri

Sehemu ya barabara ya mkato inayounganisha kata za Kibosho kati, Kibosho Mashariki na Kirima ambayo inafunguliwa na wadau wa maendeleo kwa kushirikiana na wananchi, kurahisisha usafiri na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Muktasari:

  • Wananchi wa kata za Kibosho Mashariki, Kibosho Kati na Kirima wameamua kufungua barabara za mkato ili kupunguza umbali wa safari, gharama za usafiri na kurahisisha upatikanaji wa masoko na huduma za kijamii.

Moshi. Wananchi wa kata za Kibosho Mashariki, Kibosho Kati na Kirima, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wamechukua hatua ya pamoja kufungua barabara za mkato kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, hatua inayolenga kurahisisha usafiri, kupunguza gharama na kuimarisha shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo.

Maeneo hayo yanayozalisha kwa wingi ndizi na mazao mengine ya biashara na chakula, kwa muda mrefu yamekuwa yakikabiliwa na changamoto ya miundombinu duni ya barabara, hali iliyowalazimu wananchi kutumia njia ndefu za mzunguko na kupoteza muda mwingi kufikia masoko na huduma muhimu za kijamii.

Shughuli ya kufungua barabara hizo inasimamiwa na taasisi ya Navika, inayoundwa na wadau wa maendeleo kutoka katika kata husika, ikiwa na jukumu la kuratibu michango, kusimamia utekelezaji wa kazi na kuhakikisha barabara zinafunguliwa kwa viwango vinavyowezesha mawasiliano na usafirishaji wa uhakika.

Sehemu ya barabara ya mkato inayounganisha kata za Kibosho kati, Kibosho Mashariki na Kirima ambayo inafunguliwa na wadau wa maendeleo kwa kushirikiana na wananchi, kurahisisha usafiri na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Mkazi wa kijiji cha Singa na mdau wa maendeleo, Baruti Mushi, amesema uamuzi wa kufungua barabara hizo umetokana na uhitaji mkubwa wa njia za mkato, akieleza kuwa barabara zilizokuwepo zilikuwa ndefu na hazikidhi mahitaji ya wananchi.

“Tulikuwa tunatembea zaidi ya kilometa tatu kutoka kijiji kimoja kwenda kingine. Sasa tunafungua barabara za mkato zitakazopitika pia na magari na kurahisisha usafiri,” amesema.

Ameeleza kuwa awali safari ya kutoka kijiji cha Singa kwenda Uchau ilichukua kati ya saa moja na nusu hadi mbili, lakini baada ya kukamilika kwa barabara ya mkato, safari hiyo itachukua dakika 10 pekee, hali itakayorahisisha upatikanaji wa huduma za afya, masoko na shughuli nyingine za kiuchumi.

Mkazi mwingine, Amedeus Ngawaiya, amesema barabara hiyo italeta nafuu kubwa hasa nyakati za mvua, ambapo mafuriko yalilazimu wananchi kutumia njia ndefu kwa gharama kubwa.

“Awali kutoka Masoka hadi Singa tulikuwa tunalipa zaidi ya Sh2,000 kwa bodaboda, lakini sasa kwa barabara hii ya mkato tutalipa Sh1,000 tu. Mawasiliano yamerahisishwa na gharama zimepungua,” amesema.

Akizungumza kuhusu mradi huo, Makamu Mwenyekiti wa Navika, Bahati Mamboma, amesema barabara hiyo inaunganisha kata tatu za Kirima, Kibosho Kati na Kibosho Mashariki, na imepunguza umbali wa safari kutoka zaidi ya kilometa saba kwa barabara ya mzunguko hadi kilometa moja na nusu pekee.

Amesema barabara hiyo itarahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii kama elimu na afya, kwani baadhi ya huduma hupatikana Kibosho Kati lakini hazipo Kirima, na nyingine zipo Kirima lakini hazipo Kibosho Mashariki.

“Kwa barabara hii ya mkato, wananchi watazifikia huduma hizo kwa wakati, huku wakulima wakinufaika kwa kufikisha mazao sokoni kwa urahisi,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Navika, Paul Mushi, amesema taasisi hiyo imejipanga kushirikiana na wananchi na viongozi wa vijiji katika kuondoa changamoto za barabara na vivuko.

“Tumeanza awamu ya kwanza ya kufungua barabara, na inayofuata ni ujenzi wa daraja. Kila mmoja ana mchango, hata asiye na fedha anaweza kuchangia kwa mawazo,” amesema.

Ameongeza kuwa juhudi za wananchi zitaihamasisha Serikali kuunga mkono miradi hiyo ili kuharakisha maendeleo.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Singa, Rafael Mallya, amewashukuru wananchi na wadau wote waliojitoa kuhakikisha barabara hiyo inafunguliwa, akisema itachochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika vijiji husika.

“Barabara hii itawawezesha wananchi kufika sokoni kwa haraka, vijana wa bodaboda kufanya kazi kwa urahisi na kwa ujumla kuinua shughuli za maendeleo,” amesema.