Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wananchi watakiwa kushirikiana kukomesha vifo vitokanavyo na uzazi

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi akikata utepe kuashiria kuanza kwa uzalishaji katika mgodi wa dhahabu wa Bernard Kitamala uliopo katika Kijiji cha Rwamkoma wilayani Butiama. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amewataka wananchi wa Mara kutumia huduma ya M-Mama kutokomeza vifo vya uzazi.

Butiama. Serikali mkoani Mara imezitaka jamii kushirikiana kwa karibu katika kuhakikisha wanawake wajawazito wanahudhuria kliniki ipasavyo na kutumia kikamilifu huduma ya M-Mama ili kupunguza na hatimaye kutokomeza vifo vitokanavyo na uzazi.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, Januari 19, 2026 wilayani Butiama, wakati akizungumza na wananchi kuhusu kampeni ya mkoa ya kupambana na vifo vitokanavyo na uzazi.

Kanali Mtambi amesema Serikali imeanzisha huduma ya M-Mama kwa lengo la kuwafikia wanawake wajawazito popote walipo na kuhakikisha wanapatiwa usafiri wa haraka kuwafikisha katika vituo vya kutolea huduma za afya wanapohitaji kujifungua.

Amesema dhamira ya Serikali ni kupunguza na kumaliza kabisa vifo vya uzazi kwa kuweka mazingira rafiki na salama kwa wajawazito, akisisitiza kuwa mafanikio ya lengo hilo yanahitaji ushirikiano wa jamii.

“Hakuna sababu ya mama au mtoto kupoteza maisha wakati wa uzazi. Uzazi ni baraka, hivyo wadau wote wanapaswa kushirikiana kuhakikisha baraka hiyo haibadiliki kuwa laana,” amesema.

Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Rwamkoma wilayani Butiama wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Mara kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo. Picha na Beldina Nyakeke

Ameeleza kuwa mahudhurio sahihi ya kliniki yana mchango mkubwa katika uzazi salama kwa kuwa huwapa wataalamu nafasi ya kufanya uchunguzi wa kina na kuchukua hatua za mapema endapo changamoto zitabainika.

“Kuna vifo ambavyo wataalamu wamebaini vinaweza kuzuilika kabisa endapo mama atafanyiwa uchunguzi mapema. Pia wapo watoto wanaozaliwa na ulemavu kwa sababu mama hakupata huduma za afya wakati wa ujauzito,” amesema.

Amefafanua kuwa baadhi ya tabia kama wajawazito kula udongo au mkaa mara nyingi husababishwa na upungufu wa madini mwilini, hali ambayo ingeweza kubainika mapema kupitia kliniki.

“Mjamzito akienda kliniki atafanyiwa vipimo na kupewa ushauri sahihi, wakati mwingine anaelekezwa kula vyakula kama dagaa ili kurekebisha upungufu wa madini. Huduma hizi zinatolewa bila malipo na husaidia kuepusha madhara makubwa,” amesema.

Kanali Mtambi amewataka wananchi kutumia namba ya bure 155 pindi mjamzito anapofikia hatua ya kujifungua kabla ya kufika hospitalini ili apatiwe msaada wa haraka.

Amesema simu hiyo hupokelewa na wahudumu waliopo saa 24 na baada ya kupokea taarifa, gari la wagonjwa hutumwa kumchukua mjamzito na kumfikisha katika kituo cha afya.

“Kwa maeneo yasiyo na gari la wagonjwa, Serikali imeingia mikataba na watoa huduma binafsi. Ukipiga simu, mtoa huduma wa eneo lako atawasiliana na kufika kumchukua mjamzito na kumfikisha hospitalini kwa haraka,” amesema.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amekagua maendeleo ya ujenzi wa mgodi wa dhahabu wa Bernard Kitamala uliopo kijiji cha Rwamkoma wilayani Butiama, na kuwataka wananchi kushirikiana na wawekezaji ili kuchochea maendeleo.

Mgodi huo wa wazawa, unaopata msaada wa kitaalamu kutoka kampuni ya Shuo Cheng ya China, unatarajiwa kuanza uzalishaji hivi karibuni na kuzalisha kati ya kilo 25 hadi 30 za dhahabu kwa mwezi.

Wakizungumza kuhusu kampeni ya M-Mama, baadhi ya wakazi wa wilaya ya Butiama wameishukuru Serikali, wakisema ni mkombozi kwa wanawake wajawazito, hususan wa maeneo ya vijijini.

Sospeter Mgendi amesema changamoto za huduma za afya vijijini ni kubwa ukilinganisha na mijini, hivyo kampeni hiyo inaleta matumaini mapya.

“Huku hali ni mbaya, vifo vinatokea kwa kukosa huduma. Kampeni hii ni mkombozi kwani sasa wanawake watakuwa na uhakika wa kufika hospitalini na kujifungua salama,” amesema.

Kwa upande wake, Amina Wanjiro amesema kuna haja ya Serikali kutoa elimu zaidi kwa jamii kuhusu huduma hiyo ili wananchi wengi waweze kuifahamu na kuitumia.

“Wengi hatukuijua kampeni hii. Haitoshi Mkuu wa Mkoa pekee kuitangaza; watendaji wa Serikali kuanzia ngazi ya vijiji wanapaswa kutoa elimu ili jamii iwe na uelewa na kunufaika na huduma hii kwa ustawi wa wanawake na jamii kwa ujumla,” amesema.