Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wasaidizi wa nyumbani Morogoro wafundwa juu ya haki zao

Wafanyakazi wa nyumbani wameeleza kufurahishwa na mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kujua haki na wajibu wao kazini, wakisema yamewasaidia kuelewa masuala muhimu ambayo awali hawakuwa wakiyafahamu ikiwemo mikataba ya kazi muda wa mapumziko, likizo na namna ya kupata msaada wanapokumbana na changamoto za ajira.

Wakizungumza baada ya kushiriki mafunzo hayo ya siku moja yaliyoandaliwa na  Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa kushirikiana na Chama cha kutetea watumishi wa hifadhi, majumbani, watoa huduma na wa kwenye mahoteli nchini Tanzania (Chodawu),walisema elimu waliyoipata imewafungua macho kuhusu haki zao za msingi kama wafanyakazi wa nyumbani na kuwapa uelewa wa namna ya kutekeleza wajibu wao kwa waajiri.

Mmoja wa washiriki hao, Sikudhani Fuliwa amesema kabla ya mafunzo hayo wafanyakazi wengi wa nyumbani  hawakuwa wanatambua haki zao na mara nyingi walifanya kazi bila kuwa na mikataba rasmi ya ajira.

“Tumefundishwa kuhusu umuhimu wa mikataba ya kazi, muda wa mapumziko, likizo ya ugonjwa na haki nyingine za msingi. Haya ni mambo ambayo wengi wetu hatukuwa tunayafahamu. Sasa tunatoka hapa tukiwa na uelewa mkubwa zaidi wa haki na wajibu wetu,” alisema.

Aliongeza kuwa baada ya mafunzo hayo, washiriki wamejipanga kwenda kutoa elimu kwa wafanyakazi wengine wa nyumbani ambao hawakupata fursa ya kuhudhuria ili kuhakikisha taarifa hizo zinawafikia wengi zaidi.

Kwa upande wake, Salama Rashidi alisema mafunzo hayo yamemwezesha kutambua umuhimu wa kuwa na mkataba wa kazi unaoweza kumlinda kisheria pale anapokumbana na changamoto mahali pa kazi.

“Kabla ya mafunzo haya kulikuwa na mambo mengi sikuyafahamu. Sasa nimejua haki zangu za msingi kama mfanyakazi wa nyumbani na umuhimu wa kusaini mkataba wa kazi wakati wa kuanza ajira. Mkataba huo unaweza kunisaidia kupata haki zangu endapo kutatokea changamoto,” alisema.

Alisema pia mafunzo hayo yamegusia masuala ya ukatili wa kijinsia, namna ya kujilinda pamoja na kuishi kwa maelewano na waajiri wao.

Washiriki hao walitoa shukurani kwa waandaaji wa mafunzo hayo wakisema yamewaunganisha wafanyakazi wa majumbani na kuwajengea mshikamano wa kusaidiana wanapokumbana na changamoto mbalimbali za kikazi.

Aidha, walisisitiza kuwa baada ya kurejea katika maeneo yao ya kazi watatekeleza elimu waliyoipata kwa kuzingatia wajibu wao, kuheshimu mikataba ya ajira na kuhakikisha wanajua haki zao pamoja na haki za waajiri wao.

Naye mshiriki mwingine wa mafunzo hayo, Suleiman Maulid alisema kabla ya kupata elimu hiyo alikuwa hajui kwamba wafanyakazi wa nyumbani  wanapaswa kulindwa na kuheshimiwa kama wafanyakazi wengine walioko katika sekta tofauti.

“Leo nimeelewa kuwa mfanyakazi wa nyumbani ana haki ya kulindwa na kuheshimiwa kama mfanyakazi mwingine yeyote. Nitarudi kazini nikiwa na uelewa wa haki zangu, wajibu wangu na wajibu wa mwajiri wangu,” alisema.

Washiriki walieleza kuwa elimu hiyo itachangia kuboresha mahusiano kati ya wafanyakazi wa nyumbani na waajiri wao, huku ikisaidia kupunguza migogoro inayotokana na kutofahamu haki na wajibu wa pande zote mbili.