Yas kutoa huduma za mawasiliano kwa watalii Kilifair 2026
Arusha. Kampuni ya Mawasiliano ya Yas imetumia Maonesho ya Utalii ya Karibu-KiliFair 2026 yanayoendelea jijini Arusha kuonesha uwekezaji wake katika kuimarisha huduma za mawasiliano kwenye maeneo ya utalii na hifadhi za taifa nchini, hatua inayolenga kuhakikisha watalii na wafanyabiashara wa sekta ya utalii wanapata mawasiliano ya uhakika wakati wote.
Akizungumza katika maonesho hayo, Mkuu wa Kitengo cha Mauzo kwa Wateja Wakubwa wa Yas Business, Anatory Lelo, alisema kampuni hiyo imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano na huduma za data ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya sekta ya utalii, ambayo kwa sasa inategemea kwa kiasi kikubwa teknolojia na mawasiliano ya kidigitali.
Alisema upatikanaji wa mawasiliano ya uhakika katika maeneo ya utalii unachangia kuboresha huduma kwa watalii, kurahisisha shughuli za waendeshaji wa utalii pamoja na kuongeza usalama katika maeneo ya hifadhi.
“Yas imeendelea kuimarisha mtandao wake katika maeneo ya hifadhi na vivutio vya utalii ili kuhakikisha wageni wanaotembelea Tanzania wanapata huduma za mawasiliano bila changamoto. Tunatambua kuwa mawasiliano bora ni sehemu muhimu ya uzoefu wa kisasa wa mtalii,” amesema Lelo.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Yas Kanda ya Kaskazini, Robert Sanyagi, alisema kampuni hiyo imehakikisha huduma za sauti na data zinapatikana katika maeneo mengi ya utalii nchini, jambo linalowezesha watalii kuendelea kuwasiliana na familia, marafiki na wadau wengine hata wanapokuwa ndani ya hifadhi.
“Watalii na wafanyabiashara wa sekta ya utalii hawapaswi kuwa na wasiwasi kuhusu mawasiliano wanapotembelea maeneo mbalimbali ya hifadhi. Yas imeendelea kuboresha mtandao wake ili kuhakikisha huduma zinapatikana katika maeneo muhimu ya utalii nchini,” alisema Sanyagi.
Baadhi ya wageni waliotembelea banda la Yas katika maonesho hayo pia walieleza kuridhishwa na huduma zinazotolewa na kampuni hiyo, hususan huduma za data na suluhisho za kidigitali zinazorahisisha mawasiliano na shughuli za biashara.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, Yas kwa sasa ina zaidi ya minara 4,800 ya mawasiliano ya 4G na 5G nchini, ikiwa ni takribani minara 1,000 zaidi ya mshindani wake anayefuata. Uwekezaji huo umechangia kuongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo mbalimbali ya mijini na vijijini, ikiwemo maeneo ya utalii.
Kupitia ushiriki wake katika KiliFair 2026, Yas imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kusaidia ukuaji wa sekta ya utalii kwa kuwezesha mawasiliano ya uhakika na huduma za kidigitali zinazochangia kuboresha uzoefu wa watalii wanaotembelea Tanzania.