Kamishna Hamad: Hakuna sheria inayokataza watu kula mchana Z'bar
Muktasari:
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamad Khamis Hamad amesema kuna vijana waliokuwa wanavuta bangi mchana, akaagiza wakamatwe
Unguja. Sakata la watu kukamatwa kwa kosa la kula mchana wakati mwezi wa Ramadhan likiendelea kutikisa visiwani Zanzibar, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamad Khamis Hamad ametoa ufafanuzi wa suala hilo akisema hakuna sheria inayokataza watu kula mchana.
Kamishna Hamad ametoa ufafanuzi huo kutokana na watu 12 kukamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi wakidaiwa kula na kunywa hadharani katika maeneo ya viwanja vya Mnazimmoja na kuibua mjadala.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari leo Aprili 2 2024, Kamishna Hamad amesema kula mchana mwezi wa Ramadhani si kosa la jinai ingawa hilo linaweza kufanyika kwa kuheshimu wengine.
“Kuna maelekezo kuheshimu, kula hadharani watu wamefunga ni kama vile umewakwaza wengine lakini kuna sehemu ambazo zimeelekezwa watu wanakula,” amesema Hamad.
Taarifa za kukamatwa kwa watu hao kwa tuhuma za kula mchana wakati wa mwezi wa Ramadhan zilitolewa Machi 28, 2024 na Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa Mjini Magharib, Abubakar Khamis.
Kamishana Hamad amesema alipokea video fupi kutoka wa mmoja wa viongozi wa Serikali kuhusu watu wanaovuta bangi hadharani,hivyo akamuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi wakawakamate.
“Kwa sababu bangi haijaruhusiwa Zanzibar, nilimpa taarifa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharib ambaye ndio mwenye himaya hiyo na kumpa maelekezo washughulikie tatizo hilo kwa sababu, watu kama wanakaa mchana wanavuta bangi wanaona kama sisi hatupo.
“Nadhani inaweza kuwa changamoto katika utoaji wa taarifa, lakini ni yeye (Kamanda wa Polisi) anaweza kutoa ufafanuzi zaidi kwamba ni wale waliokuwa wanavuta bangi au kuna watu wengine,” amesema.
Mwananchi lilipomtafuta Kaimu Kamanda wa Polisi, Abubakar Khamis aliyetoa taarifa za kukamatwa watu hao kuhusu hatua zilizochukuliwa mpaka sasa, amesema watu hao wamepata dhamana na suala lao linaendelea na uchunguzi.
Alipoulizwa iwapo kuna watu waliokuwa wanakula chakula au ni hao waliokuwa wanavuta bangi, amesema haikuthibitika mara moja.
“Haikuthibitika kwa haraka sana kwa sababu pale ilikuwa ni taarifa za wananchi pengine walipoona wanafanya vitendo hivyo wakadhani wanakula moja kwa moja maana watu wale walikuwa sehemu ya kijiweni, uchunguzi bado unaendelea.
“Sasa lile tukio lilileta taharuki kidogo kuonekana wanavuta bangi hadharani wakati wa mchana, baada ya clip kurushwa mtaani na wananchi wakalalamikia hilo ndio ikasababisha kukamatwa kwao na uchunguzi bado unaendelea,”
Amesema upelelezi utakapokamilika watapeleka jalada kwa mwanasheria ikionekana kuna makosa watapelekwa mahakamani.