Rais Mwinyi ashiriki mazishi ya mbunge aliyefariki ghafla

Naibu Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu , akiweka udongo kwenye kaburi la aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kwahani,  Ahmed Yahya Abdulwakil jana Aprili 9, 2024 Kijiji cha  Muyuni Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.

Muktasari:

 Aprili 8, 2024, Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson alilitangazia Bunge juu ya kifo cha Mbunge wa Kwahani (CCM), Ahmed Yahya Abdulwakil kilichotokea ghafla kwa kwa shinikizo la damu

Unguja. Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi amewaongoza wananchi na viongozi katika mazishi ya aliyekuwa mbunge wa Kwahani (CCM), Ahmed Yahya Abdulwakil yaliyofanyika kijijini kwao Muyuni Mkoa wa Mjini Magharibi.

Marehemu Yahya aliyekuwa na umri wa miaka 65 alifariki Aprili 8, 2024 na kifo chake kilitajwa kilitokana na shinikio la damu. Marehemu ameacha wajane wawili na watoto 17.

Akisoma wasifu wa marehemu wakati wa maziko hayo jana jioni, Aprili 9, 2024 Katibu mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Magharibu, Awadhi haji amesema marehemu atakumbukwa kwa jinsi alivyokuwa akishirikiana na wananchi na viongozi wengine katika kuwaletea maendeleo.

Amesema katika utumishi wake ameshika nyadhifa mbalimbali tangu alipojiunga na CCM mwaka 1968 akiwa chipukizi wa Afro Shiraz Party na baadaye akajiunga rasmi CCM mwaka 1977.

Amesema katika utumishi wake alikuwa mjumbe wa baraza la wawakilishi mwaka 2017/20 na katika Uchaguzi Mkuu aligombea ubunge katika Jimbo la Kwahani na kuibuka mshindi.

Jimbo hilo awali, lilikuwa linaongozwa na Dk Mwinyi ambaye mwaka 2020 alipitishwa na CCM kugombea nafasi ya Urais.

Naibu Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu , akimuwakilisha Spika wa Bunge,  Dk Tulia Ackson katika mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kwahani,  Ahmed Yahya Abdulwakil yaliyofanyika  jana Aprili 9, 2024 Kijijini kwao Muyuni Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.

“Alikuwa mtu wa kujitoa na ushirikiano na wananchi wake, kwa hiyo atakumbukwa kwa aliyoyafanya,” amesema Awadh.

Akitoa salamu za Serikali ya Tanzania, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusuf Masauni amesema ni pigo kubwa kwa sababu alikuwa na ushirikiano mkubwa bungeni hata kwa upande wa Serikali.

“Alionyesha upendo mkubwa na alikuwa mtu wa kujitoa,” amesema Masauni.

Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera Uratibu na Baraza la wawakilishi kwa niaba ya Serikali ya Mpinduzi, Hamza Hassan Juma amesema marehemu alifanya shughuli nyingi za maendeleo kisiwani hapo.

Amesema amejenga majengo mbalimbali katika maeneo mbalimbali ndani ya jimbo lake na nje ya jimbo lake, hivyo atakumbukwa kwa kujitoa kwake.

“Ni jambo la kushukuru kwa wema wake, tutazidi kumkumbuka kwani alikuwa anajitoa sana kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wake na Taifa kwa jumla,” amesema Hamza.

Baadhi ya wananchi wa jimbo hilo wamesema wamepoteza mtu muhimu aliyekuwa akiwapigania katika maendeleo.

“Tumepoteza, japo kazi ya Mungu haina makossa, lakini tutamkumbuka kuleta maendeleo ya miundombinu katika jimbo letu, tunaomba Mungu ampokee,” amesema Saleh Mtumwa

Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Zungu alishiriki mazishi hayo kwa niaba ya Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.