Ajira za staha 70,000 kuratibiwa Zanzibar
Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji, Shaaban Ali Othman akisoma makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo katika mkutano wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Unguja Zanzibar
Muktasari:
- Ajira hizo zinatarajiwa kuwawezesha wananchi 28,339 kiuchumi kwa kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu yenye thamani ya Sh47.3 bilioni.
Unguja. Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji imekuja na vipaumbele vinane ikiwemo kuratibu upatikanaji wa ajira za staha 70,000 kwa wote kwa kushirikiana na wadau ndani na nje ya nchi.
Pia, kuwawezesha wananchi 28,339 kiuchumi kwa kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu yenye thamani ya Sh47.3 bilioni.
Hayo yamebainishwa leo Juni 6, 2026 na Waziri mwenye dhamana, Shaaban Ali Othman wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo Barazani Chukwani Unguja Zanzibar.
Waziri Shaaban amesema katika mwaka wa fedha 2026/27 ili kutekeleza vipaumbele hivyo, ameliomba baraza la wawakilishi kuidhinisha Sh19 bilioni.
“Wizara itaratibu upatikanaji wa ajira za staha 70,000 kwa wote kwa kushirikiana na wadau ndani na nje ya nchi,” amesema Shaaban
Shaban amesema katika kipindi hicho, wataratibu na kusimamia shughuli za maendeleo ya vijana nchini na kuwawezesha vijana kwa kuwajengea uwezo ili kuimarika kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Pia, kuimarisha mabaraza ya vijana kiutendaji na kuhamasisha ushiriki na ushirikishwaji wa vijana katika fursa mbalimbali kupitia ngazi za kitaifa, kikanda na kimataifa.
Ametaja kipaumbele kingine ni kuimarisha maendeleo ya vyama vya ushirika nchini, kuimarisha na kuanzisha mifumo ya kielektroniki yenye kusomana kwa ukusanyaji wa taarifa (Kanzidata).
Kuwawezesha Wananchi 28,339 kiuchumi kwa kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu yenye thamani ya Sh47.3 bilioni.
Kuandaa na kufanya mapitio ya Sera, Sheria, kanuni, miongozo na mikakati ya Wizara pamoja na kuimarisha ufanyaji wa tafiti, ufuatiliaji na tathmini na kuimarisha uhusiano na mashirikiano kati ya Wizara, Taasisi, Wadau wa ndani na nje ya nchi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi na Uwekezaji, Makame Mohamed Sufiani amesema kamati inaishauri wizara kutoa takwimu halisi juu hali iliyofikiwa hivi sasa kuhusu matokeo ya kimkakati huo ili jamii iweze kufahamu juhudi za serikali katika kukabiliana na suala la ajira kwa vijana.
Mpango wa maendeleo wa Zanzibar umeweka mikakati madhubuti ya kujenga mazingira rafiki na wezeshi kwa maendeleo na ustawi kwa vijana ambapo miongoni mwa mikakati hiyo ni kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kutoka asilimia 19 kwa mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 10 kwa mwaka 2025.
“Kamati inaishauri wizara kuwa na mpango mkaakti wa muda mrefu wa kufanya tafiti mbalimbali kuhusu changamoto zinazowakabili vijana nchini.
Pia kamati imeishauri serikali ifanye maabdiliko ya sera ya vijana kwani sera hiyo ni ya zamani ili iweze kuendana na wakati.
Kingine kilichoshauriwa, wizara kuhakikisha kuwa inasimamia ipasavyo changamoto zilizzopo katika taraibu za kusajili vikundi vya ushirika ikiwemo uhaba wa maofisa wa ushirika katika wilaya ili kuona kuwa vikundi hivyo vinaendesha shughuli zake kwa mujibu wa sheria.
Pia kamati imeishauri wizara kuharakisha kuanzisha mfumo maalumu utakaotumika katika kufanya uhakiki wa marejesho ya mikopo kutoka kwa wadau wanaopatiwa huduma hiyo.