Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Askofu Bagonza: Serikali ni mali ya wananchi

Askofu Benson Bagonza akiwasilisha mada katika mkutano wa Demokrasia uliofanyika Mjini Unguja.

Muktasari:

  • Vijana ambao si wanachama wa vyama vya siasa ni wengi kuliko waliomo ndani ya vyama, hivyo kuna haja ya kutafakari namna ya kuwashirikisha katika masuala ya uongozi na demokrasia.

Unguja. Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Benson Bagonza amesema ujenzi wa taifa lenye misingi imara ya demokrasia unapaswa kuanzia katika kubadili mtazamo kwamba, Serikali ni mali ya wananchi, badala ya wananchi kuonekana kuwa mali ya Serikali.

Askofu Bagonza ametoa kauli hiyo leo Alhamaisi, Julai 9, 2026, mjini Unguja alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu Elimu ya Uraia, Uongozi na Siasa, kwenye kongamano la kisiasa na kisheria lililofanyika Zanzibar, likiwakutanisha viongozi wa vyama vya siasa, asasi za kiraia, wanaharakati na wananchi kujadili masuala ya demokrasia, utawala bora na haki za binadamu.

"Wengi wanaamini kuwa wananchi ni mali ya Serikali. Tubadilishe mtazamo huo. Serikali ndiyo mali ya wananchi. Tukikubaliana hapo, tutakuwa tumeweka msingi wa kujenga taifa letu," amesema.

Akizungumzia ushiriki wa vijana katika siasa, Askofu Bagonza amesema kwa mtazamo wake, vijana wengi wanajikuta wakitengwa na michakato ya kisiasa kwa sababu mfumo uliopo unawalazimu kuwa wanachama wa vyama vya siasa ili waweze kushiriki kikamilifu.

Amesema vijana ambao si wanachama wa vyama vya siasa ni wengi kuliko waliomo ndani ya vyama, hivyo kuna haja ya kutafakari namna ya kuwashirikisha katika masuala ya uongozi na demokrasia.

Kwa mujibu wake, hali hiyo huwafanya wengi kupoteza fursa ya kugombea nafasi za uongozi na kubaki na haki ya kupiga kura pekee.

Aidha, amesema baadhi ya vijana hukata tamaa kushiriki katika uchaguzi kutokana na kile alichodai kuwa ukosefu wa imani katika mifumo ya uchaguzi pamoja na gharama kubwa za kufuatilia haki zao kupitia vyombo vya sheria.

"Matokeo yake ni kwamba vijana wengi huamua kutopiga kura wala kugombea nafasi za uongozi. Wengine huishia kutumiwa na wanasiasa na vyama vya siasa kutekeleza masilahi ambayo si yao," amesema.

Washiriki katika mkutano wa demokrasia uliofanyika Mjini Unguja.

Askofu Bagonza amesema pia fursa za uongozi mara nyingi huwafikia vijana wachache wenye uwezo wa kumudu gharama na vikwazo vya kisiasa, huku akisisitiza kuwa Tanzania ina vijana wengi wenye vipaji vya uongozi ambao hawapati nafasi ya kuonyesha uwezo wao.

Amesema uzoefu wake wa kukutana na viongozi wa vijana unaonyesha kuwa baadhi yao wanaogopa kutoa mawazo yao kwa sababu ya mazingira yaliyopo.

Kwa maoni yake, mfumo wa elimu nao unahitaji maboresho ili uwajenge vijana wenye uwezo wa kufikiri kwa kina, kuhoji na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.

"Elimu ya uraia inapaswa kumsaidia kijana kuhoji kuliko kupongeza, kushiriki kuliko kujitenga, kujiamini kuliko kutegemea viongozi, kuwajibika na kuwawajibisha viongozi, pamoja na kutetea haki badala ya kutetea watu au vyama," amesema.

Kuhusu siasa, Askofu Bagonza amesema kushiriki katika siasa ni haki ya kila mwananchi kwa kuwa uamuzi wa kisiasa huathiri maisha ya kila siku ya wananchi wote.

Amewataka Watanzania kutonyanyapaa siasa, akisema kufanya hivyo kunaweza kuacha nafasi ya maamuzi muhimu kufanywa bila ushiriki mpana wa wananchi.

Pia, amewataka viongozi kuwapa vijana nafasi ya kujifunza na kufanya makosa bila kukumbana na vitisho au adhabu zisizo za lazima.

"Vijana wa leo hawahitaji hotuba, matamasha, fulana, kofia au ahadi pekee. Wanahitaji kuaminiwa, kusikilizwa na kupewa nafasi ya kujifunza kupitia uzoefu," amesema.

Akichangia mada hiyo, Almas Mohamed Ali amesema ushirikishwaji wa vijana katika kila hatua ya maamuzi ya kisiasa ni muhimu kwa ustawi wa demokrasia na amani nchini.

Amesema viongozi wanapaswa kujenga daraja la mawasiliano kati yao na vijana ili kuhakikisha maoni yao yanasikilizwa na kuzingatiwa katika maamuzi yanayowahusu.

Kwa upande wake, David Manyerere amesema mfumo unaoruhusu ushiriki mpana wa wananchi, ikiwamo kupitia mgombea binafsi, unaweza kuongeza fursa za uongozi na ushindani wa kidemokrasia.

Amesisitiza kuwa mafanikio ya maridhiano ya kisiasa yanategemea ushirikishwaji wa makundi yote ya jamii, hususan vijana, ili maamuzi yanayofikiwa yaakisi mahitaji na matarajio yao.

"Nchi inaweza kufika salama ikiwa viongozi watakuwa tayari kuwasikiliza vijana na kuyapa nafasi mawazo yao katika maamuzi yanayohusu mustakabali wa taifa," amesema.