Changamoto uhifadhi bahari zaundiwa jukwaa Zanzibar
Ofisa Mdhamini Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Pemba, Dk Salim Mohamed Hamza akizungumza wakati kuzindua jukwaa la wadau wa bahari Kaskazini-Mashariki mwa Kisiwa cha Unguja Zanzibar.
Muktasari:
- Changamoto hizo ni pamoja uharibifu wa mikoko, uchafuzi wa maji, athari za mabadiliko ya tabianchi na ushiriki mdogo wa jamii.
Unguja. Jukwaa maalumu la wadau wa eneo la bahari ya Kaskazini-Mashariki mwa Kisiwa cha Unguja, limezinduliwa kwa lengo la kuratibu na kusimamia uendelezaji wa shughuli endelevu za bahari, kufuatia kubainika kwa changamoto na fursa zinazopatikana katika eneo hilo.
Miongoni mwa changamoto zilizotambuliwa ni uharibifu wa mikoko, uchafuzi wa maji, athari za mabadiliko ya tabianchi na ushiriki mdogo wa wananchi katika uamuzi kuhusu uhifadhi wa mazingira ya bahari.
Jukwaa hilo limeanzishwa kupitia mradi wa Pamoja Tuhifadhi Bahari Yetu, unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya na kutekelezwa na Umoja wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira na Maliasili (IUCN) kwa gharama ya euro milioni 11.4, sawa na zaidi ya Sh33.3 bilioni.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa eneo hilo lina fursa mbalimbali zikiwamo uvuvi endelevu, utalii wa bahari, uwekezaji, utafiti, ajira kwa vijana na maendeleo ya jamii za pwani.
Akizungumza leo Alhamisi, Julai 16, 2026, wakati wa uzinduzi wa jukwaa hilo mjini Unguja, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Zahro Kassim Al-Harous kupitia hotuba iliyosomwa na Ofisa Mdhamini wa wizara hiyo Pemba, Dk Salim Mohamed Hamza, amesema hatua hiyo imekuja kwa wakati muafaka.
"Jukwaa hili linakuja muda muafaka. Huu ni ushahidi kwamba sasa tunaimarisha zaidi juhudi hizi kwa kuunganisha nguvu, maarifa na rasilimali zetu katika mfumo mmoja wa ushirikiano," amesema.
Amesema majukwaa ya aina hiyo yataimarisha uratibu wa shughuli za uhifadhi wa bahari, kuboresha mawasiliano kati ya Serikali na wadau, kuwezesha kubadilishana uzoefu na kuhakikisha maamuzi yanayofanywa yanazingatia masilahi ya wananchi, maendeleo ya uchumi wa buluu na uhifadhi wa mazingira.
Ameongeza kuwa jukwaa hilo limejengwa katika misingi ya ushirikishwaji na uwajibikaji kupitia kamati kuu, sekretarieti, kamati ya utendaji na kamati za kiufundi.
Kwa mujibu wake, hatua hiyo ni muhimu katika kujenga mfumo imara wa usimamizi wa rasilimali za bahari unaozingatia kwa pamoja maslahi ya wananchi, mazingira na maendeleo ya uchumi.
"Dira ya uchumi wa buluu ni kuona bahari ya Zanzibar inaendelea kuwa chanzo cha ustawi wa wananchi. Pia tunashirikiana na Great Global Initiative, ambayo inalenga kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 angalau asilimia 30 ya maeneo ya bahari yanakuwa yamehifadhiwa," amesema.
Kwa upande wake, Msimamizi Mkuu wa Mradi wa Pamoja Tuhifadhi Bahari Yetu, Dk Igulu Mathias amesema mradi huo unalenga kuimarisha uhifadhi wa rasilimali za bahari, misitu ya ukanda wa pwani, matumizi endelevu ya bidhaa za plastiki pamoja na kuboresha tafiti na takwimu.
Amesema pia unakusudia kuimarisha sera zinazosimamia mnyororo wa thamani wa bidhaa za plastiki kwa kushirikiana na taasisi za utafiti na zile zinazoshughulikia uhifadhi ili kuhakikisha zinapata nyenzo zinazohitajika kusimamia rasilimali hizo kwa ufanisi.
Dk Igulu amesema mradi huo wa miaka minne, unaotekelezwa kuanzia mwaka 2024 hadi 2028, kwa bajeti ya euro milioni 11.4, sawa na zaidi ya Sh33.3 bilioni.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Uhifadhi wa Bahari Zanzibar, Dk Makame Omar Makame amesema kuanzishwa kwa jukwaa hilo kunatokana na uelewa wa pamoja kwamba rasilimali za bahari na ukanda wa pwani ni nguzo muhimu ya maisha na maendeleo ya wananchi wa Zanzibar.
"Bahari yetu inatoa ajira, chakula, kipato na fursa mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kimazingira," amesema.
Naye mkulima wa mwani kutoka Kidoti, Rukia Haji Juma amesema jamii zinazoishi maeneo ya pwani zinaendelea kunufaika na bahari kupitia shughuli za kiuchumi, huku zikijengewa uelewa wa umuhimu wa kuhifadhi mazingira ya bahari kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.