CUF yajipanga kurejea kuwa chama kikuu cha upinzani, kuwaunganisha wanachama

Muktasari:
- CUF kilikuwa chama kikuu cha upinzani visiwani Zanzibar, lakini kilipoteza nguvu yake baada ya kukumbwa na migogoro ya mara kwa mara na kusababisha Maalim Seif Sharif Hamad kukihama chama hicho.
Pemba. Chama cha Wananchi (CUF) kimesema kitafanya tathmini ya kina ili kuhakikisha wanasimamisha wagombea wenye sifa na uzalendo, huku kikijipanga kurejea kwenye nafasi yake ya kuwa chama kikuu cha upinzani nchini.
Akizungumza na viongozi na wanachama wa chama hicho kutoka wilaya nne za Pemba, leo Julai 10, 2025, Samail Gombani, baada ya uzinduzi wa ofisi ya uratibu ya chama hicho, Katibu Mkuu wa CUF, Husna Mohamed Abdalla, amesema chama kimejipanga kusimamisha wagombea wenye sifa ili kiwe na nguvu na uwezo wa kuwatumikia wananchi na Taifa.
Amesema chama hakitowapa nafasi viongozi wanaoweka mbele maslahi yao, kwani baadhi ya viongozi wakipata nafasi wanakuwa wanajinufaisha wao wenyewe na si kuwatumikia wananchi.
Pia amesema chama kitafanya ubembuzi wa kina kwa mgombea ili kufahamu ukuaji wake na tabia zake, kwa lengo la kuwapata wagombea wazalendo wenye uwezo watakaojali maslahi ya wananchi.
“CUF tumejipanga kusimamisha wagombea wenye sifa watakaojali maslahi ya wananchi, si wale wanaojali maslahi yao binafsi. Wananchi watakuwa na kazi ya kufahamu tabia na mwenendo wake kuhakikisha tunasimamisha wagombea wenye sifa,” amesema.
Pamoja na hayo, katibu mkuu huyo amesema chama hicho kitawapa kipaumbele wanawake watakaojitokeza kuchukua fomu katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwemo ubunge, uwakilishi na udiwani.
“Chama kimejipanga kuwaondolea vikwazo vyote ambavyo vinaweza kujitokeza, kuona wanawake hawatakuwa nyuma kuwania nafasi hizo kwenye ngazi mbalimbali,” amesema.
Katibu huyo ameeleza kuwa cuf bado haijafa, badala yake kimepitia changamoto, kwa sasa wanarejea wakiwa imara na kuwaunganisha wanachama wake kuelekea uchaguzi mkuu.
Pia, Husna amesisitiza mshikamano na maandalizi ya mapema kuelekea uchaguzi mkuu, huku akihimiza viongozi kufufua matawi yote yaliyolala na kusogeza chama karibu zaidi na wananchi.
Awali, Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Wilaya wa CUF kisiwani Pemba, Mbwana Ali Mbwaba, amesema tayari mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu kwa nafasi za ngazi zote umeanza, na wanachama wamejitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa Habari wa CUF, Ali Rashid Abarali, amewataka wanachama ambao ni wajumbe watakaoshiriki kuwapigia kura watia nia, kuwa ni wajumbe kutoka tawi husika ili atakayechaguliwa awe ni kutoka jimbo lililokusudiwa.
“Tunataka wajumbe watakaowapigia kura wawe ni wajumbe wa tawi husika. Hapo ndipo watakuwa na uchungu yupi mwenye sifa na uwezo wa kuwatumikia wananchi na siyo chama,” amesema.
Naye Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa, Hasina Mohammed Sharif, amewataka wanawake kujitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi bila ya kuogopa, kwani wanachama wote wana haki.
Pia ametumia fursa hiyo kuwataka wanachama pamoja na wananchi wote kujitokeza kwa wingi katika kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu ujao Oktoba 2025, ili kupata viongozi bora watakaoliongoza Taifa.