Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Mwinyi: Utoaji haki haupaswi kutegemea teknolojia pekee

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akizungumza wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa 26 wa Chama cha Wanasheria na Mawakili Zanzibar (ZLS) Unguja Zanzibar.

Muktasari:

  • Imeelezwa kuwa, Teknolojia iwe chombo cha kuimarisha ufanisi, si sababu ya kuondoa utu, usawa na imani ya wananchi kwa taasisi za sheria.

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesisitiza kuwa mafanikio ya mfumo wa utoaji haki haupaswi kutegemea teknolojia pekee, bali unahitaji misingi imara ya uadilifu, uwajibikaji na uzalendo kati ya watendaji wa sekta ya sheria.

Kauli hiyo ameitoa leo Jumapili, Juni 7, 2026, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 26 wa Chama cha Wanasheria na Mawakili Zanzibar (ZLS), unaoongozwa na kauli mbiu isemayo: “Kuikumbatia Teknologia ya Kidijitali kwa Ajili ya Mfumo Bora na Unaofikika kwa Utoaji wa Haki Zanzibar.”

Dk Mwinyi amesema: “Teknolojia iwe chombo cha kuimarisha ufanisi, si sababu ya kuondoa utu, usawa na imani ya wananchi kwa taasisi za sheria. Tuendelee kuijenga Zanzibar yenye mfumo wa sheria unaoaminika na unaowafikia wananchi wote bila ubaguzi.”

Amebainisha kuwa, mfumo wa haki unaotumia teknolojia kwa ufanisi, unaweza kuwafikia wananchi wengi zaidi, wakiwamo wale waliopo maeneo ya mbali jambo linalosaidia kupunguza ucheleweshaji wa mashauri, gharama za huduma na vikwazo vya upatikanaji wa haki.

“Serikali inaamini kuwa utawala wa sheria ni msingi wa maendeleo, amani na ustawi wa Taifa lolote. Taifa haliwezi kujenga uchumi imara, kuvutia wawekezaji wala kuimarisha mazingira ya biashara ikiwa wananchi na wawekezaji hawana imani na mfumo wetu wa utoaji haki,” amesema.

Amewataka mawakili kuwa mabalozi wazuri kwa wawekezaji, kwa kuzingatia uadilifu, weledi na uwezo wa kutoa ushauri wa kitaalamu unaoimarisha mazingira salama na ya kuaminika kwa biashara.

“Taaluma ya sheria ni ya heshima kubwa na inahitaji uadilifu na uwajibikaji wa hali ya juu. Mawakili mnapaswa kuwa washauri wazuri wa kisheria na walinzi wa haki, si watu wa kutumia taaluma yenu kwa maslahi binafsi,” amesema Dk Mwinyi.

Awali, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdalla amesema Mahakama ya Zanzibar tayari imetengeneza mifumo ya kidijitali ya usimamizi na usikilizaji wa mashauri na ilifanya majaribio mwezi uliopita kuhamasisha mawakili kutumia mifumo hiyo.

Amesema pia, majaji wanatakiwa kuwa na kompyuta za kuchapa mwenendo wa kesi na vifaa vya kurekodia sauti na video.

Rais wa ZLS anayemaliza muda wake, Joseph Shaaban Magazi amesema ni wajibu wa chama kuhakikisha teknolojia inatumika kuboresha utoaji wa huduma za sheria na haki kwa wananchi wa Zanzibar, sambamba na mabadiliko ya kidijitali yanayofanyika duniani.

Mkufunzi kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo, Profesa Zakayo Lukumay amesema mfumo wa haki lazima uongoze teknolojia, si teknolojia iongoze mfumo huo.

Mkuu wa Usalama na Haki kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini, Alex Beck amesema mageuzi ya kidijitali si tu kuanzisha teknolojia mpya, bali ni fursa ya kutafakari upya namna bora ya kutoa haki.

Amesema Uingereza imekuwa ikishirikiana kwa karibu na mfumo wa Mahakama wa Zanzibar, ikiwamo uundaji wa dashibodi mpya zinazorahisisha ukusanyaji na matumizi ya taarifa kwa pamoja kwa taasisi mbalimbali.